HOTUBA YA
MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR,
MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI KATIKA UFUNGAJI WA
MKUTANO WA 16 WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR
TAREHE 28 JUNI, 2014
.
1.0 Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia neema ya uhai na uzima na kutuwezesha kukutana tena katika mkutano huu wa 16 wa Baraza la Wawakilishi. Pia, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia nchi yetu kuendelea kuwa na amani, utulivu na salama ambayo hazina yetu kubwa inayohitaji kuenziwa na kila mmoja wetu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuzidishie umoja na mshikamano ili tuweze kuitunza amani hii na kudumisha utulivu tulio nao nchini mwetu daima milele. Amin.
2.0 Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa napenda kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti pamoja na Wasaidizi wako wote kwa namna mnavyoendelea kuliongoza Baraza hili Tukufu kwa umahiri na umakini mkubwa. Bila shaka uongozi wenu huo umesaidia sana kuyafikia malengo ya mkutano wetu huu wa 16 kwa mafanikio makubwa.
3.0 Mheshimiwa Spika, pia nawashukuru sana Waheshimiwa Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa maelekezo yao yaliyojaa busara kwa Wizara na Ofisi zetu ambayo yamechangia sana katika kuongeza kasi na umakini wakati wa kupanga na kutekeleza majukumu yetu. Aidha, shukurani nyingi sana ziwaendee Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili Tukufu kwa michango yao yenye upeo mkubwa katika kuijenga nchi yetu na kuiletea maendeleo katika nyanja zote.
4.0 Mheshimiwa Spika, kwa nafasi ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wake uliojaa hekima na busara ambao umekuwa ni chachu ya uwajibikaji kwetu katika kufikia hatua kubwa za kimaendeleo zinazoonekana hivi sasa katika nchi yetu. Vile vile, nampogeza sana Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa kuendelea kumshauri vyema Mheshimiwa Rais katika kuiongoza nchi yetu hii. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awazidishie nguvu na uwezo wa kuendelea kuitumikia nchi hii kwa hekima na busara zaidi.
5.0 Mheshimiwa Spika, natoa shukurani maalum kwa Waheshimiwa
Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji
wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa bidii kubwa wanayoionesha katika
kuwatumikia wananchi wa Zanzibar. Kwa hakika wananchi wamejenga imani na
matumaini makubwa kwa viongozi wao hawa kutokana na hatua kubwa za kimaendeleo
tunazoendelea kuzipata.
B. KUDUMISHA
AMANI, UTULIVU NA MSHIKAMANO:
6.0 Mheshimiwa Spika, ili nchi yoyote iweze kufanikiwa kupata
maendeleo endelevu, ni lazima kuwepo na amani na utulivu. Hivyo, suala la
kudumisha amani, utulivu na mshikamano hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla
lina umuhimu mkubwa sana katika ustawi wa nchi na wananchi wetu. Tumeshuhudia
mifano mingi duniani kwa nchi ambazo zimekosa amani na utulivu namna nchi hizo
zilivyovurugika kwa maelfu ya watu kupoteza maisha yao, maelfu kuwa wakimbizi,
kuwepo kwa udhalilishaji mkubwa wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto, na
uharibifu wa miundombinu ya nchi na mali za wananchi.
7.0 Mheshimiwa Spika, ukichunguza kwa makini utagundua kwamba
uvunjifu huo wa amani unasababishwa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi ya
kujilimbikizia mali, uroho wa madaraka na kupalilia tofauti za kidini,
ukabila na umajimbo.
8.0 Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio makubwa tuliyopata katika kuenzi umoja na amani, hivi sasa ndani ya nchi yetu zimejitokeza kila dalili kwa baadhi ya watu wachache kufanya vitendo vinavyoashiria uchochezi na uvunjifu wa amani jambo ambalo halikubaliki hata kidogo. Ni vyema kwa wenzetu hawa wakaelewa kwamba ni rahisi sana kuvunja amani lakini ni gharama kubwa sana kuirudisha amani pindi ikitoweka. Hivyo, natoa indhari kuwa, sote tunapaswa kuwa makini na kauli na vitendo vyetu hasa sisi viongozi wa kisiasa, kijamii na kidini ili kauli na vitendo hivyo visiwe chanzo cha uvunjifu wa amani na utulivu hapa nchini.
