Habari za Punde

Zakaatul Fitr - Umeshatekeleza wajibu wako?

Abu Ammaar

Zakatul Fitri , ambayo pia hujulikana kama Sadaqatul Fitri , kilugha inatokana na neno la kiarabu fitri na  maana yake ni kula  au futari kama inavyojulikana.

Katika sheria ni ile sadaqa inayotolewa mwishoni  mwa mwezi wa Ramadhan na kabla ya kusaliwa Eid na kupewa wanaostahiki.

KUFARADHISHWA KWAKE

Zakatul Fitri ni wajibu kwa kila muislam awe mwanamke au mwanamme ,mkubwa au mdogo ,almuradi ana uwezo wa kuitoa au kutolewa kwa niaba yake ikiwa yuko anaemuangalia.

Dalili ya kufaradhishwa kwake ni  Hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kutokana na  ‘Abdullah Ibn  ‘Umar, Allah awawie radhi(yeye na baba yake), kwamba  Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema :

 Amefaradhisha Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam Zakatul Fitri katika Ramadhaan kwa kila mtu miongoni mwa waislamu huru na mtumwa, mwanamke na mwanamme, mdogo na mkubwa kutoa  pishi moja ya tende au pishi moja ya uwele, Na akaamrisha kutolewa kabla ya watu kutoka kwenda kusali (Eid)

                                                           Imepokewa na Bukhari

Kwa mujibu wa hadithi hii, Zakatul Fitri itabidi itolewe kwa waislamu wa aina zote bila ya kujali hali, jinsi na mazingira ya muislamu husika pindi uwezo ukiruhusu na huyu muislamu kuushuhudia mwezi mtukufu wa Ramadhan.Uwezo unaokusudiwa ni kwa muislamu kuweza kuwa na vya kujitolesheza katika siku ya eid na bado kuwa na cha ziada.

Kwa hivyo kama muislamu ni mwenye jukumu la kuwahudumia wengine kwa mahitaji yao ya lazima basi ni wajibu kwa mtu huyo pia kuwatolea wale wote ambao wako chini ya jukumu lake katika kuwahudumia. Hii ni kutokana na  ufafanuzi uliotolewa na Sahaba Abu  Saeed Al Khudhriy ,Allah amuwie radhi, pale aliposema -:                                                                          

“Tulikuwa tukitoa enzi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam  pishi  moja ya nafaka au pishi moja ya tende au pishi moja ya uwele au pishi moja ya zabibu.”                                     

                                         Imepokewa na  Bukhari na Muslim

Kwa mfano  kama mtu ana mke na watoto watatu,na pia mtoto wa dada yake ambaye anamlea na kumshughulikia na mama yake mzazi; 

Ni wajibu kwa mtu huyo kutoa Zakah kwa nafsi yake mwenyewe kwanza na kisha hawa watu watano ambao wako chini ya dhamana yake.

LENGO LAKE

Lengo la Zakatul Fitri  

1       Ile haja ya kuondoa tabaka lililokuwepo kati ya  matajiri na maskini  kwani kila mtu hupaswa  kujitolea yeye mwenyewe na pia wale wote wanaomtegemea  na sadaqa hiyo kwenda kwa maskini na mafakiri.

2     Inajenga mahusiano ya karibu kati ya aliyekuwa nacho na yule ambae hana kitu hasa kwa ile siku ya furaha ambayo waislam wote hutakiwa kufurahi, na pia kuwafunza wale wenye nacho  kuwaangalia sana wale ambao hawana.

3  Inatoa nafasi kwa wale ambao wamefunga na katika funga zao walifanya baadhi ya makosa madogo madogo ambayo yanaweza  kuathiri kukubalika kwa funga zao kuisafisha.

Imepokewa kutoka kwa Sahaba ‘Abdullah Ibn ‘Abbass, Allah amuwie radhi, kwamba:-  

“Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amefaradhisha Zakatul Fitr  kwa wale waliofunga ili iwatoharishe na yale  mambo  ya kipumbavu na maneno machafu (waliokuwa  wakifanya na  kuongea wakati wa kufunga) na pia kwa wale maskini wapate kulishwa. Yoyote mwenye kuitoa kabla ya sala  basi hiyo ni   Zakah iliokubalika , na mwenye kuitoa baada  ya sala  itahesabika kama ni sadaqa miongoni mwa sadaqa”

    Imepokewa na Abu Daaud, Ibnu Majah na Ad daaru Qutniy

4      Kuendeleza malezi ya kiroho  miongoni mwa waumini  hasa kwa kuiangalia mali katika mtazamo wa kutoa sadaqa, msaada na  kuwa wakarimu  ikiwa ni moja katika njia  ya kumshukuru Allah Subhaanahu Wata’aala  kwa neema hii.

