Habari za Punde

Serikali kufanya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya kwa mwaka 2014/15

Na Faki Mjaka-Maelezo
 
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatarajia kufanya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya kwa Mwaka 2014/15 ambao utasaidia kutoa viashiria mbali mbali kwa ajili ya kutathmini Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA).
 
Utafiti huo utazishirikisha Kaya 4,560 katika maeneo 380 ya kuhesabiwa Watu yaliyochaguliwa kitaalamu katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.
 
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis ameyasema hayo alipokuwa akifungua Mafunzo ya Wadadisi, Wasimamizi na Wahariri wa Utafiti huo yaliyofanyika Ukumbi wa Kwawazee Sebleni Mjini Zanzibar.
 
Amesema Utafiti huo utakaoendeshwa kitaalamu utaanza rasmi Octoba 6 mwaka huu na kuchukua miezi 12 kumalizika kwake.
 
Mkuu huyo wa Mkoa amefahamisha kuwa hakuna lengo binafsi la kuwachunguza Wananchi hali zao za maisha katika utafiti huo badala yake unakusudia kukusanya Takwimu sahihi za Mapato na Matumizi ya Kaya husika ili kutathimi hali halisi kwa Maendeleo ya Taifa.  
 
Abdallah amesema dhamana ya Mafanikio ya utafiti huo ipo Mikononi mwa Washiriki hao hivyo wanapaswa kujitahidi katika mafunzo hayo ili lengo lililokusudiwa liweze kutimia.
 
Ametoa Wito kwa Masheha wa Shehia na watendaji wengine katika maeneno yatakayohusika na Utafiti huo kutoa mashirikiano kwa Wadadisi na Wasimamizi wa Utafiti huo ili kutimiza lengo.
 
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mohamed Hafidh Rajab amefahamisha kuwa Utafiti huo utasaidia kupata Takwimu zitakazosaidia kupata Mchanganuo na kadirio la Pato la Taifa sambamba na kujua Mfumuko wa Bei unavyoenda nchini.
 
Mafunzo hayo ya Watafiti yanayodhaminiwa na Benki ya Dunia kupitia Mpango mkuu wa kuimarisha Takwimu Tanzania yanawashirikisha Wadadisi na Wasimamizi 217 Unguja na Pemba,ambapo yatachukua jumla ya siku 18 kumalizika kwake.
 
Utafiti wa Mwaka 2014/15 ni wa mara ya Tano kufanyika tokea Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 ambapo Utafiti wa mwaka 2009/10 ulionesha kuwa Asilimia 44 ya Wazanzibari hawamudu Mahitaji yao ya Chakula na mambo mengine.
 
IMETOLEWA NA MAELEZO ZNZ

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.