Na Salum Vuai, MAELEZO
MIFUMO ya kisasa ya kuishi ambapo watu wengi
wanaiga mila za kimagharibi, imeelezewa kuwa inachangia sana
ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza hapa Zanzibar .
Akitoa mada katika warsha ya siku mbili ya
kujadili mpango kazi unaojadili namna na kupambana na magonjwa hayo
inayofanyika hoteli ya Zanzibar Ocean View iliyoko Kilimani mjini Zanzibar, Meneja
wa kitengo cha maradhi yasiyoambukiza-‘NCD’ Dk. Omar Mwalimu alisema, njia
pekee inayoweza kufanikisha kupunguza magonjwa hayo, ni kwa jamii kufuata mfumo
wa asili wa kuishi.
Alifahamisha kuwa, miongoni mwa mambo
yanayowaathiri sana watu, ni matumizi ya tumbaku na sigara, kunywa pombe na
kutokuishughulisha miili yao
kwa kufanya mazoezi.
Dk. Mwalimu alisema, utafiti uliofanywa mwaka
2011 kubaini chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza, umegundua kuwa asilimia 7.3 ya
wananchi wa Zanzibar wanatumia bidhaa za tumbaku, asilimia 1.7 wanakunywa
pombe, na asilimia 18 tu ndio wanaofanya mazoezi.
Aidha alisema, utafiti huo umeonesha asilimia
33 ya wananchi, wanakabiliwa na ugonjwa wa presha.
Alieleza kuwa, katika kila watu watatu, mmoja
kati yao anaugua presha, ambapo asilimia 3.7, (watu 48,000 hadi 50,000) hapa
Hata hivyo, alisema ongezeko hilo limeanza
kubainika kwenye miaka ya 90, baada ya jamii na serikali kutanabahi, ambapo
hapo kabla mkazo mkubwa ulikuwa umeelekezwa katika maradhi mengine, ikiwemo malaria na baadae
UKIMWI.
Aidha, alifahamisha kuwa, asilimia kubwa ya wananchi
wa Zanzibar hawana utamaduni wa kula mbogamboga na matunda katika milo yao,
jambo ambalo linawakosesha virutubisho muhimu miilini mwao ambavyo vina nafasi
kubwa ya kujenga afya na kuwaepusha na maradhi mbalimbali.
“Watu wengi wanadhani kula chakula kingi ndio
muhimu, lakini hawajali ubora na umuhimu wa vyakula vinavyohitajika kwa afya
zao,” alisema.
Alisema umefika wakati sasa serikali kupitia
sekta na wizara zake mbalimbali, zichukue nafasi yao katika kuielimsha jamii
juu ya haja ya kuzingatia taratibu nzuri za kuishi, na kupunguza vyakula vya
kisasa ambavyo madhara yake ni makubwa kuliko manufaa.
Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo, walishauri
hatua mbalimbali zichukuliwe, ikiwa pamoja na kupiga marufuku uingizaji wa
sigara na pombe, ili kuinusuru jamii na janga la magonjwa yasiyoambukiza.
Wengine walipendekeza kukatazwa uuzaji wa
baadhi ya vyakula maskulini hasa vinavyoweza kuwaathiri watoto kiafya, na
badala yake wafanyabiashara wa maskulini wahamasishwe kuuza vyakula vya asili pamoja na matunda.
Aidha, walisema suala la kufanya mazoezi na la
mtu binafsi lakini anahitaji kuelimishwa ili asiuendekeze mwili, na badala yake
wafanye mazoezi japo ya kutembea na kupunguza kupanda gari hata kwa safari ya
masafa mafupi.
Akizungumza katika warsha hiyo iliyokuwa na
mada mbalimbali, Mwakilishi wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) Neema
Kileo, alisema wananchi wa Zanzibar
wanapaswa kutumia vyema neema ya mazao ya matunda yanayopishana kila baada ya
kipindi kifupi badala ya kukumbatia vyakula vya kizungu.
Aidha aliwataka wataalamu wa sekta ya afya,
kuwa na mikakati maalumu ya kusambaza elimu kwa wananchi ili wahamasike kutumia
vyakula vya asili zikiwemo mbogamboga na matunda, badala ya kukimbilia kuviuza
huku wenyewe wakipuuza kuvila.
Warsha hiyo inatarajiwa kufungwa leo.

No comments:
Post a Comment