HOTUBA
YA MAONI YA KAMATI YA MAENDELEO YA WANAWAKE NA USTAWI WA JAMII KUHUSIANA NA
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA HAKI NA USTAWI WA WATOTO KWA MWAKA 2013/2014 NA
MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA YANAYOFANYIKA KILA MWAKA IFIKAPO TAREHE
16 JUNI.
Kila sifa njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu
aliyetujaalia afya na uzima na kutuwezesha wajumbe wa Baraza lako Tukufu
kuendelea kutekeleza majukumu tuliokabidhiwa; kwa niaba ya wananchi
tunaowawakilisha kupitia nafasi mbali mbali katika Baraza lako tukufu.
Mheshimiwa
Spika,
Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako, kwa
kunipa nafasi hii ya kuwasilisha maoni
ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii, kuhusiana na Taarifa ya
Utekelezaji wa Haki na Ustawi wa Watoto kwa mwaka 2013/2014 iliyowasilishwa na
Mhe. Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa jamii, Vijana, Wanawake na Watoto.
Mheshimiwa
Spika,
Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa
Jamii, inaunga mkono taarifa iliyowasilishwa na Mhe. Waziri, ambayo ilikusanya
mambo muhimu yanayoelekeza katika kuendeleza ustawi na upatikanaji wa haki za
watoto. Pia inayoonesha namna gani nchi
yetu inavyochukua jitihada kupitia Wizara zake mbali mbali katika kuyafanyia
kazi mapendekezo na maazimio yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika
n.k ili kuhakikisha kuwa, utekelezaji wa mipango ya Wizara hizo inazingatia
maazimio hayo kwa lengo la kuleta ustawi na upatikanaji wa haki za watoto
katika nchi yetu.
Mheshimiwa
Spika,
Licha ya Kamati yangu kuunga mkono taarifa
iliyowasilishwa na Mhe.Waziri lakini Kamati imegundua kuwa, katika taarifa hiyo
kumekosekana uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji kwa mwaka uliopita wa
2012/2013 ambapo imekuwa ni vigumu kwa wajumbe wa Baraza lako tukufu, wasikilizaji
au wasomaji wengine wa taarifa hiyo kuweza kufahamu na kulingalisha hatua
zilizofikiwa za utekelezaji wa haki na ustawi kwa mwaka uliotangulia na
muelekeo wa mwaka ujao. Hivyo Kamati inaishauri Wizara, pindi itakapokuwa inawasilisha
taarifa ya utekelezaji katika Baraza lako tukufu, ni vyema ikazingatia kuingiza
taarifa ya utekelezaji wa mwaka uliotangulia ili iwe rahisi kwa wajumbe wa
Baraza, wasikilizaji na wasomaji wengine kuweza kulingalisha hatua zilizofikiwa
za utekelezaji wa haki na ustawi wa watoto.
Mheshimiwa
Spika,
Baada ya Utangulizi huo napenda kuchukua fursa
hii kwa kuwatambua wajumbe wa Kamati pamoja na makatibu wake kama hivi
ifuatavyo:-
- Mhe. Mgeni Hassan Juma Mwenyekiti
- Mhe. Hassan Hamad Omar M/Mwenyekiti
- Mhe. Ali Salum Haji Mjumbe
- Mhe. Abdi Mosi Kombo Mjumbe
- Mhe. Farida Amour Mohamed Mjumbe
- Mhe. Mwanaid Kassim Mussa Mjumbe
- Mhe. Mohamed Mbwana Hamad Mjumbe
- Ndg. Maryam Rashid Ali Katibu
- Ndg. Asha Said Mohamed Katibu
Mheshimiwa
Spika,
Siku ya Mtoto wa Afrika ni siku muhimu ambayo
inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 16 Juni na katika siku hii
jamii inapata fursa ya kufahamu hatua zilizofikiwa na Wizara katika kutekeleza
haki za watoto na hatua zilizopendekezwa kuchukuliwa kwa nia ya kuimarisha
huduma zinazolenga watoto pamoja na kuimarisha mashirikiano baina ya wazazi,
walezi, sekta zinazohudumia mama na mtoto pamoja na washirika wa maendeleo.
