Habari za Punde

DK.Shein Akutana na Marais wa Seychelles na Comoro na kuhimiza Ushirikiano.

Na Said Ameir -Samoa. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa nyakati tofauti leo amekutana na Marais wa Seychelles Mheshimiwa James Michel na Rais wa Comoro Mheshimiwa Ikililou Dhoinine ambapo walizungumzia masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo.

Mazungumzo na marais hao yalifanyika sambamba na Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa unaoendelea mjini Apia katika visiwa vya Samoa ambapo marais hao wanahudhuria.

Katika mazungumzo yake na Rais wa Seychelles, Dk. Shein alimhakikishia Rais Michel kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunga mkono Mpango wa Magharibi ya Bahari ya Hindi wa Changamoto za Ukanda wa Pwani na Mabadiliko ya Tabiachi (Western Indian Ocean Coastal Challenges-WIO-CC) ambao unatarajiwa kuzinduliwa kesho (Jumatano) mjini Apia, Samoa.

Viongozi hao walikubaliana kuwa mpango huo ni muhimu kwa kuwa unatoa fursa ya kuziweka nchi hizo karibu katika kushughulikia changamoto zinazozikabili ambazo wakati mwingine hazipewi nafasi zinazostahili katika majukwaa ya kimataifa. Mpango huo unashirikisha visiwa vya Comoro, Madagascar, Reunion, Seychelles na Zanzibar.   

Dk. Shein na Rais Michel walieleza dhamira za Serikali na wananchi wa nchi zao za kuimarisha ushirikiano kwa kuangalia maeneo mengi zaidi ambayo nchi hizo zinaweza kushirikiana na kuwa na manufaa kwa nchi zote.

Kwa hivyo walikubaliana kushirikiana katika kukuza utalii hasa katika safari za meli za kitalii na kwamba Dk. Shein ameafiki dhana ya mpya ya kukuza utalii katika visiwa vya bahari ya hindi ijulikanayo kama visiwa vya Vanilla (Vanilla Islands).

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein na Rais Michel walieleza haja ya Tanzania na Seychelles kushirikiana vile vile katika hifadhi ya mazingira ya bahari na maliasili zake.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Seychells kwa kuwaalika viongozi wa Zanzibar kutembelea nchini mwake.

Alifafanua kuwa kufuatia mialiko hiyo Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa nyakati tofauti waliweza kutembelea visiwa hivyo na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yenye manufaa kwa Tanzania na Seychelles.


Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumwalika Rais wa Sechelles kutembelea Zanzibar ambapo Mheshimiwa James Michel alieleza kuwa ziara za mara kwa mara kati ya viongozi wa nchi zinakuza na kuimarisha uhusiano.    

Akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Comoro, Dk. Shein alimueleza Rais huyo kuwa amefurahi kuona maandalizi ya mpango wa ushirikiano kati ya Zanzibar na Comoro yanaendelea vyema ambapo maeneo ya ushirikiano yameainishwa na yanafanyiwa kazi.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni afya, elimu na utamaduni,miundombinu  pamoja na kilimo ambapo Zanzibar na Comoro zinaweza kushirikiana katika utafiti wa mazao ya kilimo .

Dk. Shein alimhakikishia Rais wa Jamhuri Comoro Mheshimiwa Ikililou Dhoinine kuwa Zanzibar iko tayari kuisaidia nchi yake kukuza lugha ya Kiswahili kwa kuwapatia fursa za masomo ya shahada za uzamili na uzamivu katika Chuo Kikuu cha Zanzibar-SUZA.

Sambamba na hatua hiyo alimueleza Rais huyo kuwa Zanzibar inaweza kuwapatia mafunzo ya lugha hiyo waandishi wa habari na watengeneza vipindi vya redio na televisheni wa Comoro ili kukuza uwezo wao wa kutengeneza vipindi kwa lugha ya Kiswahili.

Katika mazungumzo hayo Rais wa Comoro Mheshimiwa Ikililou Dhoinine alimueleza Dk. Shein kuwa ingawa wananchi wengi wa nchi yake wanasikia na kufahamu vyema lugha ya Kiswahili lakini wengi wao hawawezi kukizungumza kwa ufasaha.

Aliongeza kuwa pamoja na kuwa televisheni na redio za nchi hiyo zinatangaza vipindi kwa lugha ya Kiswahili lakini vipindi hivyo ni vichache kutokana na  watangazaji wachache wanaozungumza lugha hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi yupo nchini Samoa kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa unaoendelea hapa kwa siku nne. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.