Habari za Punde

Hotuba ya Dk Shein, uzinduzi wa kongamano la kumenzi Dk Livingstone

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN
KATIKA UZINDUZI WA KONGAMANO LA KUMUENZI
DK. DAVID LIVINGSTONE HOTELI YA
GRAND PALACE TAREHE 06 JUNI, 2014
--------------------------------
 
Mheshimiwa Askofu Michael Henry Hafidh,
 
Waheshimiwa Maaskofu wa Kanisa la Anglikana mliohudhuria,
 
Viongozi mbali mbali wa Dini na Serikali,
 
Ndugu Wananchi,
 
Tuna wajibu mkubwa wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na uzima tukaweza kujumuika leo  hii. Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa viongozi wa Kanisa la Anglikana wa Dayosisi ya Zanzibar na waumini wote wa Kanisa hili kwa kunialika kuja kuungana nanyi katika uzinduzi wa kongamano la kumuenzi Dk. David Livingstone kwa kutambua mchango wake katika kukomesha biashara ya utumwa.
 
Napenda kutoa pongezi kwa maandalizi mazuri ya kongamano hili pamoja na uteuzi mzuri wa mada ambazo zimeandaliwa kuwasilishwa na baadae kuchangiwa na washiriki wa kongamano hili.  Nawapongeza wahadhiri wote waliochaguliwa kuwasilisha mada katika kongamano hili kwa heshima kubwa waliyopewa.  Kadhalika, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wageni wetu wote waliotoka nje ya Zanzibar kuja kushiriki kwenye Kongamano hili.  Wote nawashauri watumie fursa hii kutembelea na kuona maeneo mbali mbali ya kihistoria na utajiri wa maumbile ambao Mwenyezi Mungu ameitunukia Zanzibar.
 
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Sote tuna wajibu wa kuwapongeza marafiki wa Dk. David Livingstone (FDDL) kwa kubuni utaratibu huu wa kufanya maadhimisho ya miaka 141 tangu kukomeshwa kwa biashara ya utumwa hapa Zanzibar.  Vitabu vya historia vinaeleza kuwa Soko Kuu la Watumwa la Afrika ya Mashariki lililokuwepo hapa Zanzibar, lilifungwa rasmi tarehe 06 Juni (tarehe ya leo) mwaka 1873.  Hatua hiyo ina mchango muhimu unaotokana na wamishionari wa madhehebu ya UMCA pamoja na juhudi za Dk. David Livingstone.
 
Nimefurahi kusikia kuwa utaratibu huu wa kufanya maadhimisho haya kila mwaka ni wa kupokezana ambapo mwaka jana; 2013 ilikuwa ni zamu ya wenzetu wa Bagamoyo na mwaka huu wa 2014 ni zamu ya Zanzibar.  Hali hii inadhihirisha kuwepo kwa uhusiano mkubwa wa kihistoria baina ya wananchi wa Tanzania Bara yakiwemo maeneo ya mwambao kama vile Bagamoyo.  Vile vile, hali hii ni kutokana na nafasi ya Zanzibar kuwa ni kitovu cha ziara za wageni wengi kupitia hapa katika ziara zao za maeneo mbali mbali ya Afrika Mashariki na Kati kama ilivyokuwa kwa Mmishionari huyo, Dk. David Livingstone aliyepita Zanzibar kati ya mwaka 1853 na 1856.
 
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Sisi, tukiwa viongozi na wanadamu tunajifunza kutokana na shughuli hii. Kuna  haja ya kiongozi kuacha sifa njema ili baadae watu waweze kukumbuka na kuiga mema yako kwa manufaa na ustawi wa wanaadamu wenzako.  Leo tupo hapa kufanya shughuli ya kumuenzi Dk. David Livingstone kutokana na mchango wake katika harakati za kukomesha biashara ya utumwa, biashara ambayo iliudhalilisha sana ubinadamu na haki za kibinadamu kwa jumla, kwa kiwango kikubwa.
Katika harakati zake za kukomesha utumwa, wengi wanakumbuka kauli ya Dk. Livingstone katika hotuba yake maarufu aliyoitoa mwaka 1857 akiomba Serikali ya Uingereza kupeleka Wamishionari na wafanyakazi Barani Afrika.  Katika nasaha zake, alielezea imani yake kuwa utumwa utamalizwa kupitia biashara ya bidhaa na mafundisho ya dini.  Hotuba zake hatimae zilichangia kuasisiwa kwa taasisi ya kimishionari ya ujumbe wa vyuo vikuu kwa Afrika ya Kati (UMCA) ambayo ilishirikisha vile vile wanafunzi waliomaliza masomo yao katika Vyuo Vikuu vya Oxford na Cambridge. Historia inaeleza mchango wa taasisi hii katika miaka iliyofuatia, hatimae kufikia kusimamishwa kwa biashara ya utumwa na kufungwa kabisa kwa Soko Kuu la Watumwa la Afrika Mashariki hapa Zanzibar mwaka 1873.
 
