Habari za Punde

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                      Jumatatu, 01 Setepemba , 2014
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya mataifa duniani kuimarisha ushirikiano na kuongeza nguvu ili kuziwezesha nchi zinazoendelea zikiwewo za visiwa kukabiliana na ongezeko la athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa hivyo amezitaka nchi zinazoendelea kwa umoja wao kuzishawishi nchi zilizoendelea kuongeza uhaulishaji wa tekinolojia salama na zisizochafua mazingira, kusaidia kuzijengea uwezo na kuhakikisha kunakuwepo fedha zaidi kuziwezesha nchi hizo kukabialiana na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa unaofanyika Apia, Visiwa vya Samoa leo, Dk. Shein amewahakikishia wajumbe wa mkutano huo kuwa Tanzania inaunga mkono kwa dhati maudhui ya mkutano huo unaozungumzia maendeleo endelevu katika nchi za visiwa.
Kwa hivyo aliwaeleza kuwa hatua za haraka hazina budi kuchukuliwa na kuimarisha ushirikiano katika ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 na kufafanua kuwa jambo la kupewa kipaumbele liwe ni kuongeza kasi ya jitihada za katika hifadhi ya mazingira na kuondoa umasikini.
Katika mnasaba huo aliongeza kuwa ni muhimu kuyafanyiakazi Malengo ya Milenia ambayo bado hayajafikiwa ili nchi za visiwa ziweze kujihami dhidi ya majanga yaliyo nje ya uwezo wao.
Kwa hivyo Dk. Shein alifafanua kuwa Malengo ya Milenia yanayohusiana na kuondoa umasikini, mazingira endelevu, afya ya wanawake na watoto, usawa na kijinsia na suala la uwezeshaji wa utekelezaji wake hayana budi kuchukua nafasi ya mbele katika ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.
Aliyataja maeneo mengine kuwa ni pamoja na kuwepo kwa fursa sawa za elimu kwa wote, kuhimiza uwekezaji, uendelezaji wa sekta ya utalii ili kuinua kiwango cha ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira.
Kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi Dk. Shein alieleza kuwa suala hilo ndio tishio kubwa la uhai na uwepo wa nchi za visiwa na kuongeza kuwa jamii katika nchi hizo zinaendelea kushuhudia athari za mabadiliko hayo katika shughuli zao za maisha ya kila siku kama vile katika uvuvi, kilimo na huduma ya maji ambazo zimevamiwa na maji chumvi.
Dk. Shein alisema mkutano huo unatoa fursa ya kipekee kwa nchi za visiwa na washirika wa maendeleo kujadili na kupendekeza namna ya kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi za visiwa katika kutekeleza azma yake ya kupata maendeleo endelevu.
Hata hivyo alifafanua kuwa nchi za visiwa kuwa ndogondogo, kuwa mbali na kutofikika kirahisi, kukabiliwa na majanga ya asili mara kwa mara na sababu nyingine zilizo nje ya uwezo wao ni miongoni mwa mambo yanayofanya safari ya nchi hizo kufikia maendeleo endelevu kuwa ya mashaka kuliko nchi nyingine katika kundi hilo la nchi zinazoendelea.
Miongoni mwa wajumbe waliofutana na Dk. Shein ambaye anahudhuria mkutano huo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Adulhabib Ferej.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

1 comment:

  1. Huu ni mkutano wa nchi za visiwa. Sasa iweje Raisi wetu amuakilishe Raisi Kikwete wa Jamuhuri ya Tanzania??.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.