Na Khamis Amani
IKIWA ni mwaka mmoja, miezi
minne na siku 19 zimepita, tokea kuuawa kwa Padri Evaristus Gabriel Mushi na
upelelezi wake ukiwa bado haujakamilika, Mahakama Kuu ya Zanzibar imetoa muda
wa mwisho wa kuendelea na kesi hiyo.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar
Othman Makungu, ambae ndie anaesikiliza kesi hiyo, alisema Oktoba 3 mwaka huu
ataiondoa kesi hiyo mahakamani ikiwa upande wa mashitaka utashindwa kukamilisha
upelelezi huo.
Uamuzi huo wa mahakama umekuja
baada ya kesi hiyo inayomkabili Omar Mussa Makame (35) kukaa kwa muda mrefu
bila ya kusikilizwa, huku upande wa mashitaka ukiomba muda zaidi wa kukamilisha
upelelezi huo ombi ambalo lilipingwa na upande wa utetezi.
Upande wa utetezi ulioongozwa
na Wakili wa kujitegemea Abdallah Juma Mohammed wa kampuni ya AJM Soliciter
& Advocate Chamber, aliiambia mahakama hiyo kuchoshwa na nyimbo za mara kwa
mara za upande wa mashitaka juu ya upelelezi wa kesi hiyo ambapo kila kesi hiyo
inapoitwa mahakamani upande huo unadai haujakamilika.
Alidai, madai ya upande wa
mashitaka ya kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hayana msingi wowote,
ukizingatia kesi hiyo ni ya muda mrefu.
Hivyo, wakili huyo aliiomba
mahakama imwachilie huru mteja wake bila masharti yoyote na upande wa mashitaka
ukijipanga unaweza kuirudisha tena mahakamani kesi hiyo kwa mujibu wa taratibu
za kisheria.
“Mheshimiwa jinai haiozi,
wanaweza wakaileta tena mahakamani wakati wowote baada ya kujipanga, kuachiliwa
huru kwa mteja wangu haina maana kama haitafunguliwa tena kesi hii”,
alifahamisha Wakili huyo.
Wakili wa serikali kutoka Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Abdallah Mgongo licha ya kukiri kwamba kesi
hiyo ni ya muda mrefu,aliiomba mahakama kuangalia uzito wa kesi hiyo ili kuona
haki inatendeka.
Alidai kuiahirishwa kwa ajili
ya kuendelea na upelelezi wa kesi hiyo ni sababu ya msingi kwa upande wao,hivyo
aliiomba mahakama kuipangia tarehe nyengine ya kutajwa ili kuendelea na
upelelezi huo.
Aliai upande wa mashitaka una
jukumu la kusimamia mwenendo wa kesi mahakamani na suala la upelelezi lipo
chini ya mikono ya polisi kwa mujibu wa kifungu cha 74 (1) cha sheria za
mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar.
“Ni kweli hili shitaka ni la muda mrefu kwa hesabu za haraka haraka
limeahirishwa mara 22, hatuwezi kusema ni lini upelelezi wake utakamilika,”
alidai.
Hoja hizo zilipingwa na Wakili
wa utetezi kwa madai shitaka hilo halistahiki kuwepo mahakamani, kutokana na
upande wa mashitaka kushindwa kukiri lini suala la upelelezi litakwisha na ni uthibitisho
tosha kuwa kesi hiyo itaendelea kufikishwa mahakamani na kumpotezea muda mteja
wake.
Baada ya kusikiliza hoja za
pande mbili hizo, Jaji Omar Othman Makungu alikiri kuwa ni shitaka la muda
mrefu lakini si busara kuondoshwa mahakamani kwa kushitukiza bali inapaswa
kutolewa muda wa ziada kwa upande wa mashitaka ili kujipanga zaidi.
Hivyo aliupa muda wa mwisho
upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi huo na endapo katika kikao kijacho
utashindwa, mahakama italiondosha shauri hilo.
Kesi hiyo ilifunguliwa kwa mara
ya kwanza mahakamani hapo Aprili 5 mwaka jana, ambapo mshitakiwa huyo alisomewa
shitaka la kuua kwa makusudi kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya kanuni ya
adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Siku hiyo mshitakiwa huyo akiwa
mbele ya Mrajis wa Mahakama Kuu George Joseph Kazi, alidaiwa kumuua kwa
makusudi Evaristus Mushi tukio lililodaiwa kutokea Beit el ras wilaya ya magharibi
Unguja, majira ya saa 12:50 za asubuhi ya Februari 17 mwaka jana.
No comments:
Post a Comment