Ni matumaini yangu kuwa mtapata muda mzuri kuyajadili masuala haya kwa kina katika kongamano hili tunalolizindua leo.  Nakunasihini washiriki nyote muwe makini katika kuwasilikiliza watoa mada, kuchangia mawazo, kuuliza maswali na hatimae muondoke hapa mkiwa na lengo la kuyatumia maarifa mliyoyapata na uzoefu wa maisha ya Dk. Livingstone katika kuwatumikia wanadamu wenzake ili na sisi tuwe na moyo wa kuwatumikia wenzetu.
 
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Mafundisho ya kidini yana mchango muhimu katika kumuandaa mwanadamu kuelewa ufalme wa Mwenyezi Mungu, kukuza imani na kutambua thamani ya viumbe wengine wakiwemo binadamu wenzako.  Hali hii inasaidia sana kuwafanya watu kuishi kwa kustahamiliana na kuwa raia wema wenye kuzingatia sheria na kuondokana na mambo yote yanayoweza kusababisha uharibifu katika ulimwengu na kumchukiza Mwenyezi Mungu.
 
Napenda niitumie fursa hii ili niwapongeze sana viongozi wetu wa dini wa madhehebu mbali mbali kwa kutekeleza wajibu wao wa kuwaongoza waumini wao katika misingi ya imani inayozingatia kuheshimiana, kuvumiliana, utiifu wa sheria na kuendeleza hali ya amani na utulivu nchini. Tuna wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa na nchi yenye waumini wa dini mbali mbali lakini kwa muda wote tumeendelea kuishi pamoja kwa kusikilizana, jambo ambalo limeendelea kutujengea sifa nzuri na sote tunapaswa kulisimamia na kuliendeleza katika kila hali.
 
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Taasisi za kidini zina mchango muhimu katika malezi ya vijana wetu ili kuwaandaa kwenye maisha yao ya sasa na ya baadae.  Dini zote zinakataza mambo mabaya na kutilia mkazo mambo mema.  Kwa hivyo, tuendelee kutumia fursa za mafundisho ya dini zetu kukemea tabia na mienendo inayopelekea vijana wetu wasijiingize kwenye mambo yanayokwenda kinyume na maamrisho ya dini.  Tuendelee kuwafundisha watoto wetu ili wajiepushe na hatari ya maambukizo ya virusi vya UKIMWI na athari za matumizi ya dawa za kulevya. Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa jitihada kubwa zinafanyika miongoni mwa taasisi zetu za kidini lakini ni vyema tukazidi kuongeza nguvu kwani changamoto hiyo inaendelea kuiathiri nguvu kazi yetu kila uchao.
 
Tuendelee kuelimishana ubaya wa kuwanyanyapaa na kuwatenga wenzetu waliokwisha kupata mitihani hii.  Mafundisho ya dini zetu yanatuelekeza kuwahurumia na kuwasaidia watu wenye matatizo, kwani wewe mwenyewe unaweza kuyapata lini.  Waswahili wanasema “hujafa hujaumbika”.   Hii itakuwa ni njia muhimu ya kuyatafsiri mafunzo yanayotokana na uzoefu tunaojifunza kwa Dk.Livingstone kwa kuwasaidia watu kuondokana na matatizo yanayowakabili.
 
