Na Mwantanga Ame, Pemba
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi,
amewataka viongozi wenye tabia ya kutoa ahadi za kusaidia miradi ya maendelo
kutimiza ahadi zao na waache tabia ya kutoa ahadi hewa.
Aliyasema hayo kisiwani Pemba,wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa
skuli na kituo cha afya cha Ali Khamis Camp, inayomilikiwa na jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ).
Alisema imekuwa kawaida kwa baadhi ya viongozi kutoa ahadi za
kuwasaidia wananchi lakini jambo la kusikitisha baadhi yao wanashindwa
kutekeleza ahadi zao.
Alisema hilo si jambo na linaweza kusababisha migongano na wananchi na ni vyema wenye tabia
hiyo kuacha.
Alisema inafurahisha kuona Jeshi la Wananchi wa Tanzania, limeamua
kuanzisha skuli ya hiyo na kituo cha afya ambavyo vimekuwa vikiwahudumia
wananchi wengi wa kisiwani Pemba.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza maendeleo ya elimu kisiwani
Pemba, na kukuza utoaji wa huduma bora za afya ambapo hivi sasa vituo vya
serikali vimeonekana kuelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa.
Alisema serikali imefarajika kwa kiasi kikubwa kusaidiwa kwa kupunguza idadi ya wanafunzi ndani ya skuli
zake kwa vile skuli hiyo hivi sasa ina idadi ya wanafunzi 600.
Akizunguimzia juu ya sekta ya afya, alisema serikali itakaa pamoja na
wizara inayosimamia sekta hiyo kuona haja ya kuwaunga mkono kwa kuwapatia dawa.
Aliahidi kutoa matofali 1000, mifuko 50 ya saruji na mipira 10 ya
kuchezea mpira wa miguu na 10 ya mchezo wa netball na kuahidi kukaa pamoja na shirika la umeme
kuangalia uwezaekano wa kuiunganishia umeme skuli hiyo, ambapo shilingi 8,000,000 zitahitajika.
Akisoma risala ya wanafunzi, rais wa serikali ya wanafunzi, Nd.
Ridhwani Hamad, alisema maendeleo ya skuli hiyo kwa kiasi kikubwa yanatarajia
kuimarika baada ya kumalizika kwa ujenzi.
Mapema kamati ya skuli hiyo, ilieleza kuwa wanalazimika kuongeza skuli
hiyo kutokana na idadi ya wanafunzi wanaotaka kujiunga kuongezeka.
Nae kiongozi wa kambi hiyo, Nd. Julias Kambwao, alisema kuanzishwa kwa
skuli hiyo ni sehemu ya utaratibu wa jeshi la kuunga mkono sekta ya elimu.
No comments:
Post a Comment