Habari za Punde

Wete waipongeza NIDA

Na Masanja Mabula,Pemba
ZOEZI la uwandikishaji wa vitambulisho vya taifa, limeanza kwa mafaniko katika wilaya ya Wete kwa shehia za mjini ambapo wananchi waliojitokeza wamepongeza utaratibu uliowekwa na Mamlaka ya  Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi  baadhi ya wananchi, walisema utaratibu uliowekwa na NIDA umeasaidia kuondoa usumbufu na msongamano wakati wa kuandikisha.

Walisema utaratibu huo ni tofauti na ule wa uwandikishaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambapo wananchi wengi hata kama hawana sifa waliandikishwa.

“ Hakuna budi tuipongeze NIDA kwa kuweka utaratibu na mazingira mazuri ambayo yatasaidia kuandikisha na kuondoa usumbufu wa kuweka msongamano wakati wa zoezi hili, ”alisema mmoja wa wananchi.


Naye  Mwenyekiti wa masheha wilaya ya Wete ambaye pia ni sheha  wa shehia ya mjini Ole, Khamis Shaaban Hamad, aliwataka wananchi wenye sifa za kuandikisha wafike vituoni kama utaratibu uliowekwa na masheha wa shehia zao.

Alisema kila shehia imejipangia utaratibu wake ambapo wananchi watakuwa wanaenda kwa mujibu wa vijiji na kwamba utaratibu huo utawafanya wananchi wote kupata haki yao bila ya usumbufu.

Aidha sheha wa shehia ya Mtambwe Kusini, Othman Ali Khamis, aliwataka wananchi wenye sifa kufika kwenye vituo vya kuandikisha wakiwa na vitambulisho vyote vinavyotakiwa.


Zoezi la uwandikishaji wa vitambulisho vya taifa  limeanza katika wilaya ya Wete baada ya kumalizika katika wilaya ya Chake Chake na limeanza katika shehia za mjini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.