Na Rose Chapewa, MBEYA
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu
kanda ya Mbeya, Noel Peter Chocha,
amelaani matukio ya kushambuliwa mahakimu wawili katika maeneo ya Tukuyu na
Ileje jijini Mbeya na kusababishiwa ulemavu wa kudumu.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini, Jaji huyo
alionesha kusikisitishwa na vitendo hivyo na kwamba wanafanya uchunguzi wa kina
kubaini wahusika wa matukio hayo.
Alisema anashangazwa kuwa vitendo hivyo walifanyiwa mahakimu wa kike
pekee ambapo mmoja alitobolewa jicho hivyo amelazimika kuwekewa jicho la bandia.
Jaji huyo alisema ikiwa uchunguzi utakamilika na kuonesha kuwa zipo
njama za makusudi za kufanya vitendo hivyo, mahakama haitasita kuuambia uongozi
husika ili kusitisha huduma za kimahakama katika maeneo ambayo matukio
yalitokea.
"Tukifanya uchunguzi na
kubaini kulikuwana njama za makusudi za kupanga kuwadhuru na kuwaumiza
mahakimu, hakika hatutasita kuchukua hatua pamoja na kusitisha huduma jambo
ambalo litakuwa ni hasara kwa wakazi wa maeneo hayo,” alisema.
Naye Wakili wa Serikali, kanda ya Mbeya, Edwin Kakolaki, alisema
mahakama imeweka mikakati ya kuhakikisha mashauri ya muda mrefu yanamalizika
mapema na kunakuwepo ripoti za kesi zilizoisha katika vipindi mbalimbali vya mwaka wa mahakama.
Aliwaomba wadau wa mahakama ikiwemo magereza, jeshi la polisi na
vyombo vingine vya upelelezi kuhakikisha kesi za jinai zinapelelezwa vizuri na
kwa haraka, nyaraka mbalimbali zinapitiwa kwa uhakika na mashahidi kuandaliwa vizuri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, aliwataka
mawakili wa kujitegemea kupunguza gharama za uendeshaji kesi kwa wananchi kwa
kuwa wengi wao kipato chao ni cha chini.
No comments:
Post a Comment