Na
Khamisuu Abdallah
MKUTANO
mkuu wa tatu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), uliofanyika mwishoni mwa
wiki iliyopita umeshindwa kuwapata viongozi wanne wa kitaifa, kutokana na utata
wa kikatiba.
Mkutano
huo uliofanyika ukumbi wa sanaa Rahaleo, pamoja na mambo mengine uliambatana na
uchaguzi mkuu wa viongozi wa kuliongoza Shirikisho hilo kwa miaka mitano ijayo.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Katibu Mkuu wa ZATUC, Khamis Mwinyi Mohammed,
alisema nafasi zilizoshindwa kujazwa ni Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti,
Mwenyekiti wa wanawake na Mwenyekiti wa vijana.
Alisema
sababu zilizosababisha nafasi hizo kushindwa kujazwa ni pamoja na utata wa
kikatiba, ambapo mshindi anatakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Alisema
wagombea wote wameshindwa kufikia kiwango hicho na katiba haikutoa maelezo
yoyote kuhusu hatua za kuchukua.
“Hakuna
mizengwe iliyotokea kama watu wanavyosema,
uchaguzi lazima uendeshwe kwa kwa kanuni na kanuni yetu inaelekeza hivyo, hichi
ndicho kilichosababisha kushindikana kupatikana viongozi,” alisema.
Alisema
ZATUC italazimika kuitisha uchaguzi katika kipindi cha ndani ya miezi mitatu
ijayo.
Alisema
baraza kuu la ZATUC limemteua Zaharan Mohammed Nassor kuwa Kaimu Mwenyekiti
hadi uchaguzi utakapofanyika.
Aidha
aliwataka wanachama kutumia busara pale kunapojitokeza tatizo ili kuepusha
migogoro.
No comments:
Post a Comment