Na Mwandishi wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema rasimu
ya sera ya diaspora iko kwenye hatua za mwisho na muda si mrefu itaingizwa
kwenye utaratibu wa kiserikali ili hatimaye iweze kuwasilishwa kwenye Baraza la
Mawaziri.
Akizungumza na Watanzania wanaoishi
Uingereza kwenye mkutano uliofanyika ubalozi wa Tanzania jijini London,
mwishoni mwa wiki, Pinda, alisema mchakato wa kuandaa rasimu hiyo ulihusisha
wadau wengi kwa kadri ilivyowezekana ili kupata wigo mpana wa suala zima la
diaspora.
“Katika hatua za awali, mbali ya ofisi
yangu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, tuliwashirikisha
kwa karibu Umoja wa Wanadiaspora waliorudi Tanzania (Tanzania Diaspora
Initiative) na wanadiaspora kutoka Uingereza, Marekani, China, Oman, India na
Afrika Kusini ili kupata uzoefu wao kutokea huko waliko,” alisema.
“Baadaye tukawapelekea wataalamu ambao ni
Profesa Samuel Wangwe wa REPOA, Profesa Joseph Semboja wa Uongozi Institute na
Profesa Faustine Kamuzora wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kila mmoja kwa wakati wake
na kuwaambia waichanechane kadri wawezavyo na kisha watupe mrejesho wao,” alisema.
Aliwataja wadau wengine muhimu
waliohusishwa kwenye kuichambua rasimu hiyo kuwa ni Shirika la Kimataifa
linaloshughulika na Wahamiaji (IOM) ambao wamebobea katika masuala ya wahamiaji
katika nchi mbalimbali duniani.
“Kwa mtazamo wangu hii rasimu imekaa
vizuri kwa sababu tumejitahidi kugusa kila eneo ambalo kwenu lilikuwa na
umuhimu wa kipekee. Sasa hivi imeshawekwa vizuri kimfumo na inasubiri iingie
katika utaratibu wa kiserikali,” alisema.
Wakati
huo huo Pinda alisema serikali inaandaa kongamano la siku mbili litakalojadili
mustakabali wa wana diaspora wa Tanzania
kutoka nchi zote duniani ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha na makampuni na
wafanyabishara mbali mbali.
Alisema kongamano hilo ambalo limepangwa
kufanyika Agosti 14-15, mwaka huu, linalenga kuitambulisha rasmi diaspora ama
jamii ya Watanzania inayoishi ughaibuni kama wadau muhimu katika kuleta
maendeleo nchini Tanzania .
"Lengo letu hasa ni kutaka jamii ya Watanzania ielewe kwamba tunao
Watanzania walioko nje ya nchi kwa maelfu na kuna sehemu mnaweza kuchangia
katika maendeleo ya nchi," alisema.
Alisema katika kuitambua rasmi jamii ya
wanadiaspora, serikali itapenda kujua wapo wangapi na wanafanya nini ambacho
kama Sserikali itahitaji ujuzi auutaalamu wao, inaweza kuwapata.
Alisema kongamano hilo limeandaliwa kwa
ushirikiano baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Umoja wa Wanadiaspora waliorudi nchini
waitwao (TDI).
Akifafanua zaidi kuhusu taswira nzima ya
Diaspora, alisema: "Sensa ya mwaka 2012 inaonesha katika kaya zote
zilizohesabiwa Tanzania
Bara kuna mtu mmoja au zaidi ambaye yuko nje ya nchi. Hii ni sawa na asilimia
1.2. Kwa upande wa Zanzibar, hali iko tofauti sana . Wao ni mara mbili zaidi yaani kila kaya
moja ina watu wawili na zaidi ambao wako nje ya nchi."
Alisema katika matokeo ya sensa,
ilibainika kwamba wanadiaspora wanaotoka kwenye kaya za mikoa ya Tanzania Bara wako 116,670 wakati wanaotoka Zanzibar wanafikia
304,786.
“Idadi ya Watanzania walioko Diaspora ni
421,456 ni karibu sawa na nusu milioni. Idadi hii si ndogo, ni kubwa. Na kama
kundi hili lingetumika vizuri, fedha
waliyonayo ambayo wanaituma kutoka nje, ingesaidia kuendeleza taifa
letu,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwaelezea kuhusu
mchakato wa katiba ulivyoenda na ulipofikia, maandalizi ya uchaguzi wa serikali
za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu.
“Kama serikali
tunajiandaa kwa lolote litakaloamuliwa na Bunge Maalum la Katiba. Kikubwa
tunachoomba ni kuwa na mchakato wa amani hadi uchaguzi mkuu ufike,” aliongeza.
Aliwataka wanadiaspora waendelee kuiombea
nchi ili ipate wagombea wenye kujali maendeleo ya watu kuliko kitu kingine
chochote.
Endeleeni kuiombea nchi yetu ili tupate watu
waadilifu, watu ambao wanajali watu wa hali ya chini na wenye kutaka maendeleo
ya nchi kwanza kuliko vitu vingine.
“Endeleeni kuiombea nchi yetu amani,
tuendelee kumuombea Rais Kikwete ili amalize kipindi chake vizuri na akabidhi
kijiti kwa mwingine salama,” alisema.
No comments:
Post a Comment