Na Kadama Malunde,SHINYANGA
MAHAKAMA ya hakimu mkazi wilaya ya Shinyanga mkoani
Shinyanga, imewahukumu Mathias Kalonga (40) na James Moshi (35) wakazi wa
Shatimba wilaya ya Shinyanga vijijini, kifungo cha miaka 242 jela baada ya
kupatikana na kosa la ubakaji kwa kundi,wizi wa kutumia silaha na kujeruhi.
Mwendesha mashtaka,wakili wa serikali Salome
Mbuguni aliiambia mahakama hiyo jana kuwa mnamo tarehe 18 mwezi Oktoba,2012
washtakiwa wakiwa na wenzao walivamia nyumbani kwa mlalamikaji Lesha
Jidomela,wakiwa na bunduki na mapanga kisha kumjeruhi kisha kupora simu tatu kinyume
cha sheria hilo ikiwa ni kosa la kwanza na la pili.
Alidai katika kosa la tatu na nne washtakiwa hao
wote kwa pamoja walivamia nyumbani kwa
Sayi Jidomela(ndugu yake Lesha Jidomela) kisha kupora shilingi 57,000 na simu
moja na mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa na panga kumjeruhi kwa kutumia panga
hilo.
Aidha alidai katika kosa la tano na sita washtakiwa
kwa pamoja walimbaka mke wa Lesha Jidomela kwa pamoja, lakini pia wakambaka mke
wa Sayi Jidomela.
Mahakama ilisema upande wa mashtaka umethibitisha
makosa dhidi ya washtakiwa pasipo na mashaka.
Akitoa hukumu,hakimu mkazi wa mahakama hiyo,
Thomson Mtani, alisema kutokana na kosa la wizi wa kutumia silaha kila
mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela, hivyo kila mmoja atatumikia
kifungo cha miaka 60 kwa sababu kila
mmoja alitenda kosa hilo katika nyumba mbili.
Alisema katika kosa la ubakaji kila mshtakiwa atatumikia
kifungo cha miaka 30 jela na kwa kuwa wote kwa pamoja walibaka wanawake wawili
kwa zamu kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka 60.
Hakimu huyo alisema mshtakiwa wa kwanza Mathias
Kalonga atatumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kujeruhi kwa panga
na kutakiwa kulipa fidia ya shilingi 200,000 kwa waliojeruhiwa.
Kufuatia hukumu hiyo washtakiwa watatumikia kifungo
cha miaka 242 jela,ambapo mshtakiwa wa kwanza Mathias Kalonga (40) atatumikia
miaka 122 jela na mshtakiwa wa pili James Moshi (35) atatumikia miaka 120 jela
na wote kwa pamoja kuchapwa viboko 12 kila mmoja.
Haki ya kukata rufaa imetolewa kwa upande
usioridhika.
No comments:
Post a Comment