9.0 Mheshimiwa Spika, napenda kuwakumbusha viongozi wenzangu kwamba sisi ni wachunga na tutaulizwa juu ya tunavyovichunga. Hivyo basi, tusijisahau tunapokuwa na wafuasi wetu katika mazingira tofauti kuwakumbushia jukumu la kuilinda na kuidumisha amani tuliyonayo. Nawaomba sana tusitoe nafasi kwa wale wachache miongoni mwetu wanaochochea mifarakano kwani kufanya hivyo wataivuruga nchi yetu na kudumaza maendeleo yetu. Hatutavitendea haki vizazi vyetu kama tutaiacha nchi hii kuwa katika hali ya vurugu na uvunjifu wa amani.
10.0 Mheshimiwa Spika, Serikali inasikitishwa sana na kitendo cha kihalifu kilichotokea hivi karibuni cha mlipuko wa bomu katika eneo la Darajani Mjini Unguja na kusababisha kifo cha mtu mmoja na watu wengine saba (7) kujeruhiwa, wote wakiwa hawana hatia, Serikali inatoa mkono wa pole kwa familia ya mtu aliepoteza maisha katika mlipuko huo na tunamuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahala pema peponi – Amin. Aidha, tunawaombea wale wote waliojeruhiwa katika tukio hilo wapone kwa haraka ili warudi katika shughuli zao za kawaida.
11.0 Mheshimiwa Spika, tukio hili ni la kushtusha na la kusikitisha lililotokea nchini kwetu ambapo bomu la kivita limetumika kufanyia vitendo vya kihalifu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalaani kwa nguvu zake sote kitendo hiki cha kihaini na inaendelea kulifanyia uchunguzi tukio hili na kuwasaka wale wote waliohusika ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao. Aidha, Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama imejipanga vizuri kudhibiti vitendo kama hivi visitokee tena katika nchi yetu. Natoa wito kwa wananchi kutoa mashirikiano makubwa kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa ili kuwafichua wahalifu hawa wasioitakia mema nchi yetu.
12.0 Mheshimiwa Spika, napenda kuwathibitishia wananchi kwamba nchi yetu bado ipo katika hali ya salama, amani na utulivu, hivyo waendelee kufanya shughuli zao bila hofu. Vile vile, kwa wageni wetu pamoja na watalii waliopanga kuja kutembelea nchi yetu waendelee kuja bila hofu. Nchi yetu ni salama.
13.0 Mheshimiwa Spika, napenda kuwatanabahisha viongozi wenzangu na wananchi kwa ujumla kwamba hivi sasa tupo katika kipindi cha muendelezo wa mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kipindi cha matayarisho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015. Hivyo, tunapaswa kuwa makini na kuchukua tahadhari zote kwa kauli na vitendo vyetu kwa wakati wote ili kauli na vitendo vyetu hivyo visiwe chanzo cha kuleta chuki na uhasama miongoni mwetu.
Inatupasa tuelewe kwamba mambo yote katika nchi yetu yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni tulizozitunga sisi wenyewe. Hivyo, hatuna budi kuzifuata Sheria na Kanuni hizo. Tukifanya hivyo nchi yetu itabaki kuwa na umoja, upendo na mshikamano, na hatimaye kupata maendeleo tuliyo yakusudia. Nawasihi sana Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuendelea kuwa wamoja na mshikamano ili tukienda kwenye Bunge Maalum mwezi Agosti, twende na sauti moja itakayotuwezesha kupata Katiba mpya ambayo
itakuwa na manufaa na maslahi kwa Zanzibar. Katiba mpya ndiyo
itakayoondoa kero nyingi tunazo zilalamikia kila siku.
