Habari za Punde

Wanamichezo wenye ulemavu wa akili Zanzibar wakabidhiwa michango yao

 Meneja wa Benki ya Taifa ya Biashara { NMB } Tawi la Zanzibar Rajab Maalim akielezea mikakati ya Benki yake katika kusaidia masuala ya Kijamii wakati wa hafla ya kukabidhi michango kwa wanamichezo wa Zanzibar wenye ulemavu wa akili  Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Vuga Mjini Zanzibar.
 Meneja wa Tawi la Benki ya Taifa ya Biashara { NMB } Zanzibar Rajab Maalim akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Mchango wa shilingi 2,000,000/- kwa ajili ya wanamichezo hao wenye ulemavu wa akili Zanzibar.

Kati kati yao ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar { BTMZ } Sharifa Khamis.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na baadhi ya wanamichezo wenye ulemavu wa akili wanaotarajiwa kuiwakilishi Zanzibar katika mashindano ya Taifa mkoani Kibaha.

 Mwanamichezo Ahmada Bakari wa kwanza kushoto na Haji Hamid Khatib wenye ulemavu wa akili walioshinda medali za dhahabu na fedha kwenye mashindano ya Dunia ya Olympic ya michezo yao Nchini Ugiriki wakifuatilia hafla ya kukabidhiwa michango kwa timu yao inayotarajiwa kushiriki michezo ya Kitaifa Mkoani Kibaha.
Mchezaji Mussa Haji mlemavu wa akili akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake mara baada ya timu yao kupokea michango mbali mbali kwa ajili ya kushiriki michezo ya kitaifa mkoani Kibaha hapo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
 
Washirika wa michezo ndani na nje ya nchi bado wana fursa kubwa ya  kuendelea kujitolea kuunga mkono nguvu zao katika sekta ya michezo ili kulijengea heshima nzuri ya kimichezo Taifa katika medani ya michezo  Kimataifa.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar katika hafla fupi ya kukabidhi michango uliotolewa na taasisi mbali mbali kusaidia Timu ya Wanamichezo wenye ulemavu wa akili Zanzibar wanaotarajiwa kushiriki katika mashindano ya Taifa Mkoani Kibaha hivi karibuni.
 
Wanamichezo hao 55 wa Zanzibar wa michezo ya riadha, soka, basketball na Volleball watajumuika pamoja na wenzao wa mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara katika mashindano ya michezo hiyo ili kupata timu ya Taifa ya Tanzania itakayoshiriki mashindano ya Olympic ya wanamichezo ya watu wenye ulemavu wa akili Duniani yanayotarajiwa kufanyika Nchini Marekani Mwezi Juni mwaka ujao.
 
Balozi Seif alisema wanamichezo wengi hapa nchini hasa wale wenye ulemavu wa akili wana uwezo mkubwa wa kuitangaza na kuipatia sifa nyingi Nchi endapo wataungwa mkono  pamoja na kupatia mafunzo maalum ya kina yanayohitaji zaidi uwezeshaji.
 
“ Ulemavu sio mwisho wa kila kitu. Watu hawa wanaweza wakawa wataalamu wakubwa na wanamichezo mashuhuri wa kimataifa iwapo watafunzwa na kuandaliwa mazingira mazuri ya Kitaaluma “. Alisema Balozi Seif.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizishukuru na kuzipongeza juhudi zinazochukuliwa na Taasisi, jumuiya na mashirika ya umma na hata yale binafsi yanayokubali kujitolea muda wote katika kuunga mkono sekta ya michezo hapa Nchini.


Aliwashauri wanamichezo hao wenye ulemavu wa akili watakaojumuika pamoja na viongozi na baadhi ya wazazi wao katika safari hiyo kujitahidi kuendelea kupenda mazoezi kila wakati ili wajiimarishe katika kushiriki mashindano tofauti ya Kitaifa na Kimataifa na hatimae kuliletea sifa Taifa.
 
Balozi Seif alielezea matumaini yake kwa wana michezo hao wenye ulemavu wa akili Zanzibar kwamba kinachowapeleka mkoani Kibaha ni kushindana na hatimae kuleta vikombe hapa Zanzibar si vyenginevyo.
 
“ Sina shaka kwa umahiri wa walimu wenu naamini kuwa siku ikifika tutawapokea kwa shangwe na furaha baada ya kushinda kwenye mashindano yenu yanayokukabilini muda mfupi ujao “. Alifafanua Balozi Seif.
 
Katika kuunga mkono wanamichezo hao wenye ulemavu wa akili wanaoshiriki mashindano ya Taifa Mkoani Kibaha Balozi Seif alichangia Shilingi Laki 500,000/-, akitanguliwa na Uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara { NMB } iliyokabidhi shilingi Milioni 2,000,000/-, Chama cha michezo cha walemavu wa akili Shilingi Milioni 1,000,000/-.
 
Taasisi nyengine zilizoahidi kusaidia ni pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF }, Mamlaka ya Uwekezaji Vitega uchumi Zanzibar { ZIPA } pamoja na Kampuni ya Azam waliojitolea kuwasafirisha wachezaji hao kwa nusu nauli kati ya Pemba na Unguja, na Unguja - Dar.
 
Akitoa shukrani kwa niaba ya wanamichezo hao Makamu Mwenyekiti wa Chama cha wanamichezo wenye ulemavu wa akili Zanzibar Saada Hamad aliihakikishia Serikali pamoja na wapenda michezo Zanzibar kwamba Timu yake itarudi Zanzibar na ushindi mzuri.
 
Hata hivyo Saada Hamad alisema changa moto kubwa inayowakabili  wanamichezo wenye ulemavu wa akili hapa nchini ni pamoja na ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara yanayohitajika kupatiwa watu hao wenye mahitaji maalum.
 
Mapema Mratibu wa mchezo ya Olympic Tanzania wa mahitaji maalum kutoka chama cha wanamichezo Walemavu Amour Khamis alisema lengo la mashindano hayo ni kuwaunganisha pamoja wanamichezo wenye mahitaji maalum hapa Nchini.
 
Hata hivyo Amour Khamis alieleza kwamba kupanda kwa gharama za mashindano hayo yaliyokuwa yakifanya kila mwaka nchini katika kukabiliana na hali hiyo hivi sasa yameamulika kupangwa kufanyika kila baada ya miaka minne yakizunguuka mikoa mbali mbali Nchini Tanzania.
 
Vijana wawili wa Zanzibar Ahmad Bakar na Haji Hamid Khatib waliowahi kushiriki mashindano ya Dunia ya Olympic ya michezo ya watu wenye ulemavu wa akili Mjini Athens Nchini Ugiriki tayari waliwahi kufanikiwa kuipatia Tanzania Medali ya Dhahabu na Fedha kwenye michuano hiyo ya Ulimwengu.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.