Na Othman Khamis. OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi ametoa wito kwa watendaji wote wa taasisi za umma kujituma, kuwa
makini na kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa ili kuhakikisha kwamba
vipaumbele vilivyowekwa na Serikali katika sekta ya uchumi na ustawi wa jamii
vinatekelezwa kwa ufanisi.
Akifunga mkutano wa 16 wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar uliojadili bajeti ya
Serikali ya Mwaka 2014/ 2015 kwenye ukumbi wa Baraza hilo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
Balozi Seif alisema Serikali itajitahidi kuona nyenzo hasa fedha kwa ajili yab
utekelezaji wa vipaumbele hivyo zinapatiklana kwa wakati.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaimarisha ukusanyaji wa kutoka katika vianzio vyake sambamba na
udhibiti wa uvujaji wa mapato katika taasisi na maeneo yote ili azma
iliyokusudiwa iweze kufikiwa vyema.
Balozi Seif aliwasisitiza Wafanyabiashara
pamoja na wananchi kujenga utamaduni wa kulipa kodi na ada katika huduma zote
za kiuchumi na kijamii lengo likiwa ni kuiongezea mapato Serikali Kuu kwa ajili
ya utekelezaji wa malengo yake iliyojipangia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alifahamisha kwamba Serikali imejipanga kuimarisha miundombinu ya
kiuchumi pamoja na huduma za Kijamii kama vile elimu, afya bora na
upatikanaji wa huduma za maji safi na salama.
Alieleza kwamba hatua hiyo
itakwenda sambamba na uimarishaji wa huduma za makundi maalum hasa kwa wazee
wasiojiweza, watoto na watu wenye ulemavu pamoja na kuimarisha mazingira
ya biashara kwa kuondosha vikwazo visivyo vya lazima.
Akizungumzia suala la migogoro ya ardhi
linaloonekana kuongezeka kutokana na kui8marika kwa shughuli nyingi za kiuchumi
na kijamii Balozi Seif alisema Serikali itaendelea kuchukuwa juhudi katika
kuhakikisha migogoro hiyo inapungua na hatimae kuondoka kabisa.
Alisema zipo dalili zilizobaina ambazo
zimeonyesha wazi kuwa baadhi ya migogoro ya ardhi iliyopo katika maeneo mengi
hapa nchini inasababishwa na wanasiasa wachache wanaopenda kujipatia
umaarufu pamoja na kutawaliwa na ubinafsi.
Balozi Seif alisema umuhimu wa ushirikiano
kati ya masheha,madiwani, viongozi wa serikali, wanasiasa na wananchi
unahitajika wakati Serikali Kuu inaendelea na ukamilishaji wa mpango wake wa
matumizi bora ya ardhi utakaosaidia kupunguza migogoro iliyojitokeza.
“ Naamini kwamba kama
sote tutashirikiana kwa dhati kwa nia ya kuiondoa migogoro ya ardhi
iliyojichomoza tutafanikiwa kwa kiwango kikubwa “. Alisema Mkuu huyo wa
shughuli za Serikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwasihi
wananchi wenye tabia ya kubeza wawekezaji waliopata fursa ya
uwekezaji miradi yao nchini kuwacha kuwabughudhi kwa vile tayari
wamesharidhia kushirikiana na Serikali katika kukuza uchumi.
Alisema Serikali imejitahidi kuwavutia
wawekezaji kuitumia nafasi hiyo nia ikiwa ni kuongeza mapato ya serikali pamoja
na kupunguza mfumko wa vijana wasio na ajira.
Kuhusu suala la amani Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar
alisema Serikali imesikitishwa na kitendo cha kihalifu kilichotokea hivi
karibuni cha mripuko wa bomu kwenye eneo la Darajani MjiniZanzibar ambapo mtu
mmoja aliuawa na wengine saba kujeruhiwa katika mripuko huo.
Alisema tukio hilo ni la kushtusha,
kusikitisha na Serikali inaendelea kulaani kwa nguvu zote kitendo hicho
cha kihaini huku ikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa kuendelea kuwasaka
wahalifu waliohusika na tukio hilo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Balozi Seif aliwathibitishia wananchi pamoja
na wageni wote waliopanga kuitembelea Zanzibar
kwa Visiwa vya Unguja na Pemba bado viko
katika hali ya usalama, amani na utulivu. Hivyo ni vyema wakaendelea na
harakati zao za kimaisha bila ya hofu.
Alieleza kwamba licha ya mafanikio makubwa
yaliyopatikana katika kuenzi umoja, amani na utulivu nchini lakini bado
Viongozi na Wananchi wanapaswa kutowapa nafasi wale watu wanaochochea
mifarakano ambayo inaweza kuvuruga nchi na kudumaza maendeleo ya wananchi.
“ Hatutavitendea haki vizazi vyetu kama tutaiacha nchi hii kudumbukia katika wimbi la vurugu
na uvunjifu wa amani “. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar .
Akielezea masikitiko yake kutokana na
mahudhurio yasiyoridhisha ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kufikia hatua
ya spika kuahirisha baadhi ya wakati Balozi Seif alisema hilo
ni jambo lisilokubalika kidemokrasia, kiuchumi, kisiasa na linalidhalilisha
baraza hilo .
Alisema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni
macho, masikio na midomo ya wananchi wanaowawakilisha majimboni mwao. Hivyo
kuendelea kwa kitendo hicho ni kuwanyima haki wananchi waliowachagua.
Balozi Seif alionya kwamba utoro huo
unaopelekea kuahirishwa kwa vikao hivyo vya Baraza la Wawakilishi vinapoteza
fedha nyingi za walipa kodi ambao ni wananachi.
“ Hatuoni kama ni unafiki tunapopiga kelele
kuwa Serikali inapoteza fedha za wananchi wakati sisi wenyewe pia tunachangia
upotevu huo ? “. Alikemea Balozi Seif.
Katika Mkutano huo wa 16 wa Baraza la Nane la
Wawakilishi uliojadili Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2014/2015 jumla
ya maswali ya msingi 66 na mengine 183 ya nyongeza yalioulizwa na waheshimiwa
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kujibiwa na Mawaziri wa Sekta husika.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa
hadi siku ya Jumatano ya Tarehe 22 Oktoba mwaka huu wa 2014 mnamo saa 3.00 za
asubuhi.
No comments:
Post a Comment