Habari za Punde

Hutuba ya Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif katika Hafla ya kukabidhi Mikopo kwa Vikundi 12 vya Ushirika Unguja.

HOTUBA YA MGENI RASMI, MAKAMU WA PILI WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF A. IDDI KATIKA UZINDUZI WA UTOAJI MIKOPO YA MFUKO WA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI, ZANZIBAR
-------------------------------

Mhe. Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto,
Mhe. Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) Kazi na Utumishi wa Umma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchangisha Fedha za Mfuko huu,
Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Uchangishaji Fedha za Mfuko,
Ndugu Viongozi na Watendaji wote mliohudhuria
Wageni waalikwa,
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana,
Assalaam Alaykum.
Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia sote kuwepo hapa leo hii katika shughuli muhimu, tukiwa wazima na afya njema. Pia napenda kuwashukuru nyote mliohudhuria katika hafla hii kwani inaonesha kuwa nanyi mnaguswa na jitihada zinazo chukuliwa na Serikali katika juhudi zake za kupunguza umasikini kwa wananchi wake hususan walioko vijijini.
Kadhalika, sina budi kuwashukuru waandaaji wa hafla hii ambayo imetukutanisha hapa ili kuelewa mipango ya Serikali katika kuwasaidia wananchi kukabiliana na tatizo la mitaji ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kimaendeleo.  Kwa hakika hafla hii imefana sana.
Mikopo tunayoitoa leo inatoka katika Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein aliuzindua rasmi mwishoni mwa mwaka jana katika Hoteli Zanzibar Beach Resort.
Ndugu Wananchi, kama ilivyoelezwa na Mhe. Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Mhe. Zainab Omar Mohamed kuwa Mfuko huu umetokana na Mifuko iliyokuwepo kabla.  Huu ni uthibitisho kuwa jambo hili linaonyesha ni kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikiwasaidia wananchi wake kupambana na umasikini kwa kipindi  sasa.
Kwa mfano, Serikali imeruhusu kuwepo kwa Taasisi za kifedha hapa nchini ili ziwasaidie wananchi kupata mitaji kwa ajili ya shughuli zao mbali mbali za kiuchumi na kimaendeleo wanazozifanya. Hivi sasa zipo Benki kumi (10) hapa Zanzibar, mifuko ya kutoa mikopo saba (7),  na SACCOS kubwa kumi na sita (16).  Kuwepo kwa wingi wa Taasisi hizi za kifedha kunaonyesha kuwa yapo mahitaji makubwa ya huduma za mitaji na fedha hapa Zanzibar kwa ajili ya wananchi wetu.
Hata hivyo, pamoja na kuwepo huku kwa Taasisi nyingi za fedha, imebainika kuwa wananchi wachache sana ndio wanaofaidika.
Ukweli huu ndio ulioipelekea Serikali kuona ipo haja ya kuimarisha Taasisi maalum itakayowalenga vijana waliomaliza skuli, vyuo vya mafunzo ya amali, kinamama, vijana, watu walio katika makundi maalum na wananchi wa kawaida ili kuwapatia mitaji itayowawezesha kufanya shughuli mbali mbali za kiuchumi, na hatimae kujiajiri wenyewe.

