Habari za Punde

Mawaziri wajibu mapigo

Na Mwantanga Ame, DODOMA
BAADHI ya Mawaziri wa Serikali ya Zanzibar, wamefunguka na kuwajia juu baadhi ya wajumbe wa bunge maalum la katiba, kwa kudai hoja zao hazitikisi kibiriti kwa kuwa hazina mashiko.

Mawaziri hao walikuja juu baada ya baadhi ya wajumbe wa bunge hilo, akiwemo Mwakilishi wa  Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, kudai baadhi ya mawaziri wa serikali ya Zanzibar wamekuwa vigeu geu na wamekuwa wasaka tonge, kwa kushindwa kuelezea hoja zao kama walivyokuwa wakifanya Zanzibar.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mawaziri hao, walisema wanawashangaa wajumbe hao kwa kuwashushia lawama kwa kudai wako kimnya, huku wao wakisimama na kutoa hoja zilizojaa matusi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Dk. Mwinyihaji Makame, akitoa mchango wake, alisema ipo haja kwa wajumbe wa bunge kujiuliza ni kwanini tume zilizoundwa kabla ya mapendekezo ya rasimu ya sasa, maoni yao yaliokataliwa.

Alisema wanaotaja mawaziri wa Zanzibar, kwenye mjadala huo hawana hoja na inaonesha jinsi walivyofilisika kisiasa katika  kutetea hoja zao.

“Mawaziri walikuwa wakitetea hoja hakuna anaekataa hoja kwani mambo yote waliyazungumza baada ya kukubalika katika serikali na sio kama wamekaa kimya,” alisema Mwinyihaji.

Alisema serikali katika kutetea hilo tayari imefanikiwa kuruhusiwa kukopa, kujiunga na Umoja wa Mataifa kwa mambo yasiokuwa ya Muungano, kupunguza  orodha ya mambo ya muungano kutoka 32 hadi saba jambo ambalo linajionesha  kama kazi waliyoifanya imetoa matunda.

Alisema inasikitisha kwa baadhi ya wajumbe kuanza kudai kuwa ndani ya miaka 50 hakuna maendeleo Zanzibar jambo ambalo sio kweli kwani Zanzibar hivi sasa ni tofauti na  miaka 300 ya utawa wa kikoloni.

Alisema madhumuni ya wajumbe hao kudai mfumo wa serikali tatu wanataka  kupewa kiti Umoja wa Mataifa, kiti cha  EAC, Benki Kuu na sarafu yao, mamlaka ya kuamua sera na uchumi, uraia na kuukataa uraia wa Zanzibar.


Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi Maalum, Haji Omar Kheir, alisema anashangaa kuona mawaziri wa Zanzibar wanasakamwa kwa kudaiwa kuwa wao ni wasaka tonge, na wako mstari wa mbele kuvuruga Muungano huku wengine wakiwataka wasirudi Zanzibar.

Alisema vitisho hivyo ni sawa na kutikisa kibiriti ambacho kwao kimejaa na haoni haja kwa wajumbe wa bunge hilo kuanza kutishana.

Mohammed Aboud Mohammed, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, akitoa maelezo yake, alisema katiba ya Zanzibar haikani utanzania na sio jambo jema kwa wajumbe hao kutoa maeneo ambayo hayana ukweli.

Alisema kuna watu waliokuwa wakitoa maoni ambayo yalionekana kukinzana tangu awali na haitashangaza wajumbe hao kuona wanawashutumu mawaziri.

Nae mjumbe, Pereira Ame Silima, alisema wazo la kuleta mfumo wa serikali tatu yeye binafsi hakubaliani nalo kwa vile vigezo vinavyotumika havionekani kama vina mantiki ya kufanyika kwa mabadiliko ya mfumo wa sasa wa muungano.

Mjumbe Waride Bakari Jabu, alimuumbua mjumbe mwenzake Chiku Abwao ambae alidai  hashangai kumuona apendekeza muungano wa serikali mbili uvunjike kwa vile yeye ni raia wa Congo.

Aidha mjumbe Hija Hassan Hija, akitoa mchango wake alisema mfumo wa serikali tatu ndio utakaosaidia Zanzibar kupata haki zake.

Felister Bura, alisema bila ya kuwepo mfumo wa serikali mbili basi watambue Watanzania watagawana mbao na ni lazima wajumbe wa bunge hilo kujenga mshikamano.
Makame Mshimba Mbarouk, alisema anashangazwa na Katibu Mkuu wa CUF kutaka serikali tatu wakati hapo awali alitaka  serikali mbili.

Nae Faharia Khamis Shomari, alisema dhamira ya serikali ya kumruhusu Jemshid, alikuwa na dhamira ya kumfanya aje aone maendeleo ya Zanzibar na sio kutawala Wazanzibari kwa mlango wa nyuma.

Said Arif alisema sehemu kubwa ya maoni ya katiba yamechafuliwa na wasomi kwani baadhi yao wamekuwa wakitoa maoni yanayotofautiana.

Nae Januari Makamba akitoa maelezo yake, alisema kama Watanzania wanataka kuvunja Muungano ndani ya mwaka mmoja ama miwili na kuunga mkono mfumo wa serikali tatu basi watambue hayo ni majanga.


Dk. Ave Maria Semakafu, alisema fursa iliyopo ya kurudi kwenye katiba itasaidia wananchi kwani hivi sasa kuna mahitaji makubwa ya kielimu ambayo yamekuwa yakichangiwa na bajeti ndogo inayotengwa na serikali.

3 comments:

  1. mimi watu wa bara kutetea muungano wa serekali mbili sishangai nashangaa hao wazanzibar wanaotaka serekali mbili

    ReplyDelete
  2. Mawaziri wa CCM Zanzibar ni vigeugeu, hawawezi kuitetea Zanzibar wanatetea matumbo yao na wakiambiwa kweli hugeuka kuwa wabaguzi

    ReplyDelete
  3. Mwinyihaji Makame. Unazungumzia mambo ya Mungano kutoka 32 hadi 7. Iwapo hao wapinzani munaowalaumu hawakupiga kelele nyie kwa akili zenu za kuchangiwa dodoma si mungeliona ni sawa tu kama munavyoona ni sawa hili suala la Serikali mbili ambalo ndio jinamizi kuu la mafanikio na maendeleo ya Zanzibar. Musidanganye wazanzibari. Hamuna mpango wowote ni wizi tu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.