Na
Haji Nassor, Pemba
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kisiwani Pemba, imekiri kupokea barua ya
kutaka ufafanuzi wa kisheria, kutoka kwa ndugu na jamaa wa marehemu Omar Bakar
Omar, alieuawa akiwa mikononi mwa polisi, wakidai wamegundua mchezo mchafu juu
ya tukio hilo .
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Mdhamini wa ofisi hiyo kisiwani humo, Albaghiri
Yakuot Juma, alisema awali kabla ya kupokea barua hiyo, wawakilishi wa familia
ya marehumu, walifika ofisini kuomba utaratibu wa kuandika barua hiyo.
Alisema
baada ya kuwaelekeza kwa kina, hatimae wiki mbili zilizopita waliwasilisha
barua hiyo, inayolilalamikia jeshi la polisi mkoa wa kaskazini Pemba, kwa
kushindwa kuchukua hatua baada ya kutokea mauaji ya ndugu yao .
Alisema
baada ya wao kuipokea barua hiyo, amemkabidhi mwanasheria wao kwa hatua za
kisheria, ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa Mkuu wa upelezi wa makosa ya jinai
mkoani humo, ili kujua hatua ya uchunguuzi ulipofikia.
Alisema
baada ya hapo, yeye binasfisi aliwasiliana na RCO huyo ingawa alimpa majibu
kwamba ndio kwanza anaripoti kazi, hivyo ni vyema akampa nafasi ili kulifuatilia
kwa kina suala hilo .
Katika
hatua nyengine, aliwaomba ndugu na jamaa wa marehemu kufuatilia suala hilo kila mara kwa vile
ofisi hiyo haina kazi moja.
Mmoja
wa ndugu wa marehemu, Salim Bakari Omar, alisema ni kweli baada ya kuona jeshi
la polisi limewatelekeza juu ya tukio hilo, waliamua kwenda kwa DPP kufuata
utaratibu wa kisheria.
“Tokea
mwezi Machi kaka yetu alipopigwa risasi na polisi wa mkoa wa kaskazini Pemba,
hali imebaki kuwa shwari kama alieuawa alikuwa kuku, hata hatujaulizwa lolote,
ndio maana tukaenda ofisi ya DPP kwa hatua za kisheria,” alisema.
Hivyo,
alisema watahakikisha suala hilo, linafikia kikomo cha kisheria na kuviomba
vyombo vinavyohusika kuhakikisha wanawasaidia, kutokana na kukumbwa na msiba
mzito wa kaka yao .
Kamanda
wa polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan, alisema jeshi la polisi
mkoani humo, haijaitelekeza familia ya marehemu, ingawa uchunguzi wa suala hilo umefanywa makao
makuu ya polisi Unguja.
Alisema
makao makuu ndio itatoa majibu juu ya tukio hilo lililotokea Machi 19 mwaka huu na hapo
ndipo atajulikana nani sheria imchukulie hatua.
Alipopigiwa
simu DCI Ilembo juu ya hatua ya uchunguuzi ulipofikia, alisema hakuna anaepaswa
kujua lolote kutokana na kazi anayoifanya yeye na tume yake.
Alimwambia
mwandishi wa habari hizi, kwamba taarifa za tume yake hazimuhusu huku
akisisitiza kuwa hawezi kusema tume inaweza kumaliza uchunguzi wa tukio hilo muda gani.
“Sasa
wewe mwandishi umesikia wapi kwamba uchunguzi unawekewa siku, nnanvyokueleza
mimi sina cha kukwambia juu ya tukio hili maana bado uchunguzi unaendelea na
sijui lini utamaliza”, alisema kwa ukali Ilembo.
Hata
hivyo, baada ya kukata simu baadae alimpigia simu mwandishi wa habari hizi,
akamwambia kuwa upelelezi wa tukio unaendelea.
Uchunguzi
wa awali uliofanywa na mwandishi wa habari, umebaini kuwa jalada la kesi hiyo
tayari limeshafikishwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Unguja, ingawa juhudi
za kumpata Mkurugenzi hazikuzaa matunda.
Machi
19 mwaka huu, majira ya saa 3:00 usiku, eneo la Bahanasa shehia ya Piki wilaya
ya Wete, kuliripotiwa kuuawa kwa mzee Omar Bakar Omar (54), baada ya kupigwa
risasi ya ubavuni na polisi waliokuwa doria, baada ya kudaiwa kutaka kuwavamia
polisi, madai ambao yalikanushwa na wanafamilia.
No comments:
Post a Comment