Habari za Punde

NEC Zanzibar yawajadili wanaotaka kurithi nafasi ya Mansoor

Na Khamis Amani
KAMATI Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) Zanzibar, imejadili majina ya wanaCCM waliojitokeza kuomba kugombea nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Kiembe Samaki na baadae kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu.
Jimbo la Kiembe Samaki liko wazi kufuatia aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo, Mansour Yussuf Himid kuvuliwa uanachama mwishoni mwa mwaka jana.
Aidha Kamati hiyo imeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohammed Shein, kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 kwa mafanikio makubwa.
Kamati hiyo pia imeipongeza Jumuiya ya Vijana wa CCM Zanzibar kwa kufanikisha matembezi ya umoja huo katika mikoa yote mitano ya Zanzibar.
Kamati hiyo imesema, matembezi hayo yameweza kuleta mafaniko makubwa ndani ya mikoa hiyo ambayo yameleta hamasa ya aina yake na hivyo kufufua ari miongoni mwa wanaCCM na wananchi wa mikoa waliyopita vijana hao.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC-Zanzibar, Waride Bakari,ilisema  matembezi hayo ni mfano wa kuigwa na kuwataka vijana kuwa na mshikamano ili kutetea nchi yao.
Kamati hiyo pia imewapongeza viongozi, wanachama na wapenzi wote wa CCM na wananchi wa Zanzibar kwa kujitokeza kwa wingi kila pahala zinapofanyika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar kichama na kiserikali, na kusisitiza haja ya kujitokeza kwa wingi siku ya kilele cha maadhimisho hayo Januari 12, mwaka huu.
Aidha Kamati   imetoa mkono wa pole kwa waathirika wa ajali ya Kilimanjaro II, pamoja na wananchi wa Maziwang’ombe na Shumba mjini kufuatia ajali ya moto iliyoteketeza nyumba zao.
Kamati hiyo imewataka wale wote walioondokewa na ndugu zao wawe na moyo wa subira, kutokana na kuondokewa na wapendwa wao na kumuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema Peponi.

Aidha Kamati hiyo imetoa salamu za mkono wa pole kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kufuatia kifo cha Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa kilichotokea katika hospitali ya Kloof Medi-Clinic mjini Pritoria nchini Afrika ya Kusini.

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.