Habari za Punde

Balozi Seif: CCM bado madhubuti na inazidi kuimarika

 Mlezi wa CCM Mkoa wa Magharibi Balozi Seif akipandisha Bendera ya CCM Mbele ya Tawi la CCM Mombasa kwa Mchina kabla ya kuweka jiwe la msingi la Twi hilo
  Balozi Seif  ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akiweka jiwe la msingi la Tawi la CCM Mombasa kwa Mchina.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Tawi la CCM  Mombasa  kwa Mchina Nd. Ahmada Yahya Abdulwakil akitoa ufafanuzi wa ujenzi mbele ya Mlezi wa CCM Mkoa wa Magharibi Balozi Seif mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la Tawi hilo.

 Mlezi wa CCM Mkoa wa Maghribi Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika Picha ya pamoja na uongozi mzima wa Tawi la CCM Mmobasa kwa Mchina, Wilaya ya Dimani na Mkoa wa Magharibi mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la Tawi hilo.
Wanachama wapya 79 wa CCM na Jumuiya zake wa Tawi la CCM Mombasa kwa Mchina wakila liapo mara baada ya kukabidhiwa kadi na Mlezi wa CCM Mkoa wa Magharibi Balozi Seif Ali Iddi.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
 
Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema wimbi la vijana wa vyama vya upinzani kuamua kuvihama vyama hivyo na kujiunga na CCM ni dalili za umadhubuti  wa chama hicho unaoonekana kuimarika kila wakati.
 
Alisema chama cha Mapinduzi chenye sera  na ilani imara inayokiwezesha kushinda kila baada ya miaka mitano tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania ndio kimbilio la watu wote wenye busara ya kutaka kujiunga na ulingo wa siasa.
 
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mlezi wa Mkoa wa Magharibi Kichama alisema hayo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Tawi la Chama cha Mapinduzi Mombasa kwa Mchina Wilaya ya Dimani Mkoa wa Magharibi.
 
Alisema makundi ya wafuasi wa vyama vya upinzani wanaoamuwa wenyewe kuvihama vyama vyao na kujiunga na Chama cha Mapinduzi ni muelekeo wa ishara kwa CCM kuendelea kuongoza dola katika uchaguzi  Mkuu ujao wa mwaka 2015.
 


Hata hivyo Balozi Seif aliwatahadharisha Viongozi na Wanachama wa CCM wasikae na kubweteka na mawazo ya kushinda uchaguzi bila ya sera na mikakati ya kujipanga vyema kwa ajili ya ushindi huo.
 
Aliwaomba wana CCM popote pale walipo nchini Tanzania kuendelea kushikamana na kuacha majungu, fitna na makundi ili  ushindi uwe rahisi zaidi ya chaguzi zote zilizopita za mfumo wa vyama vingi hapa Nchini.
 
Balozi Seif aliupongeza Uongozi, wanachama na  wapenzi wa chama hicho waliojitolewa kwa nguvu zao na kuhakikisha kwamba ujenzi wa Tawi la Mombasa kwa Mchina unasimama imara.
 
Alisema licha ya kuungwa mkono na wapenzi na watu tofauti katika ujenzi wa Tawi hilo lakini nguvu za ukamilishaji wa tawi hilo zitaendelea kubakia mikononi mwa Viongozi pamoja na Wanachama wenyewe wa Tawi hilo.
 
Aliutaka uongozi wa Mkoa wa  Magharibi kuwa na tahadhari ya uvamizi wa makaazi unaofanywa na baadhi ya watu kwa lengo maalum la kuongeza nguvu za  kuimarisha vyama vya kisiasa katika kujiandaa kwa uchaguzi Mkuu ujao.
 
Balozi Seif akiwa pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar   aliwakumbusha masheha na Wakuu wa Wilaya  nchini kuendelea kufuata sheria za nchi ipasavyo ili kila mwenye haki yake anapata fursa  bila ya vikwazo,ubaguzi wala itikadi za kisiasa.
 
Alisema tabia ya baadhi ya watu zaidi wana siasa kushindikiza masheha kutoa vibali  kwa wafuasi au vijana wao kwa kutaka kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi wakati muda wa ukaazi wa vijana hao haujatimia ni kuvunja sheria za nchi.
 
“ Suala hili la kutishwa masheha na kulaumiwa Wakuu wa Wilaya nililikemea nilipokuwa katika ziara yangu wiki hii Kisiwani Pemba. Na hapa nalirejea tena kwa kuwakumbusha masheha na wakuu hao wa Wilaya kufanya kazi zao kwa kujiamini “. Alisema Balozi Seif.
 
Aliwataka na kuwaasa vijana kujiepusha na ushawishi huo wa wana siasa wa kutaka kuwalazimisha kufanya mambo yaliyo kinyume na sheria na utaratibu wa Nchi.
 
Katika kuunga mkono ujenzi wa Tawi hilo la Mombasa Kwa mchina Mlezi huyo wa Mkoa wa Magharibi Kichama Balozi Seif aliahidi kukamilisha ukumbi wa Tawi hilo kwa kutoa mchango wa Jipsam, taa ,mafeni yote ukumbini hapo pamoja na kusaidia  Seti moja ya Jezi kwa Timu kati ya timu 16 zilizomo ndani ya Tawi hilo .
 
Mapema akitoa Taarifa fupi ya ujenzi wa Tawi hilo Mwenyekiti wa Ujenzi ambae pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM  Nd. Ahmada Yahya Abdulwakil  alisema ujenzi huo ulioanza rasmi Tarehe 28 Septemba 2013 umekuja kufuatia wanachama hao kukosa ofisi ya kufanyia kazi  zao za Kisiasa.
 
Nd. Ahmada alisema tawi hilo lenye ofisi zote zinazohitajika zikiwemo za jumuiya za chama litakuwa na huduma za kisasa zinazokwenda na wakati  pamoja na ukumbi wa Mikutano ambao utakodishwa kwa shughuli za kijamii ili kuliongezea mapato Tawi hilo.
 
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ujenzi wa Tawi la CCM Mombasa kwa Mchina aliwashukuru viongozi na wapenzi wote wa chama hicho waliojitolea kuunga nguvu katika ujenzi wa Tawi hilo lenye hadhi ya chama chenyewe.
 
Katika hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi la Tawi la CCM Mombasa Kwa Mchina Balozi Seif alikabidhi kadi kwa wanachama wapya  79 wa chama cha Mapinduzi pamoja na Jumuia zake wa Tawi hilo.
 
Ujenzi wa  Tawi la Chama cha Mapinduzi Mombasa kwa Mchina  hadi sasa umeshagharimu zaidi ya shilingi Milioni 45,100,000/- .
 
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.