Na Mandishi Wetu
USHIRIKIANO
wa pamoja unahitajika baina ya jeshi la Polisi Zanzibar na wadau wa utalii ili
kukomesha vitendo vya uhalifu dhidi ya watalii.
Akizungumza
na viongozi wa Jumuiya ya wawekezaji wa sekta ya utalii Zanzibar (ZATI) na
Jumuiya ya watembeza watalii (ZATO) ofisini kwake Ziwani mjini Unguja, Kamishna
wa Polisi Zanzibar, CP Hamdan Omar Makame, alisema sekta ya utalii inakabiliwa
na changamoto kubwa ya uhalifu.
Alisema
utalii una mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi hivyo ni lazima wadau wote
wajipange ili malengo yaliyokusudiwa yafikiwe.
“Asilimia
80 ya mapato ya serikali yanatokana na utalii,” alisema.
Alisema
kukiwa na ushirikiano wa dhati baina ya taasisii hizo na jeshi la polisi kutapunguza
mwanya kwa wahalifu kushambulia watalii.
“Tafadhalini
msinipe nafasi ya kupumzika, wakati matukio yapo nipigieni simu hata usiku wa
manane, tukio la uhalifu likitokea saa mblili usiku lisifikishwe asubuhi, toeni
taarifa mapema kabla halijaathiri nami nakuhakikishieni polisi watafika mapema
kwenye eneo la tukio”, alisema.
Alitumia
fursa hiyo kuziomba taasisi hizo kulisaidia jeshi la polisi vifaa vya kisasa
vinavyoendana na teknolojia iliopo zikiwemo radio za digitali na kamera zitakazoliwezesha
kumuona askari akiwa katika eneo lake la kazi alilopangiwa.
Aidha
aliwataka kuweka kamera maalum kwenye magari yanayobeba watalii ambazo zitanasa
matukio yote yanayofanywa dhidi ya watalii.
Aliwahimzwa
wamiliki wa mahoteli kuweka kamera za usalama (CCTV) ndani na nje ya hoteli ili
kunasa picha za wahalifu.
Akizungumzia
sababu zinazochangia uvunjifu wa amani hasa katika sekta ya utalii, alisema
ukosefu wa ajira kwa vijana huchangia vitendo vya uhalifu.
Nae
Kamishna wa Kamisheni ya Utalii kutoka sekta binafsi, Hassan Ali Mzee, alisema kamisheni
ina uhisiano mzuri wa kidipolomasia na balozi zote ambazo nchi zao zinaleta
watalii.
Alisema
uhalifu unapotokea Kamisheni inapata picha mbaya kutoka ofisi za kibalozi, hivyo
aliliomba jeshi la polisi kuunda kikosi kazi kitakachopewa nguvu ya kudhibiti
uhalifu dhidi ya watalii.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya watembeza watalii, Khalifa Mohammed Makame, alisema usalama ni
uhai kwa sekta ya utalii na kuviomba vyombo vya usalama likiwemo jeshi la polisi
kushirikiana na sekta binafisi hasa watembeza watalii.
Mwenyekiti
wa bodi ZATO, Naila Jidawi, alisema
vitendo vya uhalifu vinachangia kupunguza idadi ya watalii.
No comments:
Post a Comment