Mheshimiwa
Spika,
Maoni
ya Kamati yangu yatagusa maeneo mbali mbali yanayohusiana na Wizara hii ikiwa
ni pamoja na baadhi ya maeneo ya taarifa iliyowasilishwa na Mhe. Waziri na
Kamati itatoa ushauri kwa Serikali, Wizara na Jamii kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika
KINGA DHIDI YA VITENDO VYA
UDHALILISHAJI WA WATOTO.
Itakumbukwa
kuwa, katika kikao cha Disemba cha 2013, Mhe Mwenyekiti wa Kamati hii, Mgeni
Hassana Juma aliwasilisha hoja binafsi inayohusiana na kutoa Maazimio Dhidi ya Vitendo vya
Udhalilishaji wa Watoto na Wanawake Zanzibar ambapo hoja hiyo ilitolewa kwa
mujibu wa Kanuni ya 27(1)(n), 27(3), 49(1) na Kanuni ya 50
ya Kanuni za Kudumu za Baraza la Wawakilishi toleo la 2012).
Mheshimiwa Spika,
Katika
hoja hiyo kulikuwa kuna mambo ya msingi ambayo yalihitaji kushughulikiwa kwa
haraka na miongoni mwa mambo hayo ni kuitaka Serikali kuanzisha mkakati wa
Kitaifa wa Kupambana na kutokomeza udhalilishaji wa watoto utakaojumuisha wawakilishi
kutoka makundi mbali mbali na pia Serikali iweke kipaumbele katika bajeti zake kuanzia
bajeti ya mwaka 2014/15 na bajeti zinazofuata juu ya kupambana na kutokomeza
udhalilishaji wa watoto. Hivyo Kamati inaitaka Serikali kutoa tamko juu ya
hatua iliyofikiwa katika hoja hiyo kwani Serikali haijaleta tamko lolote katika
Baraza lako tukufu tokea kupitishwa kwa hoja hiyo.
Mheshimiwa
Spika,
MALALAMIKO
YA VITENDO VYA UDHALILISHAJI WA WATOTO NA NAMNA KESI ZINAVYOSHUGHULIKIWA.
Kamati imekuwa ikishuhudia jitihada mbali mbali
zinazochukuliwa na Wizara hii, katika kupinga vitendo vya udhalilishaji wa
watoto kwa kuanzishwa kwa Vituo vya Mkono kwa Mkono Unguja na Pemba,
Kamati za Shehia za Kupinga vitendo vya udhalilishaji n.k. Kamati inaipongeza
Wizara na inaziunga mkono jitihada hizo lakini kwa upande mwengine Kamati yangu
imekuwa inasikitishwa sana na uchache wa kesi zinazohukumiwa.
Mheshimiwa
Spika,
Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014,
jumla ya malalamiko 2,337 (Unguja 2,239
na Pemba 98) yameripotiwa katika vituo vya Mkono kwa Mkono lakini katika
malalamiko hayo, 87 tu ndio yaliyowasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Kamati
imebaini kuwa idadi hiyo ni ndogo sana ukilinganisha na malalamiko yaliyopo
huku waathirika wakubwa katika vitendo hivyo wakiwa ni watoto wenye ulemavu
hasa hasa wenye ulemavu wa akili. Hivyo Kamati inaiomba Serikali kuangalia kuna
matatizo gani yanayopelekea kukwamisha kesi hata ikawa kuna kesi chache tu
ambazo zinasilishwa mahakamani na baadae kuchukua hatua za haraka ili kuondoa
mrundikano wa kesi za watoto mahakamani. Kufanya hivyo kutapelekea watoto
kupatiwa haki yao ya msingi ya kuishi na kuhifadhiwa kutokana na vitendo vya
udhalilishaji.
Mheshimiwa
Spika,
KUHUSU
MISAADA NA USTAWI WA WATOTO
Kamati inaipongeza Wizara kupitia Idara ya
Ustawi wa Jamii kufanya zoezi la
utambuzi kwa watoto wanaoishi
katika mazingira magumu zaidi katika Wilaya 5 za Unguja (Mjini, Kati, Kusini, Kaskazini A
na Kaskazini B) na Wilaya 3 za Pemba (Mkoani, Chake Chake na Micheweni) na
kubaini kuwa, kuna watoto wapatao 698 (332 wanawake na 366 wanaume) wanaoishi
katika mazingira magumu zaidi.
