Makamu wa kwanza wa Rais. Maalim Seif Sharif Hamad akiwasalimia maafisa wa Polisi Makao Makuu ya Polisi Zanzibar
Makamu wa kwanza wa Rais. Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Polisi Ziwani alipofika kuwatembelea.
Na Khamis Haji, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ametoa wito kwa Jeshi la Polisi Zanzibar kutekeleza
majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya kazi na kuhakikisha askari hawafanyi
kazi kwa misingi ya upendeleo, chuki, rushwa, wala ubaguzi wa aina yoyote.
Maalim Seif ameyasema hayo leo wakati
alipotembelea Makao Makuu wa Polisi Zanzibar Ziwani, na kuzungumza na Kamishna
wa Polisi Zanzibar, Hamdan Makame pamoja na maafisa wa Jeshi hilo.
Makamu wa Kwanza amesema kwa kiasi
kikubwa Polisi Zanzibar limepata mafanikio makubwa katika kusimamia majukumu yake,
hasa ya kupunguza matendo ya uhalifu, lakini wapo miongoni mwa askari hujihusisha
na matendo yaliyo kinyume cha maadili yanayolitia doa jeshi hilo.
Alisema zipo taarifa kwamba baadhi ya
Maafisa wa polisi huvujisha taarifa na kuwapa watuhumiwa wa dawa za kulevya, pale
jeshi hilo linapojiandaa kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria.
Maalim Seif amesema tabia hiyo haina
budi kukomeshwa kwa nguvu zote kwa sababu hudhorotesha mikakati ya kukomesha
uingizwaji na biashara ya dawa za kulevya katika visiwa vya Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema dawa za
kulevya zinasababisha madhara makubwa kwa wananchi hasa vijana, na Polisi
wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti uingizwaji wake kwa
kushirikiana na taasisi za Kitaifa na Kimataifa.
“Nasikia baadhi ya wakati taarifa huvujishwa
na maafisa wa Polisi. Kitengo cha Polizi cha Dawa za Kulevya lazima kiwe na
watu waaminifu sana, Kamishna hili ni tatizo kubwa lazima tulikomeshe”, alisema
Maalim Seif.
Amelipongeza Jeshi hilo kwa juhudi kubwa
linazozichukua kuwakamata watuhumiwa wa dawa za kulevya na kuwafikisha mbele ya
sheria, lakini hata hivyo amesema bado juhudi zaidi zinahitajika kuwamata
wafanyabiashara wakubwa ambao mara nyingi hawapatikanwi.
Amesema Jeshi hilo litajipatia sifa
kubwa zaidi na kuipatia sifa nchi, iwapo litafanya kazi kwa kuzingatia weledi,
ukakamavu na uwezo wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha
utawala bora unazingatiwa kikamilifu.
Ameeleza kuwa Polisi wanatakiwa
kujiepusha na tabia ya kufanya kazi kwa upendeleo na wahakikishe wanawapatia
haki sawa watu wote, iwe kwa viongozi, watoto wa viongozi au wananchi wa
kawaida.
“Sisi wanasiasa tuna kawaida jamaa zetu
wanapofanya makosa na kukamatwa tunampigia simu Kamishna, msikubali kufanya
upendeleo na kuwakandamiza wananchi wanyonge, hakuna mtu aliye juu ya sheria”,
alionya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji
ya Polisi, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamadan Makame amesema miongoni mwa
changamoto zinazolikabili jeshi hilo ni ukosefu wa vifaa vya kutendea kazi,
uhaba wa nyumba za kisasa kwa ajili ya askari, kuibukwa kwa uhalifu mpya wa
kwenye mitandao.
Changamoto nyengine amezitaja kuwa kuibuka
vikundi vya kidini vilivyosajiliwa na baadhi ya maeneo ya ardhi yanayomilikiwa
na Jeshi la Polisi kuvamiwa na viongozi na baadhi ya wananchi.
Aidha, Kamishna huyo amesema ipo haja
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilione Jeshi la Polisi ni lake, licha ya kuwa
lipo chini ya Serikali ya Muungano, kwa kurejesha utaratibu wa zamani wa kulisaidia
kufanikisha baadhi ya majukumu yake, ikiwemo operesheni maalum zinazotekelezwa hapa
Zanzibar.
Hata hivyo, Kamishna Makame alitaja
miongoni mwa mafanikio makubwa ya Polisi Zanzibar hivi sasa ni kupungua kwa
matukio ya uhalifu mkubwa, kupungua ajali na makosa ya barabarani, wananchi
kuongeza imani kwa Jeshi hilo, na kufanikisha vizuri suala la kudumishwa amani katika
visiwa vya Unguja na Pemba.
No comments:
Post a Comment