Na Asya Hassan
MTOTO Milembe Matias Shija (6) mkaazi wa Mwera bonde la mpunga wilaya ya magharibi
Unguja, amepata michubuko katika sehemu mbali mbali za mwili wake baada ya
kupigwa na mama yake wa kambo.
Tukio hilo limetokea juzi asubuhi nyumbani kwao Mwera.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mtoto huyo alisema mama yake alimpiga marungu
katika maeneo tofauti ya mwili wake bila kosa baada ya kumfunga kamba ya kifua.
“Nimeamaka asubuhi baada ya baba kuondoka mama alinipiga na kwa rungu na
kunifunga kamba ya kifua bila kujua kosa langu,” alisema.
Mtoto huyo alisema mama yake huwa na kawaida ya kumpiga na kumnyima chakula
wakati baba yake hayupo na kumwambia
akirudi baba yake asimwambie na kama atamwambia atampiga tena.
Nae baba mzazi wa mtoto huyo, Matias Shija, alisema juzi aliporudi usiku
hakumkuta mtu nyumbani na kukaa hadi saa mbili usiku hajawaona na kuamua kwenda
kuuliza kwa jirani.
Alisema baada ya kumuona mtoto wake alifahamishwa kilichotokea na kumchukua
na kurudi nae nyumbani.
Alisema baada ya kurudi mkewe ambae aliondoka kuwakimbia askari alimuliza
kuhusu tukio hilo lakini alikataa na
kumwambia mtoto huyo kapigwa na wenzake nje.
Aidha alisema mkewe huyo ana kawaida ya kumpiga mtoto wake,kwani iko siku alimkuta
mwanawe kajichinja vidole vya mkono wa kulia na alipomuliza alimwambia kajikata
alipokuwa akimenya chungwa.
“Juzi baada ya kutokea tukio hili nimesikia hii tabia imezoeleka,mimi
nikiondoka yeye anampiga na vile vidole alivojikata alimkata yeye,” aisema.
Kwa upande wa jirani, Zuwena Juma, ambae alimshughulikia mtoto huyo baada
ya kupigwa kwa kumpeleka polisi na hospitali, alisema tukio hilo halileti
taswira nzuri katika jamii.
Nae Daktari aliemshughulikia,Salum Omar Mbarouk, alisema mtoto huyo amepata
majeraha ya kuchunika sehemu ya uso,viganja vya vidole vya mkono wa kulia
ambayo vinaonesha kukatwa na kitu chenye ncha.
Nae Sajenti wa polisi kutoka dawati la jinsia na watoto Mwera,Haji Mohammed
Iddi, alisema taarifa hiyo waliipokea juzi na kumuandikia PF3 na baadae
kumpeleka hospitali kwa matibabu.Kwa upande wake, Mratibu wa GEWE, Asha Abdi,
alisema matukio kama hayo hutokea kila wakati na upande wao wamekuwa wakitoa
juu ya kupunguza udhalilishaji.
No comments:
Post a Comment