Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amepata mapokezi mengine
makubwa kutoka kwa wafuasi wa Chadema, katika ziara yake ya siku ya pili
wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.
Umati mkubwa wa wakaazi wa wilaya hiyo walijitokeza katika viwanja vya Kiganamo kumlaki kiongozi
huyo, aliejipatia umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania.
Kutoka Kigoma mjini hadi Kasulu ni umbali wa kilomita 95, lakini
wananchi walitembea kwa miguu kumsikiliza kiongozi huyo huku msafara wake
ukisindikizwa na pikipi zaidi ya 200.
Shughuli za biashara zilisimama kwa muda wakati msafara wa mapipiki
ukipita, huku maduka mengi yakionekana kufungwa.
Akihutubia mkutano huo, Zitto alisema ataendelea kuwa mwanachama
mtiifu wa Chadema hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa, lakini vyovyote
iwavyo ataendelea kushirikiana na wananchi wa Kigoma.
Kuhusu mgogoro katika chama chake, alisisitiza kwamba mtu wa Kigoma
kugombea uenyekiti wa Chadema sio uhaini, lakini mashtaka yote aliyoandaliwa na
chama yalilenga kumlaumu kwa kutaka uenyekiti wa chama.
“Mimi sina chuki na mtu, lakini linapokuja suala la nchi na chama,
mimi nachangia nchi kwanza chama baadae,” alisema.
Alisema ataendelea kutetea wananchi kwa kufanya kazi zake za Ubunge
mpaka pale atakapokosa sifa za kufanya hivyo.
Wakati huohuo, habari zinasema baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya
CHADEMA wamemuonya Zitto kwa kile
wanachodai ukiukwaji wa waziwazi wa taratibu za chama.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wajumbe hao walishangazwa na kitendo cha Zitto kujiandalia ziara zenye
mwelekeo hasi kwa chama hicho.
Kilichowashangaza wajumbe hao
ni kitendo cha Mbunge huyo kufanya ziara
jimbo la Kasulu bila kukitaarifu chama huku mashabiki wake wakiutumia mkutano
huo kukashifu chama na viongozi wake.
Walisema kitendo kinachofanyika hakikubaliki na ni ukiukwaji mkubwa wa
kanuni na taratibu za chama.
No comments:
Post a Comment