Na
Joseph Ngilisho,Arusha
JESHI
la Polisi nchini limetangaza bingo ya shilingi milioni 10, kwa mtu
atakayesaidia kufichua magaidi
waliohusika kuripua bomu katika baa ya Arusha Night Park, iliyopo
Mianzini jijini hapa,ambapo watu 15 walijeruhiwa vibaya.
Aidha
limekana taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ambae
amekuwa akitoa taarifa juu ya kujulikana kwa watuhumiwa wa mabomu walioripua
katika kanisa katoliki la mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti na katika
mkutano wa Chadema,eneo la Soweto .
Mkurugenzi
wa upelelezi wa makosa ya jinai,Isaya Mngulu, ametoa kauli hiyo mbele ya
wanahabari jijini hapa na kusisitiza kuwa polisi imeshindwa kuwatia mbaroni
watuhumiwa wa mabomu na upelelezi bado unaendelea.
Alisema
licha ya kuripua baa hiyo,watu hao walitega bomu jingine katika baa ya Washington iliyopo
jijini hapa, ambalo halikuweza kuripuka baada ya kugundulika majira ya saa 6
usiku na kwamba polisi wanalifanyia uchunguzi zaidi.
Akijibu
swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua kauli ya mkuu wa mkoa wa Arusha
aliyoutangazia umma kwamba mtandao wa waripuaji wa mabomu umejulikana, alisema
taarifa hiyo anaijua yeye kama msemaji wa
serikali ila jeshi la polisi haliwezi kutoa taarifa ya upotoshaji.
“Nimesema
muulizeni yeye, huyo ni msemaji wa serikali, hayo aliyowaambia mrudieni mkamuulize
yeye, sisi kama polisi hatuna taarifa kama hiyo,’’ alisema.
Akizungumzia
hali ya ulinzi na usalama katika jiji la Arusha, alisema polisi hawawezi kutoa
ulinzi wa kila eneo lenye mkusanyiko wa watu ila aliwasihi wananchi kujilinda
wenyewe kwani jeshi hilo
halina uwezo wa kutoa huduma kila eneo kutokana na uchache wao.
Aliwataka
wafanyabishara katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kuhakikisha
wanafunga kamera za usalama (CCTV) yenye
uwezo wa kurekodi matukio muda wote na kuimarisha ulinzi katika maeneo yao muda wote.
Aidha,
alisema ni vyema wananchi wakachukua tahadhari na kutoa taarifa polisi pindi
wanapoona kitu kisichoeleweka ama kumshuku mtu mwenye kubeba mfuko ambao
utakuwa na mashaka.
Akielezea
hali ya majeruhi, alisema watu 15 waliojeruhiwa na kulazwa kati yao saba wameruhusiwa na wengine nane wanaendelea kupatiwa
matibabu katika hospitali ya mkoa Mount
Meru .
Aliwataja
wanaoendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo ni Evance Maleko, Evarist
Richard, Petro James, Christine Zakaria, Pius Shayo, Antelus Zakaria,Sudi
Ramadhani na Mariam Juvenary Hans.
Aliongeza
kuwa jeshi la polisi limeunda kikosi maalumu cha wataalamu wa kuchunguza
mripuko wa bomu,kwa kushirikiana na jeshi la wananchi JWTZ na Ofisi ya Mkemia
Mkuu wa serikali ili kubaini bomu hilo ni la aina gani.
No comments:
Post a Comment