Ndugu Wananchi, Serikali imeamua kuimarisha Mfuko huu ili kuweza kutoa mikopo nafuu kwa wananchi wake.  Ziko nchi duniani zikiwemo India, Bangladesh, Bolivia, Indonesia na hata Uingereza zinazoendesha mifuko ya aina hii.  Kwa nchi za Mataifa machanga, nchi zinazoendelea zaidi na suala hili ni Bangladesh na India.
Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi una dhamiri kuu ya kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini, vijana na kinamama ili nao wapate kuinua hali yao ya maisha.  Hata hivyo, ni vyema ikaeleweka kuwa fedha za mfuko huu sio sadaka.  Mwananchi atapatiwa mkopo na baadae arejeshe ili wananchi wengi zaidi wakopeshwe.  Tunataka kukopa iwe harusi na kulipa pia iwe harusi. Siyo kukopa iwe harusi kulipa iwe matanga.  Tuyakumbuke maneno aliyoyasema Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein alipokuwa anauzindua mfuko huu tarehe 21 Disemba, 2013.  Alisema “Tutahakikisha kuwa jitihada za kuanzisha mfuko huu zinakwenda sambamba na juhudi kubwa za kusimamia utoaji wa mikopo yenyewe, udhibiti na urejeshaji wa fedha ili mfuko huu uwe endelevu na wananchi walio wengi waweze kufaidika na jitihada zetu.  Napenda kuihimiza Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto kwa kushirikiana na Taasisi za fedha zijipange vizuri juu ya suala hili”.
Ndugu Wananchi, wito wangu kwa makundi yote haya tuliyoyalenga kuwapatia mikopo, kuchangamkia fursa hii adhim inayotolewa na Serikali yetu na kuitumia mikopo hiyo kwa madhumuni yaliyokusudiwa siyo kuolea, kununua dhahabu au kujengea nyumba, kwa sababu mkopo huu unatakiwa kulipwa.  Unatakiwa kurejeshwa ili na wengine wapate.
Ndugu Wananchi, kama alivyoeleza Mhe. Waziri kwa uwazi kabisa kuwa Wizara yake itahakikisha kuwa huduma hizi za mikopo nafuu zitapatikana katika kila Shehia miongoni mwa Shehia zote za Unguja na Pemba. Hili ni jambo jema sana kwa sababu huduma za fedha zitakuwa zimekurubishwa kwa walengwa hasa, kwa sababu wengi wao wanaohitaji mikopo hiyo wanaishi katika Shehia hizo.  Mabenki mengi yanatoa huduma zao zaidi mijini, tena kwa makundi maalum yenye dhamana za mali zisizohamishika, kama vile nyumba na kadhalika. Hata mifuko mingine ya mikopo inayojaribu kuwafikia wananchi wa mashamba, hufanya hivyo kwa kuwataka wananchi hao wawafuate mjini.
Lakini muundo wa Mfuko huu umetayarishwa katika hali ya wananchi wenyewe kuumiliki na kuwa nao katika maeneo yao, hivyo kuwa ni jambo lenye kuleta mafanikio makubwa katika siku chache zijazo.
Ndugu Wananchi, malengo na shabaha ya Serikali yenu ni kuwa na huduma endelevu za kutoa mikopo vijijini kupitia mfuko huu.  Azma hii haitofikiwa ikiwa wakopeshwaji wataingia mitini baada ya kupata mikopo.
Aidha, azma hii haitofikiwa ikiwa hakuna elimu ya kutosha miongoni mwa wakopaji kuhusu masuala ya fedha (financial literacy).  Natoa wito kwa Chuo chetu cha Fedha, kuanzisha vipindi maalum vya redio na televisheni kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi wetu juu ya namna bora ya kutunza fedha katika maisha yetu. Taaluma kama hizi zitawasaidia wakopeshwaji kutumia mikopo yao kama ilivyokusudiwa.
Ndugu wananchi, kazi yangu hasa niliyopewa leo ilikuwa ni kuzindua utoaji mikopo katika Mfuko huu, ila nimehisi niweke wazi kidogo juu ya mambo yanayohusiana na shughuli za Mifuko ya aina hii.
Baada ya kusema haya sina budi kuwaomba wale wote waliotusaidia kutunisha mfuko huu waendelee kufanya hivyo katika kuwasaidia wananchi wetu katika maeneo mengine ya kimaendeleo, na nisisitize kama alivyosema Mhe. Waziri na Mwenyekiti wa Kamati ya utafutaji fedha za Mfuko huu kuwa Serikali itasimamia ipasavyo kuona matumizi mazuri ya fedha hizi yanafanywa, na walengwa wanafaidika na Mfuko huu.
Mwisho, naomba niwashukuru tena waandaaji wa shughuli hii kwa kunialika kuwa mgeni rasmi.  Lakini pia ninawapongeza wale wote watakaobahatika kupata mikopo hii leo.
Baada ya kusema hayo, naomba sasa nitamke kuwa utoaji wa mikopo ya mfuko wa uwezeshaji wananchi umezinduliwa rasmi, na niko tayari kukabidhi hundi kwa wahusika.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.