C. MATUKIO MUHIMU:
Mripuko wa Maradhi ya Homa ya Dengue:
14.0 Mheshimiwa Spika, nchi yetu hasa Jiji la Dar-es-Salam
limekumbwa na mripuko wa maradhi ya homa ya Dengue. Kutokana na mripuko
huo Zanzibar nayo imekumbwa na wasiwasi wa kujitokeza watu walioambukizwa
maradhi haya. Kwa mujibu wa maelezo ya kitaalamu, maradhi haya yanasambazwa na
mbu anaeuma wakati wa asubuhi hadi jioni. Mbu hawa wanazaliana katika maji safi
yaliyotuwama.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ni kwamba kwa upande wa Zanzibar watu …… walionekana kuwa na dalili za ugonjwa huo, lakini baada ya uchunguzi wa kimaabara hawakuthibitika kuwa waliathiriwa na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ni kwamba kwa upande wa Zanzibar watu …… walionekana kuwa na dalili za ugonjwa huo, lakini baada ya uchunguzi wa kimaabara hawakuthibitika kuwa waliathiriwa na ugonjwa huo.
15.0 Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa wananchi wote kufuata masharti ya afya na kutunza mazingira yetu ili kuhakikisha mbu huyu anakosa maeneo ya kuzalia na anatoweka katika maeneo yetu. Aidha, tuchukue tahadhari na kumuwahisha mgonjwa anayeonyesha dalili za ugonjwa huu katika vituo vya afya ili kunusuru maisha yake na kudhibiti kuenea kwa maradhi haya.
Migogoro katika Jamii:
16.0 Mheshimiwa Spika, kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii na nchi yetu kuwa na rasilimali ndogo ya ardhi, kumejitokeza migogoro inayohusiana na umiliki wa ardhi kwa shughuli za kilimo, biashara na uwekezaji. Serikali itachukua kila juhudi kuhakikisha migogoro hii inamalizika na kuondoka kabisa. Tunahitaji mashirikiano na Masheha, Madiwani, Viongozi wa Serikali pamoja na Wanasiasa na wananchi kwa jumla wakati Serikali inaendelea na ukamilishaji wa Mpango wake wa Matumizi Bora ya Ardhi utakaosaidia kupunguza migogoro iliyojitokeza. Zimeonekana dalili kuwa baadhi ya migogoro hii kukolezwa na baadhi yetu Wanasiasa kwa sababu binafsi za kisiasa. Naamini kwamba kama sote tutashirikiana kwa dhati kwa nia ya kuiondoa migogoro hii tutafanikiwa kwa kiwango kikubwa. Inawezekana kama sote tutatimizi wajibu wetu.
17.0 Mheshimiwa Spika,
Kumekuwepo na migogoro ya ardhi baina ya wawekezaji na wananchi kwa baadhi ya
maeneo. Serikali imejitahidi sana kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza
nchini mwetu. Nia ya kufanya hivyo kwanza ni kuongeza mapato ya Serikali,
lakini pili kuongeza ajira kwa vijana wetu. Ni ukweli usiopingika kuwa
sekta hii binafsi ndiyo inayotoa ajira nyingi. Hivyo, ningewasihi
wananchi waache kuwabeza wawekezaji hawa ambao tumewaita wenyewe ili waje
kushirikiana nasi katika kukuza uchumi wetu na kuongeza ajira kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Spika, jambo la kusikitisha ni kuwa baadhi ya wawekezaji wetu, hasa wa mahoteli, huajiri watu kutoka nje ya nchi yetu na kuwaacha watu wetu ambao wana taaluma sawa na hao kutoka nje. Ningependa kuwasihi wawekezaji hao kuacha mara moja tabia hiyo kwani hawawatendei haki wenyeji. Naziomba Taasisi husika, kama vile Kamisheni ya Kazi, Kamisheni ya Utalii na Uhamiaji kuliangalia suala hili kwa umakini mkubwa. Kazi ambayo inaweza kufanywa na Mzanzibari kusiwe na haja ya kuajiriwa mtu kutoka nje ya nchi.
