Habari za Punde

Utoro wa Wajumbe wa BLW wamkera Makamo wa Pilli wa
Na Himid Choko, BLW

MAKAMO  wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa  Balozi Seif Ali Idd  amekemea vikali tabia mbaya ya utoro iliyojengeka kwa baadhi ya wajummbe wa Baraza la Wawakilishi kutohudhuria vikao vya Baraza hilo.

Mheshimiwa  Makamo wa Pili wa Rais ametoa onyo hilo leo wakati akifunga Mkutano wa 16 wa Baraza la Nane la Wawakilishi ambao pamoja na mambo mengine ulijadili Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa  mwaka wa fedha 2014/2015.

Balozi Seif amesema  si vyema kwa Mheshimiwa Mjumbe wa Baraza La Wawakilishi kukwepa majukumu yake ya Msingi kwa kukimbia vikao vya baraza hilo isipokua kwa sababu za msingi zinazokubalika kwa mujibu wa kanuni za Baraza hilo.

Amesema kitendo cha Mheshimiwa Spika au Mjumbe yeyote anayeongoza Kikao hicho kuakhirisha Vikao vya baraza Mara kwa mara kutokana na  sababu ya mahudhurio yasiyoridhisha ni jambo lisilokubalika kidemokrasia , kiuchumi, na kisiasa .

Amesema  tabia hiyo ya utoro kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  inakidhalilisha chombo hicho kikubwa  mbele ya macho, masikio na midomo  ya wananchi wanaowawakilishi majimboni mwao na taifa kwa ujumla .

Amesema  pia kitendo hicho cha Utoro p kinawanyima haki wananchi kusikia na kuona mambo yao yanazungumzwa na kutafutiwa ufumbuzi unaofaa.

Aidha Makao wa Rais amelishauri Baraza la Wawakilishi kubadilisha mfumo wa utoaji wa posho za vikao vya baraza hilo ili kuweza kuwabana wawakilishi wenye tabia mbaya ya utoro.


Kwa mujibu wa wa Kanuni ya 74(2) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi Toleo la 2012 , Mjumbe yeyote ambaye bila ya Dharura inayokubalika na Spika au Mwenyekiti wa Kamati  atashindwa kushiriki katika Kikao cha Baraza na Kamati zake  hatolipwa posho  kwa ajili ya kikao hicho na endapo posho kwa  ajili ya kikao hicho imelipwa mapema , atakatwa kutoka kwenye stahili zake nyengine zitakazolipwa baadae.

Katika Mkutano huu wa 16 wa Baraza la Nane la Wawakilishi ulioanza tarehe 15  Mei, 2014  , jumla ya maswali  ya msingi 66 na  183 ya nyongeza yaliulizwa na waheshimiwa wajumbe na kujibiwa  na Mawaziri wa Sekta mbali mbali.

Aidha  Mkutano huo ulijadili Hotuba juu ya Mwelekeo wa hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo Zanzibar 2014/2015 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka 2014/2015.

Mambo mengine yaliyojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na Hotuba za Bajeti za  Wizara zote 16 za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  na Miswada miwili ya Sheria  (Mswada  wa Sheria ya Kutoza  Kodi  na Kubadilisha Baadhi ya Sheria  za Fedha  na Kodi  Kuhusiana na Ukusanyaji na Udhibiti wa Mapato ya Serikali  na Mambao Mengine Yanayohusiana na Hayo pamoja na Mswada wa Sheria ya Matumizi  ya Fedha.

Aidha Mkutano huo pia ulipokea Taarifa ya Utekelezaji wa Haki za Mtoto kwa mwaka wa 2014/2015 ambapo  Miswada miwili  ya Sheria  ilisomwa kwa mara ya Kwanza na inatarajiwa kujadiliwa Barazani hapo katika Mkutano ujao.

Miswada hiyo ni pamoja na Mswada wa Sheria ya Maadili ya Viongozi Wa Umma na Kuanzisha Tume ya Maadili ya Viongozi na Mambo Yanayohusiana na Hayo, na Mswada wa Sheria ya Kufuta  Sheria ya Wauguzi na Wakunga Namba 9 ya Mwaka 1986 na Kuanzisha badala yake Sheria Mpya ya Wauguzi na Wakunga na Mambo yanayohusiana na Hayo.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi kimeakhirishwa hadi  Siku ya Jumatano ya tarehe 22 Oktoba , 2014 saa 3:00 asubuhi .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.