Habari za Punde

Zanzibar isiwe shamba la Madawa ya Kulevya

Na Salim Said Salim
 
KAMA msimu wa mvua unavyokuja kwa kishindo na kuondoka pole pole, ndivyo ilivyo kwa suala la matumizi na biashara ya dawa za kulevya Zanzibar.
 
Kwa mara nyingine tena suala la matumzi na biashara ya dawa hizi haramu ambazo zimekuwa zikiharibu maisha ya mamia ya watu, hasa vijana, limeibuka tena katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea hivi sasa Zanzibar.
 
Baadhi ya wawakilishi, wakizungumza kwa masikitiko makubwa na hasira, wamedai kuwa bado hapajafanywa juhudi za kutosha za kupambana na janga hili.
 
Wawakilishi wamedai kuwa eneo wanalopitia watu muhimu katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar (VIP) linatumiwa kuingiza na kusafirisha nje dawa za kulevya kwa usalama.
 
Hizi ni shutuma nzito ambazo hazifai hata kidogo kupuuzwa na hili linapata uzito ukitilia maanani kuwa serikali ilipoanzisha utaratibu wa kupekua mizigo na wasafiri wanaostahiki kutumia eneo hilo la VIP baadhi ya waheshimiwa walionekana kutofurahishwa na hatua hiyo.

Wapo waheshimiwa wachache walioona kupekuliwa mizigo yao wakati wakiondoka au wakija Visiwani ni sawa na kuwadhalilisha hawa mabwana na mabibi wakubwa wa nchi hii.
 
Kwa watu wanaojiheshimu na kufahamu kwanini wanaitwa waheshimiwa basi hatua hii ingeliwafurahisha kwa vile inawapa nafasi nzuri ya kuuhakikishia umma wanaoutumikia kwamba na wao ni raia safi na hawapaswi kutiliwa shaka.
 
Ukweli ni kwamba matumizi ya dawa za kulevya kwa watu wa Visiwani, mijini na mashamba, yanaathiri watu wa jinsia na rika zote, lakini zaidi vijana.
 
Taarifa mbalimbali zinaeleza kwamba matumizi ya dawa hizi hatari Visiwani yanakua kwa kasi ya kutisha.
 
Hivi sasa tuaambiwa wapo watu wapatao 4,000 Zanzibar (kama sio zaidi) wanaotumia dawa za kulevya na wengi wao tayari wameshaathirika kimwili na kiakili.
 
Zaidi ya thuluthi moja ya wagonjwa wa akili wanasemekana kuwa chanzo cha kufikia hali hiyo, ni matumizi ya dawa hizi za kulevya.
 
Hii sio idadi ndogo kwa visiwa hivi vyenye watu milioni 1.3, ambavyo hapo zamani vilisifika sana kwa usafi, upole na uadilifu wa watu wake.
 
Leo hii hali ni tofauti kabisa. Mamia ya vijana wake wameathrika na dawa hizi hatari na kusababisha wengine kupoteza akili au maisha. Ni kawaida siku hizi kupita katika baadhi ya vijiwe vya Zanzibar na kukuta vijana wanasinzia ovyo mchana kweupe, na hao wachache waliokuwa macho wanazungumza mambo ya ajabu ajabu kwa ile akili zimeanza kuwapiga chenga.
 
Baadhi ya vijana wanaotumia dawa za kulevya wamezusha simanzi katika familia zao na wengine kuzitia umasikini kwa kuiba fedha vitu vya thamani na kuviuza kwa bei poa ili wapate fedha za kununulia dawa hizi ambazo bei yake ni kubwa sana kwa mtu masikini.
 
Hii leo baadhi ya maeneo ya Zanzibar yamekuwa maarufu sio kwa washoni wazuri wa cherahani, wasusi stadi wa nywele au waimbaji maarufu wa taarabu, bali kwa kuwa na vituo vya vijana wanaotumia dawa hizi hatari.
 
Siku hizi, zipo sehemu zinazojulikana kwa majina ya Peshawar, Colombo, Kandahar na Kunduz, yote haya ni maeneo maarufu ya nchi za nje zinazojulikana zaidi kwa kuzalisha au kutumia dawa za kulevya duniani.
 
Mara nyingi na hata hivi karibuni pamesikika habari za watu kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar wakiwa na dawa za kuleya kwenye mizigo au matumbo yao.
 
