Na Mwashamba Juma
SERIKALI imeandaa mikakati madhubuti kukabiliana
na tatizo la ajira kwa vijana linalorudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Tatizo hilo
limewasababishia vijana wengi kuwa tegemezi kwa kushindwa kubuni mbinu za
kujikwamua na ugumu wa maisha jambo ambalo hurudisha nyuma juhudi zao katika
kujikwamua kimaendeleo.
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Kazi na
Utumishi, Fatma Gharib Bilali, aliyasema hayo katika ukumbi wa Salama Bwawani,
wakati akifunga kongamano la vijana lililokuwa likijadili mpango mkakati wa
ajira kwa vijana Zanzibar .
Alisema suala la ajira kwa vijana sio tu
chanagamoto inayoikabili serikali ya Zanzibar
bali ni tatizo la dunia nzima ambapo moja ya jitihada za serikali ni kuandaa kongamano
la vijana lililowapa fursa ya kutoa mawazo kwa serikali na kujadili pamoja na
kutoa mawazo ya kukabiliana na changamoto hizo.
“Kongamano hili ni juhudi za serikali ya Zanzibar
katika kuwapatia fursa za ajira vijana wake ili kujikwamua na maisha,” alisema.
Alisema kongamano hilo limetoa fursa kwa vijana
kutoa maoni yao juu ya kuboresha rasimu ya mpango mkakati wa ajira kwa vijana
wa Zanzibar ya mwaka 2014/ 2019 pamoja
na kuwataka vijana kuiga mifano ya wenzao waliothubutu na kuweza kukabiliana na
changamoto za ajira nchini.
Alisema serikali kupitia wizara yake, itahakikisha
kuyafanyia kazi mapendekezo na michango iliyowasilishwa kwenye mpango mkakati huo,
sambamba na kufanya jitihada za kuwapatia vijana wake ajira zenye staha.
Aidha alisema kongamano lilianisha fursa za ajira
kwa vijana hasa kwenye sekta ya kilimo, biashara, utalii na ujasiriamali
kupitia vyama vya ushirika na vyuo vya amali.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kazi Duniani
kanda ya Afrika Mashariki, Alex Musindo, alisema ILO limekuwa likitoa kipaumbele
kwa serikali ya Zanzibar katika kuipatia fursa za upatikananaji wa ajira kwa
vijana.
Alisema ni jukumu la wote kutekeleza mpango mkakati
wa ajira kwa vijana na kuufanya kuwa endelevu kwa maendeleo ya nchi na
mustakbali wa vijana katika kujikwamua na ugumu wa maisha.
Akizungumzia suala la ujasiriamali kwa vijana, Mkurugenzi
huyo alisema ujasiriamali sio suluhisho pekee la kutatua changamoto za ajira
kwa vijana, bali ni sehemu ya biashara na kuongeza kuwa taasisi za umma, serikali
pamoja na ajira binafsi zina wajibu wa kuwagomboa vijana na janga la uhaba wa
ajira.
Nae Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama huru vya
Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Khamis Mwinyi wakati akizungumzia sheria za
utekezaji wa sheria hiyo, alisema bado haisimamiwi ipasavyo na kutoa mwanya kwa
wageni kuchukua nafasi za wazawa jambo ambalo huwasababishia vijana kukutana na
hali ngumu ya ukosefu wa ajira.
Alisema taasisi yake inahakikisha mazingira bora
ya kazi kwa wafanyakazi sambamba na kuendeleza jitihada za kupigania maslaahi
ya kazi zao.
Alisema mpango mkakati wa ajira kwa vijana,
unaenda sambamba na vipaumbele vya mikakati ya kimataifa ya kuhakikisha ajira
kwa vijana duniani.
Alisema ZATUC kama sehemu ya ILO itahakikisha inatekeleza
mikakati ya ajira kwa vijana Zanzibar
kwa sasabu ongezeko la ajira kwa vijana linaimarisha vyama vya wafanyakazi.
Katibu wa Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA),
Salahi Salahi, alisema kongamato limewawezesha kujua matatizo na mafanikio ya
vijana kutokana na tatizo la ugumu wa ajira kwa vijana ambalo serikali
inakabiliana nalo.
Alisema vijana wana wajibu wa kuuliza na uendeleza
mpango huo sambamba na kuwataka kuuliza juu mwendelezo wake kwa serikali.
No comments:
Post a Comment