Na Khamis Haji, OMPR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewazindua wasomi na wataalamu wa Zanzibar wawe na kawaida ya kufanya tafiti mara kwa mara, zitakazosaidia kuinua hali za maisha ya wananchi na kukuza maendeleo ya nchi yao.
Akizindua maabara za utafiti wa mazao ya Kilimo katika kituo cha Kizimbani Unguja, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif amesema tabia ya baadhi ya wasomi kufanya tafiti kwa ajili ya kupata shahada na baadaye kuzifungia kwenye mabakati haisaidii jamii, wala nchi yao.
“Natoa wito kwa wasomi na wataalamu wa fani mbali mbali Zanzibar, jikiteni katika kufanya tafiti ambazo zitawanufaisha wananchi kuondokana na umasikini na kukuza maendeleo ya nchi yenu”, alihimiza Makamu wa Kwanza wa Rais.
Amesema huko nyuma wasomi wengi na hata Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hawakuwa na uhakika wa fedha za kufanikisha tafiti, lakini hivi sasa kuna fursa nyingi ikiwemo kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH, ambayo inaendelea kufadhili masomo na tafiti za maeneo tafauti.
“Ni lazima watafiti wetu wafanye kila bidii kuhakikisha kwamba mbegu watakazo zipeleka kwa wakulima baada ya kuzifanyia utafiti ni zile zinazostahamili kwa kiasi kikubwa mabadiliko haya ya hewa”, amesema.
Amesema tafiti zenye mashiko ni zile zinazowashirikisha wananchi wenyewe, hasa katika nyanja za kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara, uendeshaji wa viwanda, pamoja na sekta nyengine za uzalishaji na utoaji wa huduma.
Ameeleza kuwa pale ambapo wakulima wenyewe hawatashirikiswa hawataweza kutumia matokeo ya tafiti hizo katika kuzalisha mazo bora na yaliyo mengi zaidi.
Maalim Seif amesema ufunguzi wa maabara hizo zilizojengwa na kupatiwa vifaa na Tume ya Taifa Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa thamani ya shilingi milioni 640, umekuja katika wakati muafaka ambapo Zanzibar inahitaji kupata utaalamu wa mbegu na mazao yanayoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH, Hassan Mshimba, alisema taasisi zipatazo 20 zinanufaika na fedha kutoka tume hiyo, lakini kituo cha Utafiti wa Kilimo Kizimbani kimeonesha uwezo wa hali ya juu katika usimamizi wa fedha zinazotolewa na kuzitumia katika malengo yaliyowekwa.
Amesema fedha na misaada inayotolewa kwa Zanzibar kutoka COSTECH si fadhila bali ni haki yao kwa sababu Tume hiyo ni ya Muungano, hivyo Zanzibar ina haki ya kupata haki na fursa zote zilizomo ndani ya Tume hiyo.
Amesema kwa Zanzibar mbali na msaada huo ambao pia unajumuisha mafunzo kwa wafanyakazi, pia inanufaika na mafunzo ya kuzitumia fursa za kilimo kibiashara kwa ajili ya kuinua hali za maisha ya wananchi wa Unguja na Pemba.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili, Affan Othman Maalim akizungumza katika hafla hiyo, amesema maabara hizo kupatikana kwake ni hatua kubwa katika kufanikisha malengo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu saba, katika kuendeleza shughuli za utafiti, ikiwemo katika mazao na kilimo kwa faida ya wananchi.
“Hii ni hatua muhimu kwa serikali hii na n i mafanikio makubwa katika azma yake ya kukuza kilimo, ili kiendelee kuwa mkombozi wa wananchi kote Zanzibar”, amesema Katibu Mkuu.
Aidha, Affan amesema hatua hiyo itainua hadhi ya Zanzibar katika nyanja ya utafiti wa Kilimo na Maifugo, ambapo Zanzibar ilisifika tokea miaka ya 1910, ikiwa ni ya kwanza katika eneo hili la Afrika ya Mashariki na Kati.
No comments:
Post a Comment