Matayarisho ya Uchaguzi
Mkuu wa 2015:
18.0 Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar tayari imeanza
rasmi maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Kazi hiyo imeanza kwa kufanya
uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya Majimbo ya Uchaguzi Zanzibar kama
inavyoelekezwa na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984. Aidha, Tume inaendelea
kupokea maoni ya wadau wa uchaguzi juu ya kazi ya uchunguzi wa idadi, majina na
mipaka ya Majimbo ya Uchaguzi kutoka kwa wadau mbali mbali wakiwemo Vyama vya
Siasa, Asasi za Kijamii, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Taasisi za Serikali,
Wawakilishi, Wabunge na Madiwani pamoja na Wananchi wote katika Wilaya husika.
Hivyo, tunawaomba wananchi kujitokeza kwa wingi wakati wa utoaji wa maoni hayo
tukiwa katika hali ya amani na utulivu.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeendesha kazi za uandikishaji
wa wapiga kura wapya na uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura. Kazi
hiyo ilianza katika mwezi wa Juni 2013 Mkoa wa Kaskazini Unguja na ilimalizika
katika mwezi wa Novemba 2013, Mkoa wa Kusini Pemba. Zoezi hilo lilifanyika kwa
kuwaandikisha wananchi wote waliojitokeza ambao wana sifa za kupiga kura kwa
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, Aidha, Tume ilitoa nafasi kwa wananchi kufanya uhakiki
wa Daftari la wapiga kura katika vituo vilivyotumika kuandikisha wapiga kura
hao ili kuona usahihi wa taarifa zao na uhalali wa wapiga kura hao. Pia,
Tume ilitoa fursa ya kuweka pingamizi juu ya wale waliopoteza sifa za kuwemo
katika daftari ili Daftari liwe na wapiga kura wenye sifa za kupiga kura. Vile
vile, Tume ya Uchaguzi itaendesha zoezi jengine la uandikishaji wa wapiga kura
kwa wananchi ambao walikosa nafasi ya kujiandikisha katika awamu zilizopita.
Lengo ni kuhakikisha kila anaestahiki kupiga kura anapata haki yake hiyo
ya kidemokrasia.
Udhalilishaji wa kijinsia:
19.0 Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni, vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto vimeshamiri sana katika
visiwa vyetu vya Unguja na Pemba. Tafiti zinaonesha kwamba watoto wa jinsi zote
hawako salama na udhalilishaji huu. Wafanyaji wa vitendo hivi ni watu wa karibu
wa watoto hao ambao wanategemewa kuwa ni walezi na walinzi wao. Hebu tujiulize
tunatengeneza jamii ya namna gani na watoto wetu tunawaandalia hatma gani? Bila
ya shaka, jitihada zaidi za pamoja bado zinahitajika katika kupambana na tatizo
hili ili kukiepusha kizazi chetu kuangamia kutokana na janga hili.
20.0 Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande wake imekuwa ikichukuwa
jitihada kadhaa katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwa
ni pamoja na kufanya tafiti zinazohusiana na matokeo ya udhalilishaji wa
kijinsia ili kujua kiwango chake, kuzifanyia kazi sheria, sera pamoja na
kutekeleza program mbali mbali ili kupunguza kasi ya vitendo hivi nchini.
Aidha, Serikali imesimamia uanzishaji wa mifumo ya kupambana na vitendo
hivi kuanzia ngazi ya Shehia hadi Taifa pamoja na kuweka miongozo ya namna ya
kuyashughulikia na kutoa huduma kwa waathirika wa vitendo hivyo.
21.0 Mheshimiwa Spika, kupitia Baraza lako hili Tukufu
naomba kuendelea kutoa wito kwa jamii kutovifumbia macho vitendo hivi kwa
kuvipatia utatuzi na usuluhishi katika ngazi ya familia au jamii bali wavitolee
taarifa katika vyombo husika ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu
wa sheria. Aidha, naomba wananchi wasipuuze suala la kwenda mahkamani kutoa
ushahidi kwani ndio njia pekee itakayopelekea wahalifu hawa kutiwa hatiani na
hatimae kuvitokomeza vitendo hivi vya kinyama katika jamii yetu. Vile vile,
Serikali inawataka kuacha mara moja wale wote wanaojishughulisha na vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia kwani Serikali haitamuonea huruma mtu yeyote
atakaepatikana na hatia.