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Tunatambua mchango muhimu wa Kanisa la Anglikana hapa Zanzibar kwa miaka kadhaa tangu karne ya kumi na tisa ambapo mwaka 1864 Askofu George William Tozer alihamishia Makao Mkuu ya Taasisi ya UMCA kutoka Bara kuja Zanzibar na kupatiwa shamba eneo la Kiungani.  Mwaka 1871 Kanisa hili lilipatiwa shamba jengine huko Mbweni ili kuendeleza shughuli zake.  Mbali ya kuwa kituo cha mwanzo kilichoanzishwa Kiungani kilitumika kwa ajili ya kutoa faraja kwa ajili ya watumwa waliokombolewa, historia inaeleza kuwa Skuli iliyokuwepo Kiungani St. Paul ilitoa fursa ya elimu kwa vijana mbali mbali wa Zanzibar pamoja na malezi kwa vijana, mafunzo ya Uskauti na michezo mbali mbali bila ya ubaguzi wowote.  Tunajivunia jitihada za uongozi mahiri na makini wa skuli ya St. Paul Kiungani kwa kuwasaidia watoto wa wanyonge wa Zanzibar kwa kuwapa elimu, kwa ajili ya kujiandaa na maisha yao.  Hadi hivi leo wapo watu wenye ujuzi mbali mbali wanaoitumikia Zanzibar ambao walipata elimu St. Paul Kiungani.  Tuna kila sababu ya kuitunza historia ya St. Paul skuli ya Kiungani. Kuwepo kwa majengo mbali mbali ya taasisi za madhehebu ya kidini kunachangia kuongeza haiba nzuri ya nchi yetu na kuimarisha azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza utalii.  Majengo hayo ni pamoja na mahekalu, misikiti ya kale na majengo ya madhehebu mbali mbali ya Kikristo na dini nyengine hasa katika maeneo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar. Ni vyema waumini na wananchi wote wakaendelea kuyatunza na kuyafanyia matengenezo kila inapohitajika kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mji Mkongwe ili hadhi yake iendelee kudhibitiwa na yadumu kwa muda mrefu zaidi.
 
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa taasisi zetu za kidini zinaunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha huduma za jamii hasa katika kuwapatia wananchi fursa za elimu na huduma za afya.  Idadi ya Skuli binafsi zinazomilikiwa na taasisi za kidini nchini za madhebebu mbali mbali hivi sasa ni zaidi ya 20. Kadhalika, idadi ya vituo vya afya nayo inaongezeka kila uchao. Ni wazi kuwa hatua hii inasaidia sana kuwaondolea wananchi wetu usumbufu wa kupata huduma hizo muhimu katika maeneo ya mbali na kupunguza msongamano katika kupata huduma.
 
Natoa wito kwa taasisi zetu hizi kuendelea na jitihada hizo kwa kadri hali inavyoruhusu hasa katika suala la kuwatunza wazee na watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili sambamba na mipango ya Serikali tuweze kufanikiwa kwa lengo la kuwaandaa raia na waumini wema wenye elimu bora na afya nzuri, mambo ambayo ni ya msingi katika kuendeleza ustawi wa jamii.
 
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Napenda nimalizie nasaha zangu kwa kusisitiza jambo moja.  Umuhimu wa uadilifu na kuwa mfano wa kufuata maadili mema kwa viongozi wakiwemo viongozi wa dini.  Ni dhahiri kuwa mambo haya yana mchango mkubwa kwa wale tunaowaongoza. Imani zao kwetu hutegemea sana vitendo vyetu. Ni vyema siku zote tujitahidi kuwa na maadili mema ili watuamini na kutufanya vigezo vyema na tuwe washauri bora, tutakaowapa ushauri ili waweze kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali za kimaisha zinazowakabili wananchi tunaowaongoza.  Hiyo ni dhamana yetu mbele ya Mwenyezi Mungu.
 
Kwa mara nyengine tena, napenda kulipongeza Kanisa la Anglikana kwa kuendelea kushirikiana na Serikali yetu katika kuhubiri umuhimu wa kuendeleza amani na usalama wa nchi yetu. Kadhalika, natoa shukurani kwa kuendelea kushirikiana nasi katika mipango yetu mbali mbali ya maendeleo na ustawi wa jamii.  Shukurani zangu maalum kwa Askofu Michael Henry Hafidh na uongozi wa taasisi hii ya Marafiki wa Dk. David Livingstone (Friends of Dr. David Livingstone - FDDL) kwa kunialika katika hafla hii ya uzinduzi wa Kongamano la kumuenzi Dk. David Livingstone hapa Zanzibar. Napenda kuwapongeza wale wote tuliowakabidhi vyeti muda mfupi uliopita kwa kutambua mchango wao katika kulifanikisha jambo hili.  Nakutakieni kila la kheri na mafanikio mema katika kuuendeleza utaratibu huu mliouanzisha.
 
Baada ya kusema hayo, sasa napenda kutamka kuwa kongamano la mwaka huu la kumuenzi Dk. David Livingstone limefunguliwa rasmi.
 
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.