Habari za Punde

Hotuba ya Balozi Seif kwenye uzinduzi wa kitabu cha historia ya vyomba vya habari Zanzibar

HOTUBA YA MGENI RASMI, MH. BALOZI   SEIF ALI IDDI  MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR KATIKA UZINDUZI WA KITABU CHA HISTORIA YA VYOMBO VYA HABARI VYA  ZANZIBAR TANZANIA
   18 JUNI, 2014 - ZANZIBAR BEACH RESORT
------------------------------------------
 
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar,
Rais wa Baraza la Habari Tanzania, Jaji Mstaafu Robert Kisanga,
Wajumbe  wa Bodi ya Baraza la Habari Tanzania,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania,
Wadau wote wa habari mliohudhuria hapa,
Ndugu waandishi wa habari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Asaalam Alaikum.
Napenda kuchukua nafasi hii adhimu kumshukuru Mola wetu mtukufu kwa kutuwezesha kukutana hapa leo kushuhudia uzinduzi wa kitabu cha historia ya vyombo vya habari vya Zanzibar.  Nalishukuru Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa heshima iliyonipa ya kuwa mgeni rasmi katika tukio hili muhimu la kihistoria. Sio watu wengi wanaopata bahati ya kushirikishwa katika matukio ya kihistoria kama hili la leo. Ahsanteni sana. 
 
Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki kuandika kitabu hiki kwa ustahamilivu wao. Naelewa kazi ya kuandika kitabu sio kazi rahisi. Usemi wa mwandishi maarufu wa Riwaya kutoka Marekani Bwana Ernest Hemingway unatudhihirishia ukweli wa uzito wa kazi waliyoifanya ndugu zetu hawa.  Mwandishi huyu amesema: “The first draft of anything is shit”. Kwa tafsiri isiyokuwa rasmi ni kuwa “Nakala ya mwanzo siku zote ni kitu kisichofaa”. Naamini waandishi wetu waliandika na kuandika na kuandika usiku na mchana pamoja na kuharibu karatasi nyingi kabla ya kuridhika na ubora wa kazi yao.  Yote haya wameyafanya ili kutoa kitabu kinachokubalika ambacho leo hii tunakizindua.
 
Ndugu Wageni Waalikwa,
 
Kazi  hii mlionipa leo ingekamilika kwa kusema maneno kumi moja tu ambayo ni “nimezindua rasmi kitabu cha historia ya Vyombo vya Habari vya Zanzibar” lakini nahisi kuwa kwa kufanya hivyo bado nitakuwa sijatekeleza kwa dhati na kuifanyia haki shughuli hii kubwa, hivyo ni vyema nikasema machache ili kwa  pamoja tuweze kuifanikisha kikamilifu shughuli yetu hii muhimu ya leo.
 
Kitabu hiki tunachokizindua leo, bila mchango wa  Baraza la Habari Tanzania (MCT) pengine kisingeandikwa.  Nalipongeza sana Baraza hili kwa kusimamia kidete kazi ngumu ya utafiti wa kuandika kitabu hiki na hatimae kufanikisha uzinduzi ambao tunaufanya leo hii. Ahsanteni sana Baraza la Habari Tanzania.
 
Ndugu Wageni Waalikwa,
 
Msomi mmoja Bwana Michael Crichton amesema hivi: “If you don’t know history, then you don’t know anything. You are a leaf that doesn’t know it is part of a tree”.  Kwa tafsri isiyo rasmi Bwana Michael anasema “Kama huelewi historia, basi hujuwi kitu. Wewe ni sawa na jani ambalo halielewi kama ni sehemu ya mti”.
 
Vyombo vya Habari vya Zanzibar vina historia kubwa lakini kama fasihi simulizi.  Historia hii ilibakia midomoni mwa wachache; wengi wetu hatuijuwi. Tulikuwa kama jani lisiloelewa kama ni sehemu ya mmea. Ni jambo la kutia moyo na kupongezwa kuwa leo hii historia ya vyombo vya habari hapa Zanzibar imetolewa hadharani kwa njia ya kitabu.  Hatutokuwa tena majani!
 
Ndugu Wageni Waalikwa,
 
Katika nchi zinazoendelea kama India historia ya vyombo ya habari huwekwa kwenye mitaala ya kufundishia somo la Uandishi wa habari katika ngazi ya shahada. Nadhani sio vibaya nasi historia hii ikafundishwa katika chuo chetu cha uandishi wa habari ili vijana wetu waelewe wapi fani wanayoisomea inakotoka. Kujua historia ya jambo lolote kwa binadamu ni muhimu sana kwa vile unajielewa ulikotoka, wapi ulipo na nini ufanye kwa hatma ya baadae.
 