D. VIPAUMBELE VYA SERIKALI:
22.0 Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa
wananchi wake, kwa mwaka ujao wa fedha 2014/2015, Serikali itaendelea
kuvifanyia kazi vipaumbele ilivyojiwekea katika sekta za kiuchumi na kijamii
kama vilivyoainishwa katika Hotuba ya Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
2014/2015, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi na kijamii;
kuimarisha huduma za kijamii kama vile elimu, afya bora na upatikanaji wa maji
safi na salama; kuimarisha huduma kwa makundi maalum hasa wazee wasiojiweza,
watoto na watu wenye ulemavu; kuimarisha mazingira ya biashara kwa kuondosha
vikwazo visivyo vya lazima na kupunguza urasimu; kuiendeleza sekta binafsi hasa
katika uzalishaji na utoaji wa huduma muhimu kupitia ushirikiano baina ya
Serikali na Sekta binafsi (PPP); kuharakisha upatikanaji wa ajira bora hasa kwa
vijana na kuimarisha utafiti ili kuwezesha mipango bora.
23.0 Mheshimiwa Spika, vipaumbele hivi vimewasilishwa kupitia
Bajeti Kuu ya Serikali na Bajeti za Sekta husika na kujadiliwa kwa kina katika
kikao hiki. Napenda kutoa wito kwa watendaji wote wa taasisi za umma kujituma,
kuwa makini na kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa ili kuhakikisha vipaumbele hivi
vinatekelezwa ili tupige hatua zaidi za maendeleo.
24.0 Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande wake itajitahidi kuona
kwamba nyenzo, hasa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele hivi
zinapatikana na kwa wakati. Hivyo, Serikali itaimarisha ukusanyaji wa mapato
kutoka katika vyanzo vyake mbali mbali. Ili kufikia azma hii, hatuna budi
kushirikiana katika ukusanyaji na usimamizi wa kodi. Nachukua nafasi hii
kuwasisitiza wafanya biashara na wananchi kwa ujumla kuwa na utamaduni wa
kulipa kodi na ada katika huduma zote za kiuchumi na kijamii ili kuiongozea
mapato Serikali kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. Sambamba na hili,
Serikali itachukua hatua madhubuti za kudhibiti uvujaji wa mapato katika
taasisi na maeneo yote. Katika kulifanyia kazi suala hili, ni vyema kwa
viongozi na watendaji wa Serikali kufuata maadili ya kazi na kujiepusha na
vitendo vya rushwa.
25.0 Mheshimiwa Spika, sina haja ya kuelezea kwa urefu
kuhusu malengo na mipango mbali mbali ya Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Wizara na Taasisi zake kutokana na maelezo yanayohusiana na malengo
pamoja na mipango kutolewa vya kutosha na Waheshimiwa Mawaziri wakati
wakiwasilisha hotuba za Wizara zao za Makadirio na Matumizi kwa mwaka
2014/2015. Napenda tu kuwasisitiza Waheshimiwa Mawaziri kuyasimamia
malengo na mipango hiyo kuhakikisha kuwa inatekelezwa. Ningependa pia
kuwasihi Mawaziri na Watendaji wao kusimamia vyema matumizi ya fedha walizo
idhinishiwa na Baraza hili tukufu.
E. MAMBO YALIYOJITOKEZA
BARAZANI:
26.0 Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa 16 wa Baraza la Nane
la Wawakilishi, jumla ya maswali ya msingi 66 na maswali 183 ya nyongeza
yaliulizwa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kujibiwa na
Waheshimiwa Mawaziri wa sekta husika. Maswali yote ya Msingi na nyongeza
yalikuwa na lengo la kuboresha utendaji wa Serikali katika kuwahudumia wananchi
wake. Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe waliouliza na
Waheshimiwa Mawaziri kwa majibu ya kutosheleza waliyoyatoa.
