Na Kadama Malunde,KAHAMA
ZIKIWA zimesalia siku chache
kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani katika kata Ubagwe wilayani
Kahama mkoani Shinyanga,kampeni za uchaguzi huo zimeingia doasari baada ya watu
wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi CHADEMA kuwavamia na kuwajeruhi vibaya kwa
mapanga wafuasi watano wa CCM.
Akizungumza katika hospitali ya wilaya ya Kahama alikolazwa kufuatia
kupata majeraha ya mapanga, Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Kahama, Masood
Melimeli, alisema tukio hilo
lilitokea juzi majira ya saa 1:30 usiku wakati wakitokea kijiji cha Ihata
kwenda Itobola kwenye kampeni.
Alisema walipofika katikati ya pori walikutana na gari la CHADEMA aina
ya Toyota land Cruser ikiongozwa na Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki,
Sylivester Kasulumbayi na kuanza kuwashambulia kwa kutumia mapanga, nondo na
marungu.
Alisema waliojeruhiwa katika vurugu hizo ni Katibu mwenezi wa CCM,
Masood Melimeli aliyeumia sehemu ya mkono na bega, Ramadhani Salumu aliyepigwa
panga la mguu na mkono, Sebastian Masonga aliyevunjwa mkono wa kushoto, dereva
Charles Muhiga aliyejeruhiwa sehemu za kichwani na Mtendaji wa kata ya Ubagwe,
Stephen Kimario, aliyepigwa vibaya sehemu za kichwani.
Alisema katika tukio hilo
wafuasi wawili wa CCM waliofahamika kwa jina moja moja la Ismail na Samweli
walipotea kusikojulikana baada ya kukimbia kujinusuru na kifo.
Katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Shinyanga, Emanuel Mlimandago, amelaani
kitendo hicho na kusema hiyo sio
demokrasia ya kweli na kuongeza kuwa Watanzania wote hawana budi kulaani
kitendo hicho.
Mwenyekiti wa TADEA wilaya ya Kahama, Charles Lubala, akizungumzia
tukio hilo, alisema mfuasi mmoja wa CHADEMA alivamia mkutano wa CCM na ndipo
walipomkamata na kumuweka katika gari lao kwa lengo la kumpeleka kituo cha
polisi Bulungwa.
Alisema baada ya kumuweka
garini,wafuasi wa CHADEMA walitangulia mbele na kuweka vizuizi barabarani kabla ya kuanza kushambuliana.
“Kwa kweli hizi kampeni zimekuwa kama
vita kwa sasa ni hatari na tunapaswa kujihami kikamilifu kwani unaweza
kupoteza maisha kwa sababu ya kampeni tu,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kahama, Juma Protas,
alikanusha wafuasi wa chama hicho kuhusika katika tukio hilo .
“Siyo kweli,vijana watatu wa CHADEMA ndiyo waliotekwa na CCM katika eneo
la makao makuu ya kata ya Ubagwe, baada ya kutekwa wakafungwa kamba na
kuingizwa kwenye gari, ndipo wananchi wananchi walipoamua kwenda kuwasaidia na
purukushani ndipo zilipoanza,” alisema.
“Baada ya purukushani hizo,CCM wakapiga simu polisi, polisi wakaenda
kwenye kambi ya CHADEMA na kupiga risasi juu kisha kuwakamata wafuasi 13 wa
akiwemo Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylivester Kasulumbayi, na sasa wanapelekwa
mahakamani,CCM ndiyo waliteka vijana watatu
wa CHADEMA na vijana hawa hadi sasa hawajulikani walipo,” alisema.
Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kahama, Dk. Hellen Membe,
alisema siku ya tukio majira ya saa sita
usiku alipokea majeruhi watano na wanaendelea kupatiwa matibabu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Kamanda wa
polisi mkoa wa Shinyanga, ACP Evarist Mangala, alithibitisha kutokea tukio hilo na kuongeza kuwa
jeshi la polisi linawashikilia watu 13.
Kampeni za uchaguzi katika kata ya Ubagwe wilayani Kahama zinafanyika
kufuatia aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Richard Mndula kufariki dunia mwaka
jana huku kinyang’anyiro hicho kikiwahusisha wagombea watatu kutoka vyama vya CCM, TADEA na CHADEMA.
Jee tunaelekea wapi na tutafika wapi kwa siasa hizi. Iko wapi demokrasi na iko wapi ile hali ya vyama kuaminiana. Lakini hii si ajabu kwa Chadema maana ndani ya chama chao wenyewe kwa wenyewe wamepigana mbele ya mahakama kwa huyu kumpendelea huyu. Chadema wacheni siasa za chuki maana zinajenga uhasama tu.Badala ya kusonga mbele kwenye demokrasi kwa siasa hizi tunarudi nyuma.
ReplyDeletedhuluma , fitna , uroho , uchoyo , rushwa vikikithiri haya ndio matokeo yake , serikali na vyombo vyake vimezidi uonevu kwa wananchi wakati wao wanajinufaisha hali za raia zinadidimia , wakati umefika wa mapinduzi mengine ndugu zangu kama hatukuwapindua kwa nguvu hatufiki popote kwa kura huu nido ukweli , tunawaomba akina polisi na majeshi wakae chonjo watuachie tulumbane wenyewe mpaka haki isimame , tupate viongozi waadilifu
ReplyDelete