Mheshimiwa
Spika,
Kamati yetu inatambua kuwa watoto wanaoishi
katika mazingira magumu zaidi wanahitaji kusaidiwa lakini ukweli ni kuwa Wizara
haijatengewa bajeti maalum na ya kutosha
kwa ajili ya kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi.
Hivyo Kamati inatoa wito kwa Serikali kutenga bajeti maalum kwa watoto
wanaoishi katika mazingira magumu zaidi, kuzingatia masuala ya watoto katika
mipango na bajeti na pia kuitaka jamii kuchukua jukumu la kuwahudumia watoto
wao na kusaidia familia ambazo zinaishi katika mazingira magumu kwa wale wenye
uwezo wa kufanya hivyo.
KUHUSU MAENDELEO YA ELIMU KWA WATOTO ZANZIBAR.
Mheshimiwa
Spika,
Kamati yangu imekuwa ikishuhudia juhudi za
Serikali katika kuwapatia elimu wa watoto wetu, kupitia Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali imekuwa ikijitahidi kuboresha elimu ya Maandalizi na kuifanya
kuwa ni elimu ya lazima ili kuwapatia watoto wetu msingi bora kabla ya kujiunga
na elimu ya Msingi, aidha ni imani ya Kamati yangu kuwa ile program ya ECD
(Early childhood development) itaanza kufanya kazi kwa mashirikiano ya wizara
tatu zinazohusika ambazo ni pamoja na Wizara ya Elimu, Wizara ya kilimo na
Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto ambapo katika
program hii itajumuisha elimu ya makuzi ya awali ya mtoto ambayo itajumuisha
masuala ya lishe bora katika kumjenga mtoto katika ukuaji wake kiakili na
kimaadili ambao utasaidia ufahamu wa mtoto katika maendeleo yake ya elimu.
Mheshimiwa
Spika,
Aidha Katika kuboresha maendeleo ya elimu kwa
watoto katika nchi yetu Serikali kupitia Wizara ya elimu katika bajeti ya mwaka
2014/2015 imeazimia kuanzisha mradi wa kuwapatia chakula wanafunzi wa Skuli za
maandalizi, Kamati inaunga mkono azma hii ya Serikali na inachukua fursa hii
kuwashajihisha wananchi kuzallisha kwa wingi mazao ambayo yatatumika katika
kuwapatia chakula watoto katika maeneo yao mazao hayo ni pamoja na mahindi
mtama, viazi vitamu nk ili kuunga mkono juhudi za Serikali yetu.
KUHUSU
USHIRIKISHWAJI WA WATOTO KATIKA MASUALA MBALI MBALI.
Mhe.
Spika,
Miongoni mwa haki muhimu ya mtoto ni
kushirikishwa katika mambo mbali mbali yakiwemo ya kijamii, kisiasa na
kiuchumi, Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana,Wanawake na Watoto kwa
muda mrefu sasa imekuwa ikiendelea kuanzisha na kuyaendeleza mabaraza ya watoto katika ngazi za Shehia na
Wilaya. Hivi sasa kuna mabaraza ya watoto ya Wilaya matatu (3), mawili (2)
Unguja na moja (1) Pemba na mabaraza ya Shehia 218 (Unguja 139 na Pemba 79) ambapo kupitia mabaraza hayo watoto hupata
fursa ya kubadilishana mawazo na kushiriki katika shughuli mbali mbali za
kijamii. Aidha kupitia mabaraza hayo mafunzo mbali mbali yamekuwa yakitolewa
kwa watoto juu ya kufahamu haki zao na jinsi ya kujithamini na kujilinda.
Mheshimiwa
Spika,
Mwisho nachukua tena nafasi hii kukushukuru kwa
kunipa nafasi hii kuwasilisha maoni ya Kamati juu ya Hotuba ya siku ya mtoto
duniani 2014, aidha napenda kumshukuru Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii,
Vijana, Wanawake na Watoto pamoja na watendaji wake wote kwa mashirikano yao
makubwa wanayotupatia.
Mhe.
Spika,
Baada ya kuyasema hayo kwa naiba ya Kamati
yangu naomba kuwasilisha.
Ahsante,
………………………….
Mgeni
Hassan Juma,
Mwenyekiti,
Kamati
ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii,
Baraza
la Wawakilishi,
No comments:
Post a Comment