27.0 Mheshimiwa Spika, kuanzia tarehe 15 Mei, 2014 hadi leo,
tumesema sana. Waheshimiwa Mawaziri wamesema na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza
lako tukufu nao wamesema. Mawaziri wamesema wakati waliposomo hotuba zao
za bajeti, Wenyeviti wa Kamati mbali mbali nao wamesema wakati wa kusoma maoni
ya Kamati zao kuhusiana na hotuba ya bajeti ya Wizara husika. Lakini pia
Wajumbe wa Baraza lako tukufu nao pia wamesema kwa kutoa michango yao mbali
mbali kuhusiana na hotuba hizo za bajeti zilizowasilishwa. Hivyo, sote
tumesema sana. Lakini ni Mawaziri ambao wamesema zaidi wakati wa
majumuisho na wakati wa kupitisha vifungu walipotakiwa kutoa ufafanuzi na
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili tukufu. Kwa kweli kila mmoja wetu
ndani ya Baraza hili alisema sana.
28.0 Mheshimiwa Spika, Hotuba juu ya Mwelekeo wa Hali ya Uchumi na
Mpango wa Maendeleo Zanzibar 2014/2015 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Serikali kwa Mwaka 2014/2015 ziliwasilishwa. Aidha, jumla ya Wizara 16 za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ziliwasilisha Hotuba zake za Makadirio ya
Mapato na Matumizi kwa mwaka 2014/2015 na Waheshimiwa wajumbe wa Baraza lako
Tukufu walipata nafasi ya kuzichangia hotuba hizo.
29.0 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mwelekeo wa Hali ya Uchumi na
Mpango wa Maendeleo Zanzibar 2014/2015 pamoja na Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2014/2015, Waheshimiwa Wajumbe wameishauri
Serikali kuteua miradi michache inayotekelezeka. Aidha, Wajumbe
waliishauri Serikali kuendelea kutafuta vianzio vyengine vya mapato ili
kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli zake. Pia, Waheshimiwa Wajumbe
waliishauri Serikali kuongeza udhibiti wa mapato na usimamizi wa matumizi ya
fedha za Serikali.
30.0 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kuchangia Hotuba za Mawizara,
pamoja na mambo mengine Wajumbe waliishauri Serikali kusimamia mambo muhimu
ikiwemo kuzipatia Wizara vifaa na vitendea kazi, kusimamia uwajibikaji na
utunzaji wa mali za Serikali na kufanya mapitio ya sheria na kuandaa sheria
mpya ili kuleta ufanisi. Vile vile, Serikali imeelekezwa kutoa fursa sawa za
ajira kwa makundi yote, kuimarisha maslahi ya wafanyakazi na kuimarisha huduma
za kijamii kwa ujumla ikiwemo afya, elimu, maji, nishati ya umeme na
miundombinu.
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa wajumbe kuwa ushauri, michango
na mapendekezo yao yamepokelewa na yatafanyiwa kazi ipasavyo.
31.0 Mheshimiwa Spika, Miswada miwili (2) iliwasilishwa na
kujadiliwa katika mkutano huu. Mswada wa kwanza ni Mswada wa Sheria ya Kutoza
Kodi na Kubadilisha Baadhi ya Sheria za Fedha na Kodi Kuhusiana na Ukusanyaji
na Udhibiti wa Mapato ya Serikali na Mambo Mengineyo Yanayohusiana na Hayo.
Madhumuni ya Mswada huu ni kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa
matumizi ya Serikali. Katika kuchangia Mswada huu Waheshimiwa Wajumbe
waliishauri Serikali kusimamia utekelezaji wa Sheria hii na kuweka utaratibu
mzuri wa kuyarejesha mapato kwa wakusanyaji kwa mujibu wa Sheria zilizopo.
32.0 Mheshimiwa Spika, Mswada wa pili uliowasilishwa ni Mswada wa
Sheria ya Matumizi ya Fedha. Mswada huu ulikuwa na lengo la kuthibitisha
matumizi ya fedha za Serikali yatakayofanywa kwa mwaka 2014/2015.