 

HUKUMU YAKE 

Ni wajibu kwa kila muislamu.

Wajibu huu ni wa muda maalum  tu  na mtu kwa bahati mbaya akikosa kutoa katika muda wake  uliopangwa  atakuwa ametenda kosa ambalo atapaswa kurudi kwa mola wake kutubu na kuomba maghfira.

Na mwenye kuacha kuitoa kwa makusudi ilhali ya kuwa na uwezo afahamu kwamba hili ni kosa na dhambi kubwa inayohitaji kurudi kwa mola na kutubu kwani kutotekeleza wajibu ni kuasi amri ya Allah Subhaanahu Wata’aala na Mtume wake Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Na wajibu wowote katika sheria ukiachwa basi ni jukumu la asietekeleza kulilipa kama vile muislamu akiikosa sala ya fardhi au funga ya Ramadhaan.  Hivyo wajibu wa kuitoa utabaki pale pale licha ya kutekeleza toba ila utoaji wa Zakah hii baada ya muda utakuwa katika hali ya sadaqa na si Zakah tena.

MUDA WA KUTOLEWA

Muda wake  ni tokea kutua kwa jua katika siku  ya mwisho  wa mfungo wa mwezi wa Ramadhan mpaka wakati watu wanapotoka kwenda kusali sala  ya Eid.

Hata hivyo Maulamaa wamekubaliana kwamba Zakah hii inaweza kutangulizwa kabla ya muda wake kama walivyokuwa wakifanya masahaba. Na hata kwa yule ambaye kwa njia moja au nyengine hakubahatika kutoa Zakah katika muda wake bado anapaswa kutoa sadaqa kama alivyobainisha Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kupitia kwa Ibnu ‘Abbaas Allah awawie radhi (yeye na baba yake) kwamba:                                                                                                        

“Mwenye kuitoa kabla ya Sala basi hiyo ni Zakah iliyokubalika na mwenye kuitoa baada ya sala basi hiyo ni sadaqa miongoni mwa sadaqa.”

                                              Imepokewa na Abu Daaud

WANAOSTAHIKI KUPEWA

 Ni waislamu  maskini na mafakiri wasiojiweza ili na wao wapate kufurahi katika siku hii.(Hii ni rai nilioiwafiki kwani pia kuna rai kwamba wapewe wale watu wanane wanaostahiki kupewa Zakah ya mali). Pia hupaswa kutolewa kwa wasiojiweza waliopo katika nchi/mji wa anaetoa. Kwa mfano mtu yupo hapa Uingereza Zakatul fitri itolewe kwa waislamu wasiojiweza wa hapa hapa. Ila tu Maulamaa wamejuzisha kupelekwa nchi nyengine ikiwa shida na mahitaji yao huko ni kubwa na nzito.

WASIOSTAHIKI KUPEWA

Kila muislamu ambae mtoaji ana wajibu wa kumhudumia na kumuangalia. Kama mzazi, mke, mtoto na kadhalika.

Pia haijuzu Zakah hii kutumika katika kujenga misikiti au madrasah au kutumika katika miradi yoyote ya kimaendeleo hata kama ni ya kiislamu.

Ama ikiwa kuna jamaa wa karibu na ambae hana jukumu la kumhudumia; huyo anaweza kupewa Zakatul fitr ikiwa ni miongoni mwa masikini na mafakiri wasiojiweza. Na ni awlaa (vizuri) zaidi kama Zakah hii atapewa jamaa wa karibu.

KINACHOTOLEWA

Asli yake hutolewa chakula kile ambacho ni maarufu katika mji/nchi kwa mujibu wa hadithi tulizozibainisha hapo juu . Enzi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kulitolewa tende na uwele(aina ya mtama). Hivi vilikuwa vyakula maarufu. Na wakati huo pesa zilikuwepo.

 

Ama kutolewa pesa badala yake ni suala ambalo Maulamaa wametofautiana na kauli ya Jamhuur Ulamaa ni kwamba haipaswi kutolewa pesa. Sheikhul Islam Ibnu Taymiyah amejuzisha kutolewa pesa kwa sharti kwamba kutakuwa na maslaha makubwa zaidi kwa anaepewa kuliko akipewa chakula au nafaka.

Zinaweza kutolewa pesa kwa mfano hapa Uingereza kisha hao watakaokabidhiwa ni kwenda kununua vyakula na kuwapa wanaostahiki nafaka.

Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’aala atuwafikishe katika kuitoa Zakah hii katika wakati wake inshaallah. Na azitoharishe funga zetu kutokana Zakah zetu. Na pia tuitoe kwa ikhlaasi huku tukitaraji malipo kutoka kwake Subhaanah.

Allah ndie ajuae zaidi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.