Habari za Punde

Wito : Tembeleeni maonesho mjifunze historia ya Mapinduzi

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                    03 Januari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kuyatumia maonesho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kujifunza historia na malengo ya Mapinduzi hayo pamoja na mafanikio na changamoto zinazowakabili katika harakati za kujenga nchi huru yenye kuzingatia misingi ya haki na usawa.
 
Wito huo umetolewa jana na Rais wa Zanzibar na MwenyekIti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akifungua maonesho ya miaka 50 ya Mapinduzi yanayofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Taifa –SUZA Kampasi ya Beit el Ras Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
 
Amesema maonyesho hayo yanatoa fursa ya pekee kwa wananchi kuifahamu historia ya nchi yao na kujifunza mambo mengi mapya hivyo kuibua ari mpya ya wananchi kutafuta maendeleo na kuimarisha mapenzi kwa nchi yao.
 
Alieleza kuwa maonesho hayo ni muhimu kwa historia ya Zanzibar hasa ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya wananchi wake wamezaliwa baada ya tukio hilo kubwa na muhimu katika historia ya ukombozi wa watu wa Zanzibar
 
Akilinganisha takwimu za Sensa ya mwaka 1967 ambapo Zanzibar ilikuwa na wakaazi 354,818 na mwaka 2012 watu 1,303,569, Dk. Shein alifafanua kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa watu zaidi ya milioni wa Zanzibar hivi sasa walizaliwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
 
Kwa hiyo alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maoenesho hayo na kuwataka wazazi na walezi kufuatana na watoto wao wakati wakitembelea maonesho hayo ili nao waweze kujionea mambo mazuri yaliyoandaliwa katika maonesho hayo.
 
Katika kuhakikisha kunakuwepo kumbukumbu sahihi za historia ya Zanzibar na kuwawezesha wananchi kufahamu historia hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameiangiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kukusanya vitabu na taarifa mbalimbali vya Wizara na Idara za Serikali zilizotayarishwa kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ili vitumike kutunga vitabu kwa ajili kufundishia masomo ya historia na urai katika ngazi mbalimbali za elimu.
 
Sambamba na agizo hilo amezitaka Wizara zote zijiridhishe na vitabu na taarifa walizozitoa wakati wa maadhimisho haya na baadae wachapishe nakala za kutosha ili zisambazwe katika maskuli, maktaba zote nchini, Ofisi za Serikali na makumbusho ya Taifa.
 
Dk. Shein ametaka vitabu na machapisho hayo yahifadhiwe vizuri katika njia za kawaida na kieletroniki ili iwe rahisi kuzitumia siku za baadae  na kuongeza kuwa kwa wizara zenye tovuti  kumbukumbu hizo nazo ziwekwe humo ili iwe rahisi wananchi kuzipata.
 
Katika hotuba yake hiyo alisifia pia ushirikiano uliopo kati ya sekta ya umma na binafsi na kubainisha kuwa ushirikiano huo umekuwa ukitoa mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi na kukuza soko la ajira.
 
Baada ya uzinduzi huo Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitembelea mabanda ya baadhi ya Wizara na taasisi mbalimbali kuona shughuli zinazofanywa na Wizara na  taasisi hizo.
 
Uzinduzi wa Maonyesho hayo ya siku nne ambayo yanashirikisha Wizara, Idara na Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sekta binafsi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara ulishuhudiwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.  
 
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.