33.0 Mheshimiwa Spika, Baraza lako tukufu pia lilipokea Taarifa ya
Utekelezaji wa Haki za Mtoto kwa mwaka 2013/2014. Ripoti hiyo ilikuwa na lengo
la kupima utekelezaji wa kisekta wa haki za mtoto kama zilivyoainishwa katika
Sheria ya Watoto Namba 6 ya Mwaka 2011 pamoja na Mikataba ya Kikanda na
Kimataifa inayohusu uhai, hifadhi, ustawi na maendeleo ya Mtoto. Taarifa hii
inakwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambapo kwa mwaka
huu ilikuwa na kauli mbiu isemayo ‘’Elimu Bora Isiyo na Vikwazo ni Haki ya Kila
Mtoto’’. Tunatoa wito kwa jamii kuitekeleza kauli mbiu hii kwa vitendo kwa
manufaa ya nchi yetu.
F. MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI:
34.0 Mheshimiwa Spika, siku chache zijazo tutaingia ndani ya mwezi
Mtukufu wa Ramadhani ambapo Waislamu kote duniani watatekeleza Ibada ya funga.
Inasisitizwa katika mwezi huu kusameheana, kuhurumiana na kusaidiana ili
kulifikia lengo la mwezi huu kama ilivyoelezwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu katika
Qur-an Tukufu Sura ya 2 aya ya 183 inayosema:
“Enyi mlioamini mmefaradhishiwa juu yenu kufunga kama walivyofaradhishiwa
waliopita kabla yenu ili mpate kuwa wachamungu”.
35.0 Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kuwa Ramadhani ni mwezi wa
Rehma, Maghfira na Toba. Waislamu wote tuutumie mwezi huu vizuri ili kuweza
kupata fadhila zilizomo ndani yake kwa kuzingatia maadili ya mwezi huu ikiwemo
kujisitiri vizuri na kujiepusha na tabia ya kula hadharani.
36.0 Mheshimiwa Spika, katika mwezi huu ni vizuri kwa wafanya
biashara kuzingatia uuzaji wa bidhaa zao. Kwani kuna tabia kwa baadhi ya
wafanya biashara kuufanya mwezi huu kuwa ni wa kupata faida kubwa kwa
kupandisha bei za bidhaa na vyakula hasa vinavyotumika katika mwezi huu. Hivyo,
Serikali inatoa wito kwa wafanya biashara wote kupunguza bei za bidhaa na
vyakula na kuwa waangalifu na waadilifu katika matumizi ya vipimo ili kila
Muislamu aweze kupata mahitaji muhimu ya mwezi huu kwa bei nafuu.
37.0 Mheshimiwa Spika, tunamuomba Mwenyezi Mungu atukubalie funga
na ibada zetu zote za mwezi Mtukufu na miezi mengine na atuwezeshe kumaliza kwa
salama na kusherehekea vizuri Sikukuu ya Iddi el Fitri. Hivyo, tunawaomba
wananchi kufanya ibada zao kwa amani na utulivu pamoja na kujiepusha na mambo
yote yatakayopelekea kubatilisha funga zetu pamoja na kuvunja sheria za nchi.
35.0 Mheshimiwa Spika, ni vyema kwa wananchi wote
kufuata maagizo ya dini zetu hasa katika suala la kuhubiri umoja, amani na
mshikamano. Hivyo basi, tuutumie mwezi huu wa Ramadhani kama darasa kwa
kuhurumiana, kupendana na kusaidiana na tusiziache tofauti zetu za kidini,
rangi na ukabila zikatawala na kutuharibia nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu hii, napenda
nielezee masikitiko yangu kutokana na mahudhurio yetu hapa
Barazani.