Lakini kesi zao humalizika kimya kimya na wanaoonekana kufunguliwa mashitaka na kufungwa jela ni watumiaji wa dawa hizi na sio wauzaji au wale wanazoziingiza nchini.
 
Baya zaidi ni pale unaposikia kuwa pipi zinazofikiriwa kuwa za dawa za kulevya ambazo zilitoka kupitia njia ya haja kubwa kutoka kwa watu walioziingiza nchini kwa kuzificha matumboni mwao zilikuwa na saruji ndani yake!
 
Hivi kweli mtu anaweza kuhatarisha maisha yake kwa kubeba pipi ambazo ndani yake zina saruji inayoingia katika nusu kijiko cha chai? Au saruji hii ni dhahabu au almasi?
 
Hapa upo mchezo mchafu unaochezwa na watu wachache katika jamii ambao lazima ukomeshwe kama kweli Zanzibar inakusudia kupambana na biahara na matumizi ya dawa hizi hatari zinazoangamiza na kuharibu maisha ya watu.
 
Serikali inapaswa kukaza kamba na kuhakikisha watu wanaofanya biashara hii haramu wanawajibishwa kisheria ili kuinusuru jamii na kulisafisha jina la Zanzibar katika jumuiya ya kimataifa.
 
Hivi sasa tayari pamejengwa propaganda ya Zanzibar kuwa kituo maarufu cha biashara za dawa za kulevya, lakini hao wanaoieneza sifa hii mbaya kwa Zanzibar hawatuelezi ilikuwaje hata hizo dawa zikapenya kutoka huko zilikotoka na kufika Zanzibar.
 
Kama pangekuwepo udhibiti mzuri katika viwanja vya ndege vya nchi hizo wasafiri wanaobeba dawa hizo kuzileta Zanzibar wasingefanikiwa kufanya hivyo.
 
Kuinyooshea kidole cha lawama Zanzibar sio haki, hasa ukitilia maanani huko zinakotoka dawa hizi vipo vifaa vya kisasa na wataalamu wazuri zaidi wa masuala haya ya kudhibiti dawa za kulevya.
 
Hata hivyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na taasisi zake lazima ikaze kamba na kuonekana inafanya juhudi za kweli za kupambana na biashara hii haramu ambayo imeathiri vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya sasa na kesho.
 
Jambo jingine baya zaidi ni kuwa katika nchi yoyote ile ambapo matumizi ya dawa hizi huwa makubwa basi huwepo ongezeko la uhalifu na maradhi mbalimbali.
 
Kila raia anao wajibu wa kusaidia vita hivi na sio vyema kujaribu, kama ilivyo kawaida ya watu wa Zanzibar, kuligeuza suala la mapambano dhidi ya dawa za kulevya kuwa la kisiasa. Utashi wa kisiasa usiwapotezee njia sahihi ya kupita.
 
Hili ni tatizo la kijamii na linamhuhsu kila Mzanzibari mwenye uchungu na nchi yake. Njia nzuri ya kulitafutia dawa ni kwa watu kushirikiana na sio kunyoosheana vidole vya lawama na shutuma zisizokuwa na ushahidi na kutengeneza orodha ya kubuni ya huyu ndiye na yule siye.
 
Zanzibar ni ndogo na watu wake wengi wanajuana. Kama kila mmoja atafanya wajibu wake katika vita dhidi ya dawa za kulevya yatapatikana mafanikio, lakini kama kila mtu atamtupia mzigo huu mwenzake na yeye kuamua kuwa mtazamaji basi kila mtu atakuja kujijutia hali hii siku zijazo.
 
Moja ya njia nzuri ya kupambana na matumizi na biashara ya dawa hizi hatari ni watu kuacha kuoneana muhali kwa kutazama kwa misingi ya udugu, urafki au ujirani.
 
Mtu anayeshiriki katika biashara ya dawa hizi hatari hawezi kuwa rafiki mzuri au raia mwema, bali ni adui wa nchi ambaye hafai kulindwa wala kufumbiwa macho.
 
Kwa kushirikiana tu na sio kulaumiana ndio Wazanzibari wataweza kulidhibiti wimbi hili la maafa la dawa za kulevya. Vinginevyo, kila mtu atakuja kujuta kwa kuiachia hali hii kukua na kustawi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.