Na Fatma Kassim
Waziri wa Afya wa Zanzibar,
Mhe. Rashid Seif Suleiman, amesema Zanzibar inafaidika na misaada mbalimbali
inayotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) katika kupambana na vifo vya wajawazito
na watoto wachanga.
Akifungua mkutano wa wafanyakazi
wa WHO nchini Tanzania katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort,alisema misaada
hiyo inatokana na programu mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo ambazo kwa
kiasi kikubwa zimechangia kupunguza vifo vya watoto wachanga na mama
wajawazito.
Alisema kwa muda mrefu Zanzibar
ilikuwa inakabiliwa na matatizo mbali mbali lakini kupatikana kwa ofisi ya
kudumu na wataalamu wa shirika hilo nchini,matatizo hayo yamepungua.
Alilifahamisha shirika hilo kamba
Zanzibar imechukua hatua madhubuti kuzuia kuingia ugonjwa wa ebola kwa kuweka
udhibiti na upimbaji wa watu katika mipaka ya kuingilia nchini.
Mwakilishi Mkaazi wa WHO,
Rofaro Chatora, alisema mkutano huo una lengo la kuangalia changamoto
wanazokabiliana nazo katika utendaji wao wa kazi sambamba na kupanga mikakati
mipya ya kuimarisha ufanisi wa kazi zao.
Alisema kwa mwaka 2015
wanakusudia kuisaidia Zanzibar kifedha katika kutekeleza sera zake za
kuimarisha afya ikiwemo kuwapatia mafunzo wafanyakazi, kuimarisha utafiti
katika
masuala ya afya.
Mambo mengine ni kufuatilia hali
ya maradhi yanayoambukiza na yasiyoambukiza sambamba na kuwajenga uwezo wataalamu
wa afya wa Zanzibar kwa lengo la kuongeza ushirikiano wa kimataifa.
WHO limekuwa likiisaidia
Zanzibar katika harakati za kupambana na maradhi mbali mbali ikiwemo UKIMWI, kifua
kikuu, malaria na afya ya mama na mtoto ambapo katika mkutano huo wa siku nne wafanyakazi
wa WHO waliopo Tanzania watajadili mambo mbalimbali ya kuongeza ufanisi wa kazi
zao.
No comments:
Post a Comment