Na Haroub Hussein, Dar es
Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa taasisi za kodi Afrika.
Mkutano huo utakaoanza tarehe
15 hadi 19 mwezi huu utafunguliwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dk. Mohammed Gharib
Bilal.
Akizungumza na waandishi wa
habari katika ukumbi wa idara ya habari maelezo jijini hapa, Kamishna Mkuu wa
TRA, Rished Bade, alisema Tanzania imepata fursa kwa mara ya kwanza kuandaa
mkutano huo muhimu kwa taasisi za kodi ambapo utakua mkutano wa tatu tangu
kuanzishwa kwa taasisi za kodi Afrika (ATAF) mwaka 2009.
Alisema lengo la mkutano huo ni
kujadili namna ya kuimarisha taasisi za kodi Afrika, kujenga uwezo wa watumishi
katika taasisi za kodi, kubadilishana uzoefu wa ukusanyaji wa kodi katika sekta
mbali mbali pamoja na kubadilishana taarifa muhimu za biashara za kimataifa na
uwekezaji katika nchi za Afrika.
Aidha alisema mkutano huo
utawakutanisha wakuu wa mamlaka za mapato, wataalamu wa masuala ya kodi kutoka
mataifa 37 ya Afrika ambao ni wanachama wa ATAF pamoja na wafadhili ambapo
watajadili masuala mbali mbali ya kodi katika bara la Afrika pamoja na kuchagua
baraza jipya la ATAF.
Alisema mada mbali mbali
zitajadiliwa katika mkutano huo ikiwa pamoja na uongozi katika ajenda ya kodi kimataifa,
kuzingatia weledi, kanuni na misingi bora ya uongozi na utawala, usimamizi wa rasilimali
watu, usawa wa jinsia katika mafanikio ya makampuni, taswira za kodi Afrika
pamoja na kuunda fursa za baadae kwa Afrika katika kodi za kimataifa.
Alisema mbali na washiriki wa
mkutano huo kujadili masuala ya kodi pia watapata fursa ya kutembelea vivutio
vya utalii vilivyopo Tanzania.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni ‘Tathmini
ya Uongozi na mikakati ya usimamizi wa ajenda ya kodi Afrika.’
No comments:
Post a Comment