Na
Kadama Malunde, Shinyanga.
BUNDI
anaendelea kulia ndani ya chama cha CHADEMA baada ya Madiwani wawili wa chama
hicho katika manispaa ya Shinyanga kutangaza kujiuzulu kwa madai kuwa uongozi
ngazi ya taifa umeendelea kusikiliza majungu, kuwadhalilisha baadhi ya viongozi
pamoja na kuwaita wasaliti.
Madiwani waliojiuzulu ni diwani wa kata ya Ngokolo, Sebastian
Peter na Zacharia Mfuko kutoka kata ya
Masekelo huku wakieleza kuwa wameamua kuchukua
uamuzi huo kama ishara ya kuwajibika kwa niaba ya makosa yaliyofanywa na
viongozi wa chama hicho kitaifa.
Wakizungumza
na waandishi wa habari katika ofisi ya Naibu Meya wa manispaa hiyo, walisema wamekabidhi
barua za kung’atuka kwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo, ambae walidai ndie mwajiri
wao.
Diwani
wa kata ya Ngokolo, Sebastian Peter
alitaja sababu tatu zilizopelekea kukuchua uamuzi huo.
“Ndugu
waandishi wa habari sababu ya kwanza inatokana
na kikundi cha Red brigade mwezi Novemba 2013 kuandika barua kwa Katibu Mkuu ambayo ililenga
kuwadhalilisha viongozi wetu wa mkoa akiwemo Katibu wa mkoa, Nyangaki Shilungushela na Katibu wa
wilaya, Siri Yasin kuwa wamehongwa kiasi cha shilingi milioni 90, tuhuma ambazo ni uongo,”alisema.
Alisema
sababu ya pili ni Mwenyekiti wa taifa Freeman Mbowe, kuahihdi chama kitamaliza
kujenga nyumba ya marehemu Philip Shelembi aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la
Shinyanga mjini, ahadi ambazo ameshindwa kuzisimamia.
Aidha
alisema sababu ya tatu Mbowe amekuwa na tabia ya kuwaita baadhi ya
wanachama wasaliti na wahaini,
kauli ambazo hazipaswi kuzungumzwa na kiongozi wa juu wa chama.
“Chama
hiki tumekijenga kwa siku nyingi, mimi ni miongoni mwa wanachama watakaokuwa wa
mwisho kuamini kama kweli Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na
wengine kuwa ni wasaliti wa chama,” alisema.
Kwa
upande wake, diwani wa kata ya Masekelo, Zacharia Mfuko aliungana na diwani wa Ngokolo
kuchukua maamuzi magumu na na kuongeza
kuwa chama hicho kimekuwa kikifanya mambo
kwa ubabaishaji.
“Katika
kata yangu kulikuwa na sakata la Mweyekiti
wa mtaa kukigawa kiwanja cha mwananchi wakati kuna kamati ya ugawaji,
nilipokieleza chama walidai kulishughulikia lakini mpaka sasa hakuna
kinachoendelea na uongozi wa chama umekaa
kimya,” alisema.
Hata
hivyo, madiwani hao walisema pamoja na kujivua nyadhifa zao za udiwani bado
wataendelea kuwa wanachama wa Chadema kwani hawajawahi kuitwa kwenye kikao
kuhojiwa kwa lolote na kwamba kwa muda wote waliokuwa madiwani na hawakuwa na
mpango wa kujiunga na chama chengine.
Akizungumzia
kuhusu maamuzi hayo, Katibu wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga, Nyangaki
Shilungushela, alisema chama kimepata pigo kubwa lakini kitajipanga kikamilifu
ili kurudisha kata hizo mikononi mwake.
Manispaa
ya Shinyanga ilikuwa na madiwani wa CHADEMA wanane na sasa wamebaki sita huku Chama
cha Mapinduzi kikiendelea kuwa na madiwani 17.
No comments:
Post a Comment