Habari za Punde

Kampuni ya ALTEC Kuwekeza Vitega Uchumi Zanzibar

Na Othman Ame OMPR
Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na miradi ya uwekezaji katika sekta ya Viwanda, Bandari na Uwanja wa Ndege  ya ALTEC yenye makamu Makuu yake Nchini Ukrain imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza vitega uchumi vyake hapa Zanzibar.

Ujumbe wa Kampuni hiyo umekuja Zanzibar kufuatia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ya hivi karibuni aliyoifanya katika umoja wa falme za  Kiarabu { UAE } na kuyaomba Makampuni na Taasisi mbali mbali za uwekezaji kuja kuwekeza vitega uchumi vyao hapa Zanzibar.

Ujumbe wa Viongozi wa ngazi ya juu wa Kampuni hiyo yenye tawi lake Umoja wa Falme za Kiarabu kwenye Mji wa Dubai ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Dr.  Ramzan Musipov ulieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni kumi { U$ Dollar 10,000,000,000 } zitatengwa na kampuni hiyo katika mpango wake wa kutaka kuwekeza katika sekta ya Mafuta na Gesi, Bandari, pamoja na uwanja wa ndege.

Ujumbe huo ulimueleza Balozi Seif kuridhika na mazingira mazuri yaliyopo ya uwekezaji vitega uchumi hapa Zanzibar na uko tayari kutumia fursa hiyo katika kuona sekta ya Viwanda inakuwa ili isaidie kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar.


Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza ujumbe wa Kampuni ya altec  kwa uamuzi wake iliyouchukuwa wa kuangalia mazingira ya uwekezaji ndani ya visiwa vya 
Zanzibar katika kipindi kifupi tokea kupata fursa hiyo.

Balozi Seif alisema Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar   iko katika mpango wa kupanua Bandari yake sambamba na kuimarisha miundo mbinu katika uwanja wa ndege wa Pemba kwa lengo la kuongeza mapato yake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliufahamisha ujumbe huo wa Kampuni ya Altec kwamba mkazo umeongezwa zaidi kwenye sekta ya uchumi kwa kuimarisha eneo la utalii ambalo linaonekana kusaidia uchumi wa Zanzibar unaotegemea zaidi hivi sasa zao la Karafuu.

Hata hivyo Balozi Seif alisema ujenzi wa viwanda vidogo vidogo ulioachwa milango wazi kwa kushirikisha washirika wa maendeleo njeya ya nchi utaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na kupanua soko la ajira kwa kundi mkubwa la vijana wanaomaliza masomo yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.