Na Hafsa Golo
ZAIDI ya nyumba 50 na misingi zilizojengwa katika kijiji
cha Tunguu zinatarajiwa kuvunjwa na serikali kufuatia uvamizi uliofanywa na
wananchi.
Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji,Dk. Mohammed Juma, alisema eneo hilo tayari limepimwa kwa ajili
ya ujenzi wa viwanda, skuli,taasisi za serikali na binafsi.
Alisema kitendo kilichofanywa na baadhi ya wananchi
cha kuvamia na kujenga nyumba za kuishi hakiwezi
kufumbiwa macho.
Alisema watendaji wanaosimamia masuala ya ardhi
wamekusudia kutekeleza kwa vitendo majukumu yao na kwamba nyumba hizo
zitavunjwa.
"Baadhi ya wananchi wamekuwa wakijaribu kama
serikali itaweza kufanya maamuzi au tutafanya nini, tunasema tumebadilika tutazivunja
nyumba hizi kwa sababu wahusika wamevamia,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ardhi na Usajili,
Januari Fusi, alisema serikali haikurupuki katika mipango yake hata kama
utekelezaji wake utachukua muda mrefu.
Aidha alisema suala la kuwaondosha watu wote
waliovamia linasimamiwa na ngazi zote za serikali hivyo hakutokuwa na maamuzi
mengine.
Alisema serikali imechukua hatua mbali mbali ikiwemo
kutoa taaluma kwa wananchi juu ya uvamizi wa eneo hilo ambapo kwa hatua ya
awali walitoa matangazo kupitia vyombo vya habari.
Mmoja ya mwananchi ambae ni mkaazi wa eneo hilo,
Eduu Juma, alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba pamoja na taratibu
zinazoendelea kuchukuliwa na serikali lakini ni vyema serikali ikafanya
mazungumzo na wakaazi wa eneo hilo ili waweze kupata ukweli wa umiliki wao.
"Mimi sijavamia naishi hapa miaka 40 sasa na
eneo hili nimerisi kutoka kwa marehemu mume wangu leo wanataka tuhame niende
wapi na watoto hawa lazima serikali ituhurumie"alisema.
Naye Hassan Mkulima alisema kwamba serikali
haitendi haki kwa kuwa eneo hilo wanalimiki kisheria.
No comments:
Post a Comment