Na Khamis Mohammed
TUME ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC), imekamilisha awamu ya kwanza ya kazi ya uchunguzi wa idadi, majina na
mipaka ya majimbo ya uchaguzi Zanzibar
baada ya kupokea maoni mbali mbali ya wadau Unguja na Pemba.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti
wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alipokuwa akizungumza na waandishi habari ofisi za
ZEC, Maisara mjini Unguja jana ambapo alisema, kinachofanyika hivi sasa ni
kuyachambua maoni yaliotolewa katika mchakato huo uliochukuwa karibu miezi
mitatu.
Alisema katika utaratibu huo wa
kupokea maoni ya wadau juu ya idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi,
ZEC ilikutana ana kwa ana na kupokea
maoni ya vyama vya siasa 14 vikiwemo vya CCM na CUF huku vyama vyengine vinane
viliwakilisha maoni yao kwa maandishi.
Alizitaja taasisi nyengine zilizotoa maoni ni pamoja na Wabunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na
Wawakilishi wa Asasi mbali za kijamii pamoja na wananchi.
Alisema maoni makuu
yaliosikilizwa na kupokelewa na tume ni pamoja na matatizo ya mipaka ya majimbo
katika wilaya, wadi za uchaguzi na mipaka ya shehia, matatizo ya majimbo yatokanayo na mgawanyo wa hali ya jiografia,
ongezeko la idadi ya watu katika majimbo ya wilaya na maoni ya jumla ya wadau.
"Yapo baadhi ya majimbo
yenye idadi kubwa ya watu na mengine yakiwa na idadi chache na kukosekana kwa
uwiano katika mgawanyo wa majimbo uliopo hivi sasa," alisema.
"Watu wanazaliana, mamlaka
zinapeleka huduma, lakini ni vyema
kukawepo uwiano wa kuwahudumia," alisema.
"Katiba haijasema kuwa lazima jimbo lizingatie idadi ya watu, lakini inataka kuangaliwa uwiano na ZEC itazingatia hilo,"
alisema.
Alisema ZEC haijakaa kwa lengo la ukataji au upunguzaji wa majimbo ya
uchaguzi na kwamba kinachofanyika ni uvumi unaoenezwa na watu wachache kwa
maslahi binafsi.
"Ni uvumi na hofu za
wanasiasa, ZEC haijafanya uamuzi huo kwa sasa,"alisema.
Naye Mkurugenzi wa ZEC, Salum
Kassim Ali, alisema, kazi hiyo inaendeshwa kwa matakwa ya katiba ambayo inaelekeza kufanyika kila baada
ya miaka minane hadi 10 ambapo mara ya mwisho
ilifanyika mwaka 2005 ikiwa sasa ni miaka tisa tokea Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar ilipofanya
uchunguzi wa idadi, mipaka na majina ya majimbo ya uchaguzi.
Alisema, kulikuwepo na
changamoto mbali mbali juu ya zoezi hilo la ukusanyaji wa maoni ikiwemo baadhi
ya maeneo watu kuonekana kuwa na jazba za kisiasa.
"Watu walikuja kama vile ilivyokuwa wakati wa ukusanyaji wa
maoni ya katiba mpya ya Tanzania, lakini, mishowe walituelewa na kufanikisha
kazi yetu.
Juu ya mchakato huo kuhodhiwa
na wanasiasa, alisema,ZEC imejidhatiti kufanikisha mchakato huo kwa kuzingatia
matakwa ya katiba na kwamba haitokuwa na nafasi ya kwenda kinyume na matakwa
hayo kwa maslahi ya taifa na wananchi wake kwa ujumla.
"Mtaji wa wanasiasa ni
wapiga kura, huo ndio uhalisia, lakini si katika hili," alisema.
Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo
kwa baadhi ya majimbo yenye idadi kubwa ya watu likiwemo jimbo la Fuoni lenye
watu zaidi ya 60,000, Dimani watu 58,000 na Dole lenye idadi ya watu karibu
35,000.
"Haya ni baadhi ya majimbo
yenye idadi kubwa ya watu, lakini, yapo yenye idadi chache likiwemo jimbo la
Rahaleo, Chambani na Mgogoni," alisema.
No comments:
Post a Comment