Wito wangu kwa waandishi wa habari na wasomi wengine nchini kujitokeza kuendeleza historia hii ya habari kwa kuwaandikia historia magwiji wa uandishi wa habari hapa nchini. Kwa kufanya hivi vijana wetu watakuwa na watu waliofanya vizuri wa kuwaiga katika fani yao ambao kwa lugha ya Kiingereza hujulikana kama ‘role model’.
 
Ndugu Wageni Waalikwa,
 
Hakuna anayepinga umuhimu wa sekta ya habari ulimwenguni ikiwemo Zanzibar. Ni dhahiri kuwa kazi nzito inayofanywa na sekta hii haina budi kuimarishwa kwa kuungwa mkono hasa ikizingatiwa kuwa sekta ya habari inahusu kada na nyanja zote za maisha ya binaadamu pamoja na maendeleo yake kwa ujumla.
 
Pengine tufikiri tu ingekuwaje bila ya kuwepo vyombo vya habari? Je, maisha yetu yatakuwa ni yenye raha na furaha? Au yatagubikwa na wimbi zito la upweke na simanzi? Jawabu ya suala hili ni kugubikwa na wimbi zito lililojaa simanzi.
 
Historia ya masuala ya habari hapa Zanzibar yaani Unguja na Pemba ilianza karne na karne zilizopita na ni kongwe kuliko eneo lolote lingine la Afrika ya Mashariki na Kati. Kwenye karne ya 13 kwa mfano, enzi za Mwinyi Mkuu  mwaka 1204  hadi 1873 Zanzibar ilitumia zana mbali mbali za kimapokeo kwa ajili mawasiliano ya umma, ikiwemo ngoma, honi, upatu, tutu, gunda na kadhalika.
 
Vifaa hivi vilitumika katika jamii  kwa ustadi mkubwa kwani ilipopigwa ngoma, upatu au gunda watu walijua nini kimejiri ama ni suala la  biashara, mavuno, sherehe au msiba.  Kwenye masuala ya sherehe kwa mfano jamii ilikuwa ikitumia marimba hasa kisiwani Pemba. Kifaa hiki kilichotengenezwa kwa mpangilio maalum wa mbao kilitumika pia kwa kuamshia daku katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
 
Kwa upande wa magazeti historia inatuonesha kuwa Zanzibar ilikuwa ni chemchem ya vyombo vya habari.  Mwaka 1888 hadi 1963 zaidi ya magazeti 50 yalikuwa yakichapishwa na kutolewa hapa hapa Zanzibar.
 
Gazeti la kwanza lililochapishwa na kanisa la Anglican kwa lugha ya Kiingereza lilikuwa ni MSIMULIZI, na mengine yalifuata kwa kutumia lugha ya Kigujerati, Kiarabu na Kiswahili.  Magazeti haya yaliakisi wakati husika kisiasa kijamii na kiuchumi.
 
Ndugu Wageni Waalikwa,
 
Kama tunavyoelewa kwamba ulimwengu unatambua fika kuwa katika tasnia ya habari, nyanja ya utangazaji ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.  Katika kuzingatia msingi huu, Zanzibar ilianza na shughuli za utangazaji kwa kutumia vipaza sauti.  Hii ilikuwa mnamo mwaka 1945.
 
Watu walikusanyika ili kupata habari za maendeleo ya vita vya pili vya dunia katika nyumba ya Beit el Ajaib (nyumba ya maajabu) iliyopo Forodhani katika eneo la mji mkongwe wa Zanzibar.
 
Matangazo ya mwanzo kwa kutumia mawimbi yalianza kurushwa Machi 15 mwaka 1951 na yalitolewa na iliyokuwa Sauti ya Unguja ambayo sasa ni ZBC.  Matangazo kwa njia ya televisheni yalizinduliwa rasmi mnamo mwaka 1974.
 
Matangazo hayo yalikuwa na lengo la kuunga mkono kampeni ya elimu kwa umma.  Katika miaka hiyo kulikuwa hakuna sera ya utangazaji. Sheria na kanuni za kawaida ndizo zilizoongoza sekta ya utangazaji.
 
Kwa sasa Zanzibar ina vituo zaidi ya 18 vya utangazaji, vituo vya television vitano na zaidi ya majarida 30 ambavyo vinatoa huduma ya matangazo ya kibiashara na kijumuiya kwa njia ya redio, televisheni, magazeti na majarida. Lililo muhimu na ambalo napenda kusisitiza ni kwa sekta ya habari hapa nchini  kujua malengo yao katika kutetea demokrasia, utawala bora wa haki na sheria.
 
Aidha, napenda pia kusisitiza kuwa vyombo vya habari hapa nchini ni lazima vielekeze nguvu zao kwa vitendo katika kuhubiri maelewano ya wananchi bila ya kujali imani zao za dini, makabila au mafungamano yao ya kisiasa.
 