Miongoni mwa kazi za msingi za mjumbe wa Baraza la Wawakilishi ni
kuhudhuria vikao vyote vya Baraza bila kukosa, isipokuwa kwa sababu za msingi
zinazokubalika kwa mujibu wa kanuni zetu. Kitendo cha kulazimika kwa Mhe. Spika
jana asubuhi kuahirisha Baraza kutokana na sababu ya mahudhurio yasiyoridhisha,
ni jambo lisilokubalika kidemokrasia, kiuchumi na kisiasa na baya zaidi tabia
hii ya utoro inalidhalilisha Baraza letu tukufu mbele ya macho ya wananchi wetu
waliotuchagua. Sisi Wajumbe wa Baraza ni macho, masikio na midomo ya wananchi
tunaowawakilisha Majimboni mwetu. Kitendo cha kutokuhudhuria vikao vya Baraza
maana yake tunawanyima wananchi wetu kusikia na kuona mambo yao yakizungumzwa
na kutafutiwa ufumbuzi unaofaa. Kiuchumi, utoro huu unaopelekea kuahirishwa kwa
vikao vyetu vya Baraza unapoteza fedha nyingi za wananchi wetu. Hatuoni kama ni
unafiki tunapopiga kelele kuwa Serikali inapoteza fedha za wananchi wakati sisi
wenyewe pia tunachangia
upotevu huo?
Wengi wetu hapa ni wazazi na walezi. Mtoto anapotoroka darasani, mzazi
pamoja na mwalimu wake wanaweza kumpa adhabu ya viboko. Adhabu hizi
tunazitoa kwa sababu tunaelewa upo uhusiano wa karibu kati ya utoro na matokeo
ya masomo darasani. Mtoto mtoro huvuna matokeo mabaya darasani. Hakuna tofauti
athari ya utoro wetu barazani na ule wa darasani. Utoro wetu barazani
utasababisha matokeo mabaya ya utendaji wa kazi zetu ndani ya Baraza, kazi ya
kufanywa siku moja inaweza ikalala hadi siku ya pili. Huu sio ufanisi, huu ni
ule usemi wa Mheshimiwa Rais ‘Business as usual’. Kama watoto wetu tunawachapa
viboko kwa utoro, kuna haja nasi kujiwekea adhabu kwa makosa yetu haya ya
kutokuhudhuria vikao. Adhabu tunayoweza kujiwekea ni kubadilisha mfumo wa
utoaji wa posho za vikao.
G. HITIMISHO:
36.0 Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kwa mara
nyengine tena kuwakumbusha wananchi juu ya suala la kudumisha Amani, Utulivu na
Mshikamano katika nchi yetu ili tuweze kujiletea maendeleo zaidi ya kiuchumi,
kijamii, kisiasa na kiutamaduni kwa kutekeleza shughuli zetu za uzalishaji mali
bila ya bughudha.
37.0 Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena, napenda kuchukua
nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa hekima na busara zako unazozitumia
katika kuliongoza Baraza hili. Aidha, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe
wa Baraza lako Tukufu, kwa uvumilivu waliouonyesha kwa muda wote wa mkutano.
Nakushukuruni sana na ninawatakia safari njema ya kurejea Majimboni kwenu
kwa ajili ya kuwatumikia wananchi. Pia nawapongeza Watendaji wote wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada zao katika kutimiza wajibu wao
na kuleta maendeleo ya nchi.
38.0 Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuvishukuru kwa
dhati vyombo vya habari vyote hapa Zanzibar, hasa Shirika la Habari la Zanzibar
(ZBC) kupitia redio na TV ambavyo vilirusha moja kwa moja mtiririko mzima wa shughuli
za Baraza na kuwawezesha wananchi wetu kufuatilia kwa makini matukio yote
yaliyojiri Barazani. Pia nawapongeza wakalimani wetu wa lugha ya alama
kwa kazi nzuri walioifanya ya kutafsiri mawasilisho na mijadala katika kipindi
chote cha Baraza na kuwawezesha wananchi wenzetu wenye matatizo ya kusikia
kufuatilia shughuli za Baraza.
39.0 Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa
hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano, tarehe 22
Oktoba, 2014 saa 3.00 asubuhi, Inshaallah.
40.0 Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment