Habari za Punde

Kessy ashambuliwa kama nyuki Ni baada ya kuwabagua Wazanzibari

Na Mwandishi Wetu.
MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ali Mohamed Kessy (CCM), jana alichafua hali ya hewa ya Bunge Maalum la Katiba, baada ya kupinga Rais wa Zanzibar kuwa 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano.
Akichangia mjadala wa katiba mjini Dodoma, Kessy, alisema haiwezekani Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano kwa sababu hakuchaguliwa na wananchi wa Tanzania Bara na kuhoji “anakuja hapa kachaguliwa na nani?”

Hali hiyo ilisababisha majibizano kutoka kwa Wabunge wengine hasa kutoka Zanzibar, lakini Mbunge huyo hakujali na kuendelea kuisakama Zanzibar.

Kilichozua hali ya kutoelewana ni pale Mbunge huyo, aliposema Wabunge kutoka Zanzibar wanapelekwa Dodoma na kulipiwa posho wao, wake zao na watoto wao.

“Hatuwezi kuleta wabunge 83 (kutoka Zanzibar) kuwalisha wao, wake zao na watoto wao,” alisema Kessy, kauli ambayo iliwachafua Wabunge kutoka Zanzibar.

Akiendelea alisema hata gawio la asilimia nne ambalo Zanzibar inapata, inapewa bure kwa sababu haichangii.

“Katiba itamke wazi kila kwamba kila mmoja abebe msalaba wake, hatuwezi kuleta wabunge 83 na kuwalipa posho wao, wake zao na watoto wao,” alisema.


Ingawa wajumbe walikuwa wakipiga mayowe kumtaka akae, lakini Mbunge huyo alijifanya kama hasikii na kuendelea kutoa maneno ya kibaguzi akisema:“Hata hili bunge la katiba hawajachangia, haiwezekani upande mmoja kuumizwa. Kila mmoja abebe msalaba wake.”

Wabunge walishindwa kuvumilia kashfa, ndipo walipoanza kumrushia maneno Kessy wakimwita mwendawazimu, chizi na mwezi mchanga.

Mbunge wa kwanza kutoka Zanzibar kuanza kujibu hoja za Kessy alikuwa Abdalla Sheria, ambae alisema watu kama hao (Kessy) wanaotaka kuchafua Muungano wasiachiwe, huku akimuita Mbunge huyo kuwa muarabu.

Kauli hiyo ilimkera Kessy na kumtaka Sheria aache kumtukana kwa sababu hata yeye (Sheria) ana asili ya Congo.

Mjumbe Juma Ali Khatib alisema inawezeka Kessy ana ajenda ya siri au ametumwa na kukumbusha wakati mbunge huyo aliponusurika kupigwa na Wabunge kutoka CUF.

Alisema Kessy anatumia lugha zinazoudhi na kwamba kazi yake kila siku ni kuwatukana Wazanzibari na kumuonya kama ana matatizo ya akili, atapewa akili.

Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mahmoud Thabit Kombo, licha ya kusema Kessy ana uhuru wa kuchangia na kuheshimiwa mawazo yake, lakini chanzo cha mchakato wa katiba misingi yake ni umoja na mshikamano waliouacha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume na Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema Zanzibar imejitolea utaifa na utambulisho wake na ikajisalimisha kwenye udugu wa damu na kutahadharisha kwamba kamwe udugu hauandikwi kwenye karatasi.

“Kiti cha Zanzibar Umoja wa Matifa kilifutwa, Zanzibar iliacha mambo mengi EAC, Jumuiya ya Madola kwa nia njema (goodwill), baadhi ya viongozi wetu wanajaribu kuondoa nia njema hii, tuwe makini katika hili,” alisema.

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid, alisema baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, asilimia 97 ya Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi walikuwa watu kutoka Tanzania Bara.

Alisema hao ndio waliofaidika na mikopo ya nyumba, wakapata elimu na wengine watoto wao wamo ndani ya bunge hilo.

Aidha, alisema Tanzania ilipovamiwa na Iddi Amini mwaka 1978, kikosi cha kwanza kilichokwenda kukabiliana na wanajeshi wavamizi walikuwa ni askari wa KMKM kutoka Zanzibar.

Akionesha kuchukizwa na kauli za Kessy kwamba Zanzibar ni tegemezi, Hamad alisema Zanzibar ilikuwa na mapato ya kutosha na Rais wa kwanza wa visiwa hivyo, Abeid Amani Karume, alikataa kukopa badala yake alitumia akiba kubwa ya fedha alizokuwa nazo kukopesha matifa mbali mbali ikiwemo Yemen  na serikali ya Muungano.

