Habari za Punde

SHABA yamfumba mdomo Babu Shube

 Baadhi ya mashabiki waliojitokeza kufuatilia pambano la kirafiki kati ya Malindi na Shaba uwanja wa Amaan
 KIKOSI cha wachezaji wa Shaba Fc kilichomziba mdomo Babu Shube wa Malindi uwanja wa Amaan kwa kichapo cha bao 2-1
WANANDINGA wa Malindi waliotolewa nishai na wazee wa dago Shaba kwenye pambano la kirafiki uwanja wa Amaan
.(Picha zote na Ali Cheupe)
Na Ali Cheupe

TAMBO na majigambo yaliyotolewa na kocha mkuu wa timu ya Malindi Mohammed Shuberi maarufu babu Shube kwamba ataifunga Shaba kuanzia mabao matatu kwenda mbele zimegonga ukuta kufuatia timu hiyo ya Malindi kutolewa denda na wavuvi hao wa Kojani.
 
Wakicheza mbele ya mashabiki lukuki huko uwanja wa Amaan timu ya Shaba waliweza kutoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wapiga pweza hao wa funguni mjini Unguja.

Malindo ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kwenye dakika ya 17 kupitia kwa mchezaji wake Salum Nia. Kuingia kwa bao hilo kuliamsha hamasa kwa wachezaji wa Shaba na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha kwenye dakika ya 22 kupitia kwa mshambuliaji wake Kheir Shaame. 
 
Wakati ngoma ya mdundiko ikizidi kuwapa morali Shaba wazee hao wa dago waliweza kupata bao la pili kupitia tena Kheir Shaame mchezaji aliyeonekana kuwa mwiba mchungu kwa Malindi.

Timu ya Shaba imepanda daraja na inatarajiwa kucheza ligi kuu msimu wa  2014/2015 huku Malindi ikiwa tayari ndani ya daraja hilo.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.