Habari za Punde

Dk Shein apokea gwaride la wanariadha


STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

  Zanzibar                                                                                                           26.12.2014

---

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepokea gwaride la wanariadha kutoka Wilaya kumi za Zanzibar na kuwataka washiriki vizuri pamoja na waamuzi kutenda haki katika mashindano hayo kwani nia ya Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kufufua vuguvugu la michezo kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.
 
Mapokezi hayo ya gwaride la wanariadha wa Zanzibar pamoja na waamuzi wa mashindano hayo ambapo pia liliwashirikisha wanamichezo wenye ulemavu, yaliyofanywa na Dk. Shein yalifanyika katika uwanja wa Amaan mjini Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali, michezo pamoja na wanamichezo na wananchi.
                                                                          
Akiwasalimia wanaridha hao mara baada ya kupokea gwaride lao lililopita mbele yake likiongozwa na Brassband kutoka Chuo cha Mafunzo Zanzibar, Dk. Shein aliwataka wanariadha hao washiriki vizuri na washindane kwa amani kama lilivyo jina la uwanja huo wanaoshindania mashindano hayo wa Amaan, ambao uliasisiwa na Rais wa mwanzo wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Dk. Shein alisema kuwa kufanikiwa kwa mashindano hayo na kufanyika kwa vizuri huku waamuzi wakitenda haki kutaendelea kumpa hamasa ili apate kuendelea kuyaunga mkono mashindano hayo ili kufikia malengo ya serikali ya kufufua vuguvugu la michezo nchini.


Aidha, Dk. Shein aliungana na wanamichezo hao pamoja na waamuzi wa mashindano hayo kufuata viapo walivyokula mbele yake kuwa watashindana na kucheza kwa amani bila ya ugomvi na kucheza kwa amani huku waamuzi wakiahidi kutenda haki.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo,  Baraza la Michezo la Taifa la Zanzibar (BMTZ) pamoja na Wizara zote zilizosaidia kuendesha mashindano hayo.
Mapema wanariadha hao walikula kiapo kuwa watashiriki na kushindana kwa kufuata Sheria za Shirikisho la riadha la Afrika na dunia sambamba na kufuata kanuni zote zinazotawala michezo hiyo ambapo waamuzi nao waliapa kufuata sheria za Kimataifa na kanuni zote bila ya woga wala upendelea wowote huku wakiadidi zaidi kutenda haki.
Pamoja na hayo, Dk. Shein mara baada ya kumaliza kutoa salamu zake hizo kwa wanamichezo hao aliyazindua rasmi mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku mbili  terehe (26-27) Disemba mwaka huu.
Mashindano hayo yameandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa Zanzibar (BMTZ) kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA)  chini ya ufadhili wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Lengo la mashindano hayo ni kuinua mcezho wa riadha Zanzibar kuanzia vijijini, maskulini na maeneo mengine pamoja na kufufua vipaji vya wanariadha kutoka katika sehemu husika kwa lengo la kuviendeleza sambamba na kutekeleza sera ya Michezo Zanzibar.
Aidha,  lengo jengine ni pamoja na kuonesha juhudi binafsi za Dk. Shein katika kutekeleza dhamira yake ya kuona kuwa Zanzibar inarejesha hadhi yake ya asili ya ubingwa katika michezo tofauti.
 
Mashindano hayo yanawashirikisha wanariadha vijana 250 wa kike na kiume kutoka Wilaya zote kumi za Zanzibar na yatahusisha michezo yote ya riadha ikiwemo kukimbia masafa ya mita 100,200,400,800 na 1500. Pia, kurusha mkuki, kurusha tufe na kurusha kisahani.
 
Fainali za mashindano hayo zinatarajiwa kufanyika kesho jioni ambapo pia, Dk. Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
 
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar


Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.