Ndugu Wageni Waalikwa,
 
Naamini kuwa kila kazi iwe ya matumizi ya akili kama hii ambayo waandishi wa kitabu hiki  wametumia au ya misuli au mashine huwa na changamoto zake. Hata hivyo, napenda niwashukuru kwa dhati wale waliochangia kwa namna moja au nyengine katika kufanikisha kazi hii.
 
Katika kada hii ya habari, huko tunakotoka na hapa tulipo kuna wakati tumeshuhudia kwamba uhuru wa habari ukiminywa kwa sababu mbali mbali, baadhi ya wakati sio na Serikali au Taasisi bali na watu waliopewa dhamana na Serikali au Taasisi ziwe za Kiserikali au za kiraia.
 
Baadhi yao hufanya hivyo kuficha maovu wanayoyatenda jambo ambalo linadumaza maendeleo kwa jamii.  Jambo hilo halikubaliki kwenye nchi ya kistaarabu.
 
Ndugu Wageni Waalikwa,
 
Uhuru wa habari hapa Zanzibar, ijapokuwa sio wa kiwango ambacho wanataaluma wa habari hapa kwetu na wananchi wanakililia umeainishwa kwenye Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Kwa bahati mbaya kama wanasheria wanavyosema zipo sheria ambazo kwa tafsiri iliopo ni kuwa haki inatolewa kwa mkono mmoja na kuondolewa kwa mkono wa pili.
 
Ndio maana kwa kuondoa wasiwasi au dosari hiyo, hivi sasa hapa Zanzibar na Tanzania kwa jumla upo mchakato wa kuzirekebisha  sheria hizo ziende na wakati ili ziweze kukidhi haja ya jamii bila bughudha yoyote kutoka Serikalini au Taasisi, na mimi nataka niseme kwamba sheria ya vyombo vya habari hapa Zanzibar ambayo iko katika hatua nzuri kukamilika itaharakishwa ili tufikie malengo yetu tuliokusudia ya kimaendeleo, amani, utulivu na mshikamano.
 
Ndugu Waalikwa,
 
Wakati tukizindua       kitabu hiki cha historia ya Habari Zanzibar nizungumzie kidogo juu ya Waandishi wetu wa habari ambao wakati mwingine hufanya kazi katika mazingira magumu.  Vitengo vya Utawala kwenye Taasisi za habari vinashindwa kuzingatia mambo muhimu ya waandishi wa habari, kama vile kuwapatia zana muhimu wanazozihitaji, maslahi yao na hasa posho za msingi kulingana na mazingira ya kazi zao.  Hili ni tatizo ambalo limefikia kiasi ambacho limekuwa likijenga matabaka kati ya vitengo vya utawala ndani ya taasisi za habari na waandishi wa habari.  Ninazo taarifa kwamba hata bajeti zinapoingizwa, sehemu kubwa ya fedha hizo huishia kwenye kazi za utawala na siyo kupunguzia matatizo ya vitengo vya habari.  Ningewaomba sana Wakuu wa Taasisi za Habari waliangalie vizuri suala hilo na kulipatia ufumbuzi ili waandishi wetu wa habari wafanye kazi kwa raha na furaha.
 
Ndugu Wananchi,
 
Kwa upande wa waandishi wenyewe, ningewaomba waifanye kazi yao ya uandishi kwa ueledi na uadilifu kwa kufuata maadili ya uandishi wa habari waliyofundishwa, kwani wao ni muhimu kwa jamii kwa kazi yao ya kuelimisha na kuhabarisha jamii.  Habari zisiwe za kuipotosha jamii.  Habari ziwe sahihi ambazo kabla ya kuandikwa ziwe zimefanyiwa utafiti wa kina.
 
Kwa upande wa Serikali, itahakikisha inalinda uhuru wa habari, usalama wao, utii wa sheria na kuhimiza weledi na ufahamu wa mipaka ya kazi za waandishi wa habari kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
 
Ndugu Waalikwa,
 
Kwa dhati kabisa, nawashukuru tena Baraza la Habari Tanzania pamoja na washirika wake wa nje na ndani  kwa uamuzi wa busara wa kuandika kitabu muhimu cha historia ya vyombo vya Habari vya Zanzibar ambacho kitabakia kuwa urithi wa watu wa Zanzibar.
 
Kwa kumalizia, napenda kuwashukuru tena waandaaji wa shughuli hii muhimu kwa heshima walionipa ya kuwa Mgeni rasmi.  Nakutakieni nyote kila la kheri na mafanikio mema katika juhudi zenu za kuelimisha jamii kupitia vyombo vya habari.
 
Baada ya kusema hayo, sasa, kwa heshima natamka kuwa kitabu kinachohusu historia ya vyombo vya habari vya Zanzibar nimekizindua rasmi. 
 
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.