Habari za Punde

Dkt.Shein akutana na Makamu Mkuu wa Rais ZTE

  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein akisalimiana na Makamu Mkuu wa Rais wa kampuni ya ZTE Bw.Huang Dabin,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi kwa mazungumzo na Rais,[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein akifuatana na Makamu Mkuu wa Rais wa kampuni ya ZTE Bw.Huang Dabin,(kushoto) baada ya kumaliza mazungumzo yao leo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                              02 Juni, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema wakati Serikali imeelekeza nguvu zake katika kujenga miundombinu ya mifumo ya tekinolojia ya habari na mawasiliano nchini changamoto kubwa ni kuielimisha jamii kuamini kuwa matumizi ya tekinolojia hiyo kuwa ni muhimu katika kufanikisha shughuli zao za maisha ya kila siku.
 
Akizungumza na Makamu wa Rais Mwandamizi wa Kampuni ya ZTE ya China Bwana Huang Dabin ofisini kwake Ikulu leo Dk. Shein amesema mradi wa ujenzi wa mindombinu ya Mfumo wa Mawasiliano ya Habari na Tekinolojia unaotekelezwa na Kampuni ya ZTE kutoka China unalenga katika kutoa fursa kwa Serikali na wananchi wa Zanzibar kufaidika na matumizi ya sayansi na tekinolojia.
 
Alieleza kuwa kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo ambao unajulikana zaidi kwa jina la e-government ambao unajumuisha uwekaji wa mkonga wa mawasiliano pamoja na kuunganisha mkonga huo na miundombinu ya mfumo wa mawasiliano Zanzibar ni hatua muhimu katika ya kuiweka Zanzibar katika ramani ya matumizi ya tekinolojia hiyo, hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi na kuharakisha maendeleo.
 
Dk. Shein aliishukuru kampuni ya ZTE kwa kukamilisha awamu ya kwanza ya mradi huo ambao hivi sasa unaingia katika awamu nyingine ambayo itajumuisha matumizi ya tekinolojia hiyo katika sekta ya afya na kodi.
 
Alibainisha kuwa hiyo ni hatua nzuri ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha matumizi ya tekinolojia ya habari na mawasiliano katika shughuli za Serikali ili kuongeza ufanisi katika utendaji na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
 
Kwa hivyo, alitoa wito kwa Kampuni ya ZTE katika kutekeleza awamu ya pili ya mradi, kuweka mkakati wa kuelimisha jamii juu ya matumizi ya tekinolojia ya habari na mawasiliano kwa kuwa mwamko wa matumizi ya teknolojia hiyo miongoni mwa watumishi na viongozi wa Serikali pamoja na wananchi bado si wa kuridhisha.
 
Aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kukamilisha awamu ya pili ya mradi huo ili kutoa fursa kwa mradi huo kuendelea kwa awamu nyingine ambayo itazihusisha sekta za elimu na utalii.
 
Mhe. Rais alimuhakikishia Bwana Huang kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kufanya kazi na kampuni hiyo na ameikaribisha kuangalia maeneo mengine ambayo kampuni hiyo ina utalaamu na uzoefu ambayo inaweza kushirikiana na Serikali kama uvuvi, utalii na  afya.     
 
Wakati huo huo Makamu wa Rais Mwandamizi wa Kampuni ya ZTE Bwana Huang Dabin ameeleza kuwa ameridhishwa kuona kampuni yake imeweza kukamilisha awamu ya kwanza ya mradi huu ambapo sasa mradi umeingia katika awamu ya pili.
 
Alibainisha kuwa katika awamu ya pili, mradi unahusisha kuzifikishia Ofisi na taasisi za Serikali huduma za mkonga wa mawasiliano na kuuwezesha mfumo wa kodi nchini kutumia tekinolojia hiyo pamoja na kuiwezesha Wizara ya Afya kutumia tekinolojia hiyo katika kutoa huduma kwa wagonjwa.
 
Alifafanua kuwa chini ya matumizi ya mfumo huo wa mawasiliano katika sekta ya afya, kumbukumbu za mgonjwa zitaweza kupatikana katika hospitali yoyote atakayokwenda mgonjwa bila ya kulazimika kutembea na mafaili yake.
 
Bwana Huang alisisitiza kuwa azma ya kampuni yake ni kuifanya Zanzibar iweze kutumia mfumo wa tekinolojia ya habari na mawasiliano katika shughuli zote na kuifanya Zanzibar ing’are katika matumizi ya tekinolojia hiyo.
 
Kwa hivyo alibainisha kuwa Kampuni yake imekusudia kujenga vituo sita vya kijamii vya matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo watoto na vijana watajifunza na kuvitumia ili kuhamasisha matumizi ya tekinolojia hiyo.  
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
  E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz& sjka1960@hotmail.com
No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.