Habari za Punde

Balozi Seif : Serikali itahakikisha inalinda uhuru wa habari

Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
ameonya kwamba vitengo vya  utawala kwenye Taasisi za Habari vimekuwa vikishindwa kuzingatia mambo muhimu wanayopaswa kupatiwa waandishi wa Habari kulingana na mazingira yao ya kazi ili watekeleze vyema majukumu yao kwa ufanisi.
 
Alitoa onyo hilo wakati akizindua rasmi Kitabu cha Historia ya Vyombo vya Habari Zanzibar kilichoandikwa na wazoefu wa tasnia hiyo hapa Zanzibar hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 
Balozi Seif alisema ukosefu wa zana muhimu zinazohitajiwa na waandishi pamoja na maslahi yao na hasa zile posho za msingi limekuwa ni tatizo kubwa kiasi ambacho hujenga matabaka kati ya vitendo vya utawala na taasisi za Habari.
 
“ Ninazo taarifa kwamba hata bajeti zinazoingizwa, sehemu kubwa ya fedha hizo huishia kwenye kazi za utawala na sio kupunguzia matatizo mengi ya vitengo vya habari “. Alisema Balozi Seif.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba wakuu wa taasisi za Habari kuliangalia  vizuri suala hilo na kulipatia ufumbuzi ili waandishi wa Habari wafanye kazi zao kwa raha na furaha.
 
Aliwaomba waandishi wa Habari kuendelea kufanya kazi zao kwa ueledi na uadilifu wakizingatia maadili ya fani hiyo kwa vile wao ni muhimu kwa jamii katika kuelimisha na kutoa habari.

Alihimiza umuhimu wa habari zinazoandikwa kufanyiwa uhakiki mzuri ili zinapowafikia walengwa ziwe zenye kutoa taaluma badala ya kupotosha wale wanaopokea habari hizo.
 
Alifahamisha kwamba Serikali itahakikisha muda wote inalinda uhuru wa Habari, usalama wa waandishi, utii wa sheria na kuhimiza weledi na ufahamu wa mipaka ya kazi za waandishi kwa mujibu wa katiba na sheria.
 
Alieleza kwamba uhuru wa Habari muda mrefu ulikuwa ukiminywa na baadhi ya Viongozi kwa lengo la kuficha maovu yao jambo ambalo halikubaliki katika nchi zilizokubaki kutoa fursa ya kidemokrasia ya Tasnia ya Habari kutekeleza wajibu wake bila ya kuingiliwa.
 
Akigusia sheria ya vyombo vya Habari Zanzibar ambayo iko katika marekebisho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwahakikishia wanahabari Nchini kwamba Serikali itajitahidi kuona kwamba sheria hiyo inaharakishwa ili ifanye kazi zake kama kawaida.
 
Balozi Seif alilipongeza Baraza la Habari Tanzania { MCT } pamoja na washirika wake  wa ndani na nje kwa uamuzi wa busara wa kuandika kitabu muhimu cha Historia ya vyombo vya Habari Zanzibar ambacho kitabakia kuwa urithi wa watu wa Zanzibar.
 
Alisema hakuna anayepinga umuhimu wa sekta ya Habari ulimwenguni ikiwemo Zanzibar. Hivyo alisema ni dhahiri kuwa kazi nzito inayofanywa na sekta hiyo haina budi kuimarishwa kwa kuungwa mkono hasa ikizingatiwa kuwa Habari inahusu kila kada.
 
Mapema Mtafiti Kiongozi wa chapisho la kitabu hicho nguli Bibi Maryam Hamdan alisema historia ya habari Zanzibar imeanza tokea karne ya 12 jambo ambalo historia yake inapaswa kuendelezwa kwa faida ya vizazi vijavyo.
 
Bibi Maryam aliiomba Serikali Kuu kutoa msukumo kwa wataalamu wa kihistoria kufanya utafiti wa masuala mbali mbali ya kitaifa na Jamii ili vizazi vya sasa na vile vitakavyofuatia viweze kufaidika na utafiti huo.
 
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania { MCT } Nd. Kajubi Mukajanga alisema kitabu hicho ni muendelezo wa machapisho mbali mbali ya tasnia ya habari yanayosimamiwa, kuchapishwa na kutolewa na Baraza hilo.
 
Nd. Kajubi alisema Baraza hilo limeunda idara tatu  kwa lengo la kuifanya sekta ya Habari Nchini inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa kiwango kinachokubalika kimataifa.
 
Wakitoa ushuhuda wa masuala ya kihabari hapa Zanzibar magwiji wa fani hiyo katika visiwa vya Zanzibar Bwana Salim Said Salim, Bibi Tatu Ali Abdulla Maarufu Shangazi pamoja na Bibi Nasra Salim walisema fani hiyo imepata changamoto iliyokuwa ikiwakabili baadhi ya wana habari wa zamani.
 
Hata hivyo magwiji hao walisema yapo mafanikio makubwa hivi sasa kutokana na mabadiloiko ya sayansi na teknolojia kiasi kwamba sekta ya habari imekuwa wazi na huru kwa kiasi kikubwa.
 
Hafla hiyo fupi ya Uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Vyombo vya Habari Zanzibar ilihudhuriwa na wana habari mbali mbali , washirika wa sekta hiyo pamoja na baadhi ya Maafisa wa Ofisi za Kibalozi waliopo Nchini Tanzania.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.