THE
UNITED REPUBLIC
OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
Fax: 255-22-2113425
|
![]() |
PRESIDENT’S
OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX
9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Februari 4, 2014, amepokea hundi
ya Sh. milioni 100 kutoka Benki ya CRDB kusaidia wahanga wa mafuriko yaliyozikumba
wilaya tatu za Kilosa, Mvomero na Gairo katika Mkoa wa Morogoro, mwezi
uliopita.
Rais
Kikwete amekabidhiwa hundi hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dkt. Charles
Kimei katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, na kuhudhuriwa
pia na Mhesimiwa William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia pia masuala ya maafa.
Akizungumza
kabla ya kukabidhi hundi hiyo kwa Rais Kikwete, Dkt. Kimei amesema kuwa fedha
hizo ni sehemu ya Sh. Milioni 850 ambayo ni asilimia moja ya faida ya Benki
hiyo ambayo hutengwa kila mwaka kwa ajili ya kuunga mkono shughuli za jamii.
“Sote
tumeona madhara makubwa yaliyosababishwa na mafuriko haya. Watu wengine
wamepata hasara – akinamama, watoto, wajawazito na wazee. Hawa wote wanahitaji
misaada ya ziada ili kukabiliana na athari za mafuriko hayo,”
amesema Dkt. Kimei.
Akizungumza
kabla ya kupokea hundi hiyo, Rais Kikwete ameelezea kwa ufupi mafuriko hayo
yaliyotokea alfajiri ya Januari 22, mwaka huu, 2014 na athari ambazo zimetokana
na mafuriko hiyo katika maeneo ya Magole, Dakawa na Mateteni huko Dumila, Wilaya
ya Mvomero, ambayo aliyatembelea mwishoni mwa mwezi uliopita kujionea madhara.
“Waswahili
husema kuwa ajali haina kinga na ni kweli. Unajua mafuriko yaliyotokea katika
eneo la Dumila hayakutokana na wala na mvua ya pale. Mvua ilinyesha kule
Kiteto, Mkoa wa Manyara, lakini walioathirika kwa mafuriko ni hawa jamaa zetu
wa Dumila. Bahati tu ni kwamba mafuriko hayo yalilikumba eneo hilo alfajiri
wakati watu tayari wameamka na ndio maana hakuna mtu aliyepoteza maisha yake
katika eneo hilo,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Watu
wamepata hasara kubwa. Baadhi nyumba zao zimesombwa na kuzolewa na maji,
nyingine zimebomoka, watu wamepoteza mali
zao nyingi kama vile nguo na wengine hata
chakula chao kimesombwa na maji. Wanahitaji msaada na kwa kweli sisi katika
Serikali tunaishukuru sana
CRDB kwa kutoa msaada huu kwa sabababu unachangia katika jitihada za Serikali
kukabiliana na tatizo hili.”
Akizungumza
katika shughuli hiyo, Mheshimiwa Lukuvi amesema kuwa tathmini mpya imeonyesha
kuwa watu walioathirika katika mafuriko
hayo ni 9,268 na kati ya watu hao kaya 522 hazina makazi kabisa baada ya nyumba
zao kubomolewa na maji, nyingi zaidi 466, zikiwa katika Wilaya ya Kilosa.
Amesema
kuwa nyumba 537 zimeharibika hata kama wenye nyumba hizo bado wanaendelea
kuishi ndani ya nyumba hizo na nyingine 1,036 ziliingiwa na maji hata kama hazikuharibika.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
04 Februari, 2014
No comments:
Post a Comment