Na Othman Khamis, OMPR
MJUMBE wa Bunge Maalum la
Katiba, Hamad Rashid Mohamed, amesema dhambi kubwa itafanywa na wajumbe wa bunge
hilo kama watawakosesha Watanzania rasimu ya katiba mpya wanayoisubiri kwa
shauku kubwa.
Alitoa kauli hiyo wakati akitoa
nasaha zake kwa niaba ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wa kundi la 201
kutoka Zanzibar, kwenye chakula cha jioni kilichoandaliwa na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, nyumbani kwake mtaa wa Farahani mjini
Dodoma.
Alisema wajumbe hao wamebeba dhima kubwa kwa
kukubali kwao kula kiapo kilichokwenda sambamba na kutumia kodi za wananchi
zilizotolewa kwa kutakiwa kuwatengenezea katiba mpya.
Alisema wajumbe wa bunge hilo hasa
wale waliotoka vyama vya upinzani na taasisi za kijamii wanapaswa kusimamia
vyema ukamilishaji wa rasimu inayopendekezwa na bunge ili kukata kiu waliyonayo
Watanzania kwa kipindi kirefu sasa.
Alisema vyama vya upinzani zikiwemo taasisi za
kijamii na wana harakati ndio waliosimama kidete kudai uwepo wa katiba mpya
jambo ambalo lilikuwa zito kukubaliwa na CCM.
“Hakuna nji nyengine yoyote ya mkato katika
kukipa changamoto chama cha Mapinduzi isipokuwa upande wa upinzani kukubaliana
na rasimu iliyoandaliwa na Bunge maalum la katiba itakayopelekwa kwa wananachi
kwa ajili ya kupigiwa kura,” alisema.
Alitahadharisha kwamba
Watanzania wamejinyima mambo ya msingi likiwemo kuwapatia elimu watoto wao na
kuamua kodi wanazochangia kuzielekezwe kupata katiba mpya.
Aliwanasihi viongozi wa kisiasa
pamoja na jamii kuzikimbia chokochoko za kisiasa zinazochangia cheche ya
kusambaratisha jamii kama zilivyotokea mataifa mbali mbali Duniani.
Alisema Tanzania hadi sasa bado haijafikia
hatua za watoto pamoja na wake wa Wabunge kuteswa, kudhalilishwa hadi kufikia
hatua ya kubakwa kutokana na vurugu zinazotokana na siasa na hitilafu za kidini
kama zinavyofanyika katika mataifa mengine.
Alisema Tanzania ina fursa
kubwa ya kidemokrasia iliyojengeka tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi
vya siasa ambayo imekuwa ikipatikana ndani ya vyombo vyake vya maamuzi.
Mapema akiwakaribisha wajumbe hao wa bunge hilo, Balozi Seif alisema rasimu iliyoandikwa na bunge hilo
imeisaidia Zanzibar kwa zaidi ya asilimia 90 na kusababisha malalamiko kwa Watanzania Bara.
Alisema wakati huu ni muhimu na
ndio mahali pekee pa kupata maslahi ya Zanzibar ndani ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania, vyenginevyo Zanzibar itaendelea kulalamikia kero za Muungano
endapo rasimu inayopendekezwa na Bunge maalum haitapita.
Aliwakumbusha wajumbe wa bunge
hilo kwamba Zanzibar ilikuwa na malalamiko mengi kuhusu kero za Muungano
masuala ambayo sasa ni muda muwafaka wa kuyamaliza kupitia mchakato huo.
Alisema koti la Tanzania Bara linalodaiwa
kuvaliwa ndani ya mambo yasiyo ya Muungano litavuliwa iwapo rasimu hiyo itapigiwa
kura na kupita.
No comments:
Post a Comment