Na Mwandishi Maalum, New York
Nchi zinazoendelea hususani Afrika,
Kusini mwa Jangwa la Sahara zimeshauriwa kujiwekea mipango, sera, taratibu na sheria
zinazotekelezeka ambazo kwayo zitaongeza na
kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili si tu kuongeza kasi ya
ukuaji wa uchumi wake lakini pia kuwa na
maendeleo endelevu.
Aidha
nchi hizi zimeambiwa kuwa
kile kipindi cha kusubiri kuletewa maendeleo kwa maana ya kuwategemea
wafadhili kupitia uwekezaji wa moja kwa
moja ( FDI) au misaada kimeshapita kwa kuwa
hakuna nchi inayoweza kuleta maendeleo kwa nchi nyingine.
Hayo yamejitokeza siku ya Jumanne hapa Umoja wa Mataifa, wakati wa majadiliano yasiyo rasmi ya mada iliyohusu mapato ya ndani ( public financing) kama njia moja wapo ya uwezeshaji wa
maendeleo endelevu. Majadiliano haya yanafanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya
Mkutano wa Tatu wa Kimataifa juu ya
Uwezeshaji wa Raslimali Fedha kwa Maendeleo Endelevu. Mkutano
utakofanyika mapema mwakani huko Addis
Ababa, Ethiopia.
Ujumbe wa Tanzania katika majadiliano haya unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bibi Dorothy Mwanyika.
Mchokoza mada wa majadaliano hayo, Profesa Atul Kohli
kutoka Chuo Kikuu cha Princeton cha
Marekani, ameeleza si tu kwamba hakuna nchi au mtu anayeweza kumletea maendeleo mwingine lakini pia
hakuna mfumo mmoja wa maendeleo ambao
unaweza kutumika kwa nchi zote.
Amesema nchi nyingi za Afrika Kusini
mwa Jangwa la Sahara zimendelea kuwa
nyuma kimaendeleo tofauti na baadhi ya
nchi za Asia, kwakuwa zimeendelea kuwa tegemezi wa misaada ya nje na vile vile
kuwa na madeni makubwa.
Profesa Kohli amesema, nchi masikini zinaweza kujifunza mambo
mawili au matatu kutoka nchi zenye uchumi
wa kati kama vile Korea ya Kusini na Malaysia ambazo pamoja na kuwa na utashi
wa kisiasa wa kuondokana na utegemezi
pia ziliamua kwa dhati pamoja na mambo mengine kuibua vyanzo vya mapato
yao ya ndani na kuwa na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato hayo pamoja na
matumizi yake.
Aidha
amesema hakuna nchi ambayo imeweza kupiga hatua kubwa ya kiuchumi na
kimaendeleo pasipo kufanya mageuzi ya viwanda ikiwa ni pamoja na kuvilinda
viwanda vyake.
“Hakuna nchi ambayo imeweza kupata
mafanikio makubwa katika eneo la viwanda
bila serikali kuingilia kati au
kusaidia. Ipo mifano hai ya namna
ambavyo hata serikali za mataifa makubwa zilifanya katika karne za 18, 19 na
20 kulinda viwanda vyao dhidi ya bidhaa kutoka nje”. Amesema Profesa Atul Kohli.
Uzalishaji wa bidhaa kwaajili ya masoko ya nje ni moja ya eneo ambalo siyo tu linaongeza mapato ya ndani lakini pia
inaifanya nchi kutokuwa mwagizaji zaidi wa biadhaa kutoka nje.
Aidha ameeleza kuwa utashi wa
kisiasa, nchi imara, viongozi wanaowajibika wasiokuwa waoga katika kusimamia
vipaumbele wanavyovipanga ni moja ya sababu ambayo baadhi ya nchi zenye uchumi wa kati zimefika
hapo zilipo.
Amesisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na upanuzi wa wigo wa
mapato hayo, unahitaji pia watendaji wanaowajibika na ambao wako tayari kuziba
mianya ya ukwepaji kodi na wanaowajibika kwa wananchi wao kwa kuwa
wanamkataba nao.
“Ni lazima msimamie maendeleo
yenu kutokana kile mlichonacho bila ya kutegemea misaada
kutoka nje. Imarisheni vyanzo vyenu vya mapato,uwekezaji wa ndani na mitaji ya
kijamii. Mnaweza kutegemea misaada ya
nje muhimu lazima muwe na mapato yenu imara ambayo hayatawafanya muwe tegemezi”, amesisitiza Profesa
Kohli.
Akichangia majadiliano hayo, Naibu
Katibu Mkuu, Bibi Dorothy Mwanyika
amesema, nchi nyingi zinazoendelea
Tanzania uzoefu umeonyesha kuwa
upatikanaji wa misaada kutoka nje na inayotolewa kwa wakati na inayotabilika
imeweza kutoa unafuu kwa nchi
zinazoendelea ambazo hazina uwezo wa kukusanya
mapato yake zenyewe.
Hata hivyo ameeleza kuwa hivi sasa nchi
zinazoendelea zimegudua kuwa siyo tu kuwa misaada hiyo haitoshi lakini wakati mwigine
haitabiriki huku ikiwa ni ya muda mfupi. Na kubwa zaidi sehemu kubwa ya misaada hiyo
ikirudi kule ilikotoka ili hali walengwa wakinufaika kidogo.
Akasema ni kutoka na uzeofu huo ndiyo maana
Tanzania inathamini mfumo huu mpya wa
kuwa na vyanzo tofauti vya mapato vitakavyosaidia kusukuma mbele ajenda za
maendeleo endelevu baada ya 2015.
Naibu Katibu Mkuu amesema ni kwa
kulitambua hilo ndiyo maana Tanzania
imejiwekea taratibu za kuhamasisha raslimali za ndani ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa vyanzo vya mapato yake ukusanyaji wa kodi na kuziba mianya ya ukwepaji
kodi pamoja na kupunguza misamaha ya kodi.
Vile vile Bibi Mwanyika amesema, nchi zilizoendelea zinatakiwa kuongeza kasi ya ushirikiano wake
katika udhibiti wa utoroshaji wa fedha
pamoja na fedha chafu jambo ambao
amelieleza kuwa linachangia
katika kuzifanya nchi zinazoendelea kukosa mapato ya kutekeleza mipango ya maendeleo.
Naibu Katibu Mkuu pia amegusia suala la mzigo wa madeni
kwa nchi zinazoendelea na kueleza kuwa
ni mzigo unaozielemea nchi hizo na hasa
ikizingatiwa zina lazimika kukopa ili
kuziba pengo la upugufu wa mapato yake.
No comments:
Post a Comment