Alisema Zanzibar ilipungukiwa na fedha katika miaka ya 1984 na mkopo wa mwisho kutolewa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano ilikuwa dola milioni 15. 

“Zanzibar inaweza kujitegemea, inaweza na iliweza, ilikuwa inaisaidia hata Yemen, msijidanganye,” alisema.

Aliwataka viongozi kuwa na tahadhari na kauli zao akitahadharisha kwamba migogoro mikubwa inayoshuhudiwa duniani sasa ni vita vya udini na ukabila, madaraka na kugombea rasilimali.

“Tukiyaendekeza mambo haya udugu wetu utavunjika, hatukuungana kwa mali, tumeungana kwa damu,” alisema.

Steven Wassira alikuwa mtu wa mwisho kumshambulia Kessy, ambae alimtaka kuwa mwangalifu na ulimi kwa sababu vita vyote duniani vinaanzishwa na ulimi wa mtu mmoja na kumuonya kwamba atapata faida gani akiwagawa Watanzania.

Baada ya malumbano hayo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alisema Kessy alikuwa amevunja ibara ya 46(1) h, ambayo inamzuia mjumbe kutotumia lugha za kuudhi, kubagua, kunyanyapaa au kudhalilisha wengine.

Hivyo, alimtaka mjumbe huyo kuomba radhi ambapo licha ya Kessy kuomba radhi lakini alisema alinukuliwa vibaya.

Mapema akichangia mjadala huo, Mbunge John Komba, alimshutumu aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Wariona, kwa kuwa chanzo cha vurugu zinazoendelea kuhusu mchakato wa katiba na kuliomba bunge kumtolea tamko


“Huyu mzee ni shida, sawa na mtu aliefufuka kijijini, inakuwa shida hamkai, sisi tuna mamlaka ya kusema chochote, unapopigwa mtu mzima chuchumaa chini,” alisema.

6 comments:

  1. huyu jamaa anaongea ukweli nyinyi wazanzibari hamutaki kumfahamu tu lakini anachokiongea si ubaguzi kabisa

    ReplyDelete
  2. Nyinyi waznz watu hawakutakini nyiyi munawalazimisha tu, mumeshika hisani hisani, siku hizi hamna kulipa hisani nyinyi mushawasaidia basi, lakini kwa sasa mumekuwa mzigo musikatae. Tenda wema uondoke usingoje shukurani

    ReplyDelete
  3. Hapa mimi ndo ninapohisi kama yale mapinduzi hayana maana au ndo naamini kuwa kayataarisha Nyerere mana wao ndo walonufaika na mapinduzi ya Zanzibar, ukweli tumepinduwa tu lakini hatuwezi kujitawala serekali ya ZNZ imefeli mpaka mishahara itoke Tanganyika?

    ReplyDelete
  4. Kwakweli wamemuonena kawa mbia maneno stahiki wa znz, hauonekane mchangowao bungeni wanachofata wao ni pesatu

    ReplyDelete
  5. Msema kweli ni kipenzi cha Mmungu Ali kessy amesema ukweli ijapokuwa unauma ,watamshambulia ali lakini kiukweli ujumbe umesha fika waliotaka Tanganyika uwafike watu wote Viongozi wetu Zanzibar ni mzigo tena ni mzigo usio na mfano hawjiabishi wao tu wanaabisha jamii nzima ya Kizanzibari tumekuwa ovyo na tutaendelea kuwa hivyo wachina wanasema ukimpa mtu samaki pia umfundishe jinsi ya kuvuwa lakini viongozi wetu hawafundishiki .

    ReplyDelete
  6. Nchi ya Tanzania watu wanaishi kwa uongo na ukiwa unaujua ukweli unalazimika kuugeuuza na kuwa uongo, kwani ukisema ukweli unahatarisha maisha hebu angalieni huyu Mheshimiwa Kessy amesema ukweliii na wala hakuna neno la kuuddhi hata kidogoo lakini ni aibu kwa taifa la Tanzania kuwa waliuficha ukweli huo, badala yake kuongea uongo tuuu.
    Mimi sipendi watu kuishi kwa muda uliopita yaani hawazungumziii maendeleo ya sasa na yajayo bali wao ni kuzungumzia Viongozi wetu waasisi walifanya hiki, walifanya kile kiukweli wazee wlijitahidi kwa moyo mmojaa, Samahanini kama nitawauzi wengine lakini huu ndo ukweli viongozi wetu wa sasa wametawaliwa na Tamaa, Wizii, Urasimuu na Uongoo hivi kweli tutaendelea si dhani ni lazima tubadilike na tuwe na uchungu na nchi pamoja na wananchi hapo kidoogo tunaweza kuaza step moja mbele ya kutafuta maendeleo.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.