Na Kauthar Abdalla
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania imesema itahakikisha inazifanyia kazi changamoto zinazoikabili
sekta ya usafiri wa anga ili kuimarisha usalama wa sekta hiyo.
Waziri wa Usafirishaji, Dk. Harison
Mwakyembe, aliyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Mbwana Juma
Mbwana, katika mkutano wa kwanza wa
jumuiya ya vyuo vya usafiri wa anga uliofanyika hoteli ya Ocean View Kilimani
Zanzibar.
Alisema pamoja na kuimarika kwa
sekta hiyo katika miaka ya hivi karibuni bado kuna mambo kadhaa yanatakiwa
kufanyiwa kazi ili kuchochea kazi ya maendeleo ya nchi.
Alisema usafiri wa anga ni moja
ya sekta zinazopelekea ukuaji wa uchumi kwa haraka hivyo ukuaji wake na uimara
wa miundombinu ya sekta hiyo ni lazima iendane na mahitaji ya kazi ya ukuaji
wake.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa
usafiri wa anga katika uchumi wa Afrika,Mawaziri wanaohusika na sekta hiyo
waliazimia kuanzisha mikakati ya kitaifa,kikanda na bara zima ili
kuhakikisha usalama wake kwa lengo la
kuchangia sekta nyengine za uchumi hivyo umoja huo ni lazima uzingatie
utekelezaji wa majukumu yake,” alisema.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
mamlaka hiyo Dk.James Diu, alisema mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto mbali
mbali ikiwa ni pamoja na kutokuwa na wataalamu wa kutosha katika fani hiyo
jambo ambalo linakwamisha harakati za kimaendeleo katika jumuiya na kushindwa
kuendelea mbele.
Malengo mkakati ya mamlaka ya
usafiri wa anga Tanzania ni pamoja na kuwa na sauti ya pamoja ya vyuo wanachama
na kuhimiza vyuo hivyo kuendeshwa kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na
kimataifa.
No comments:
Post a Comment