Na Hassan Hamad,OMKR
WATOTO milioni 153 wanaishi bila ya
uangalizi wa wazazi duniani kote, huku Tanzania ikiwa na watoto wa aina
hiyo wapatao 11,216.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akifungua mkutano wa
kimataifa wa siku tano kwa nchi wanachama wa vijiji vya SOS, unaofanyika hoteli
ya Zanzibar Beach Resort.
Pamoja na mambo mengine mkutano huo
unajadili namna ya kukuza uelewa katika uendelezaji wa vijiji vya watoto vya
SOS, pamoja na kutathmini mafanikio na changamoto zinazovikabili vijiji hivyo.
Alisema idadi ya watoto wanaokosa
uangalizi wa wazazi imekuwa ikiongezeka kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo
kufariki kwa wazazi, hali ya umaskini, unyanyasaji na talaka.
Alisema matokeo ya hali hiyo ni
kuongezeka kwa ajira za watoto ambapo Zanzibar pekee inakisiwa
kuwa na asilimia 9.2 ya watoto kati ya umri wa miaka mitano hadi 17
wanaojihusisha na ajira hizo.
Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo,
juhudi za pamoja zinahitajika kati ya taasisi za umma na binafsi, kuhakikisha
haki za watoto zinalindwa, sambamba na kuzisaidia familia zenye watoto yatima
na zinazoishi katika mazingira magumu.
Alisema serikali kwa upande wake
inaridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na SOS Zanzibar na Tanzania, na kuzitaka
taasisi hizo kuzidisha bidii katika kuleta ufanisi.
Alielezea matumaini yake kuwa kampeni ya
CARE FOR ME iliyozinduliwa na vijiji vya
SOS mwaka 2012, italeta faraja na mafanikio kwa kuwapatia watoto huduma bora
zikiwemo za elimu.
Aliyashukuru mashirika ya misaada ya
Norway (NORAD), Austria (ADA) na Denmark kwa kuunga mkono miradi ya SOS, hatua
ambayo alisema inaisaidia serikali kukabiliana na matatizo yanayowakabili
watoto.
Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti
wa bodi ya vijiji vya SOS Zanzibar, Mohammed Bhaloo, alisema SOS Zanzibar inawahudumia
watoto 800 kwa kuwapatia elimu bora, kupitia
skuli ya msingi na sekondari ya Hermann Gmeiner iliyo chini ya kijiji
hicho.
Alisema SOS Zanzibar pia ina kituo cha afya ambacho hutoa
huduma kwa watoto wa kijiji hicho pamoja na wananchi wa maeneo ya karibu ambapo
zaidi ya wagonjwa 1,400 hupatiwa matibabu katika kituo hicho kwa mwaka.
Aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine
SOS Zanzibar kupitia mpango wake wa kuwajengea uwezo watoto, inazisaidia
familia 180 zenye watoto 1000 Unguja na Pemba, ili ziweze kuimarisha huduma kwa
watoto hao.
Akizungumzia kuhusu historia ya vijiji
vya SOS Zanzibar, Bhaloo alisema azma ya kuanzishwa kwa vijiji hivyo iliasisiwa
mwaka 1984 na kuanza kuwahudumia watoto kuanzia mwaka 1991.
Aliishukuru serikali na taasisi binafsi
kwa ushirikiano wao katika kuunga mkono juhudi za vijiji vya SOS, na kwamba
mafanikio makubwa yamepatikana tokea kuanzishwa kwa vijiji hivyo.
Mkutano huo wa siku tano unazishirikisha
nchi mbali mbali zenye vijiji vya SOS zikiwemo Austria, Cameroon, Ethiopia,
Malawi, Msumbiji,Morocco, Uganda, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Tanzania na
wenyeji Zanzibar.
No comments:
Post a Comment